WANAFUNZI wasichana wapatao 196 wa shule ya sekondari ya Moreto iliyopo kata ya Lugoba tarafa ya Msoga Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, wamenusurika kufa baada ya bweni lao kuteketea kwa moto jana asubuhi.


Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ametoa msaada ya magodoro 50 yenye thamani ya Sh milioni 2.2 kwa kuwa mali zote wasichana zimeteketea.


“Tumshukuru Mungu pamoja na kutokea kwa hasara ya kuteketea kwa mali, lakini hakuna madhara kwa wanafunzi yaliyotokea,” amesema Ridhiwani.


Amewapa pole walimu na wanafunzi na kuwaomba wadau wengine, kujitokeza kwenda kusaidia pale watakapojaaliwa.


Mkuu wa Shule hiyo , Justine Lyamuya, amesema, ajali hiyo ni ya Oktoba 5, asubuhi ambako walianza kuona moshi mzito katika bweni mojawapo wanaloishi wasichana wa shule hiyo.


Alisema wakati moto huo unazuka, wanafunzi hao walikuwa kwenye masomo yao darasani.


"Tulifuatilia na kukuta moto umeshashika kwenye bweni hilo na jitihada za kuuzima zilishindikana,” alisema Lyamuya na kuongeza kuwa mali zote za wanafunzi wanaolala kwenye bweni hilo zimeteketea kwa moto hivyo kwa sasa wanafanya tathmini kujua kiwango cha hasara.


Polisi mkoani Pwani inafanya uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo cha moto huo.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Boniventure Mushongi amesema, jengo hilo linatumia nishati ya umeme wa jua.


Amesema uchunguzi wa kina utafanyika kujua kiini cha kuzuka kwa moto huo.


Amesema bweni hilo linakadiriwa kuwa na wanafunzi 196.


Kamanda Mushongi amesema thamani za mali za wanafunzi zilizoteketea katika moto huo, bado haijafahamika.

Chanzo-Habarileo

Kama Una Habari,Picha,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255762 561 399

Share To:

msumbanews

Post A Comment: