Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo 2019/20 katika Ngazi ya Astashahada na Stashahada wametakiwa kuzingatia na kufuata sheria, kanuni na taratibu za Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume - Zanzibar ili waweze kusoma na kufanikiwa kwa lengo  la kulijenga Taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kampasi ya Karume, Zanzibar Dkt. Rose Mbwete wakati wa semina elekezi (orientation) kwa wanafunzi wa hao.

Dkt Mbwete amewataka wanafunzi hao kuhakikisha wanafuata taratibu zote za Chuo, pamoja na kuhakikisha  wanahudhuria vipindi darasani kikamilifu.

Wanafunzi hao pia wamekumbushwa kuwa haki zinaendana na wajibu hivyo watimize wajibu wao na uongozi wa Chuo utatimiza haki zao kwa wakati.

“Napenda niwapongeze kwa dhati na kuwakaribisha sana katika chuo chetu pia hakikisheni mnajua haki zenu na wajibu mlionao ili kuweza kuishi vizuri muda wote mtakapokuwa  hapa chuoni” alisema Dkt. Mbwete.

Dkt. Mbwete amewataka wanafunzi hao watumie vizuri fursa ya kusoma Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ili waweze kuwa mabalozi wazuri wanaporudi katika jamii na hatimaye kukiletea sifa nzuri Chuo.

“Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere bado kinaenzi lengo kuu la kuanzishwa Chuo hiki na kimerndelea  kuhakikisha katika kila kozi inayotolewa hapa mwanafunzi lazima asome uongozi, maadili, uzalendo na utawala bora ili kuandaa  Taifa bora”.

Awali kabla ya kuongea Mkuu wa Kampasi, Kaimu Naibu Mkuu wa Kampasi ya Karume anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Ndugu John Samandito aliwaasa wanafunzi kusoma kwa bidii bila kukata tamaa.

Naye Kaimu Msajili wa Kampasi ya Karume Zanzibar Dkt. Paul Mtasigazia amewataka  wanafunzi hao kuwa na maadili na kuhakikisha wanapendana na kuacha tabia ya ubaguzi wa namna yoyote ile ili waweze kuishi vizuri wawapo Chuoni.

“Hakikisheni mnaepuka kubaguana kwa makabila wala jinsi nyingine yeyote ile mkae mkijua kuwa watu wote ni sawa hivyo mheshimiane”.

Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Kampasi ya Karume Zanzibar
25/10/2019
Share To:

msumbanews

Post A Comment: