Benki ya NMB imefanikiwa kukabidhi udhamini wa vifaa vya michezo kwa ajili ya wachezaji 150 wanaotarajia kushiriki mashindano ya kimataifa ya Diplomatic Golf 2024.
Michuano hiyo inayotarajia kuanza kutimua vumbi kwa siku mbili kuanzia Septemba 21-22, 2024 katika viwanja vya Kili Golf vilivyoko Mkoani Arusha yana lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Songea Mississippi (SOMI) na klabu mwenyeji ya Kili Golf, jumla ya mashimo 36 yataamua mshindi kutoka kwa washiriki wote 150 kutoka nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na wachezaji kutoka Dubai na Marekani.
Mratibu wa mashindano hayo, Reinfrida Rwezaura, amesema kuwa maandalizi yote kuelekea mashindano hayo ya msimu wa sita mwaka huu yamekamilika.
Amesema lengo kuu la mashindano hayo ni kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia vituo vya kulelea watoto yatima na kuwasaidia wale wenye uhitaji, ikiwa ni pamoja na kusaidia wasichana wajawazito kurudi shule.
Pia mashindano haya yanatoa jukwaa la wachezaji kuonyeshana makali yao katika mchezo wa Gofu kutoka mikoa na nchi mbalimbali, pia yanatoa fursa kuonyesha ujuzi wao na nidhamu ya michezo lakini pia ya yanachangia jitihada za nchi za kukuza utalii kupitia michezo.
Kwa upande wake Meneja wa benki ya NMB, Kanda ya Kaskazini Baraka Ladislaus amesema kuwa wamedhamini jezi hizo kwa ajili ya kuvaa wachezaji ikiwemo fulana, kofia na taulo maalum za kujifutia jasho.
Amesema lengo la Benki ya NMB, kutoa udhamini huo ni kutokana na kuvutiwa na malengo yake ya kusaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
"Mbali na udhamini huu lakini Benki pia imepeleka timu kushiriki mashindano haya, kwa ajili ya kuchangamana na jamii lakini pia kuonyesha uwezo wetu kama NMB katika michezo"
Amesema kuwa wao kama Benki wanaendelea kutoa masuluhisho mbalimbali ya kifedha kwa ajili ya kusaidia jamii kutatua changamoto zao za shughuli za kiuchumi na kijamii pia.
Benki ya NMB imesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Idara ya Mashirikiano baina ya Sekta za Serikali na Sekta Binafsi (PPP) iliyopo chini ya Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakaowezesha ufadhili wa miradi ya maendeleo na ya kimkakati visiwani humo.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo visiwani Zanzibar jana, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB Juma Kimori alisema makubaliano hayo ni mwendelezo wa mkakati wa benki hiyo unaolenga kujenga thamani ya pamoja kwa wadau wake wote ikiwemo Serikali na kusisitiza kuwa makubaliano hayo yatakuwa chachu ya maendeleo endelevu ya kiuchumi visiwani Zanzibar.
“Makubaliano ambayo tumetia saini leo ni ya kimkakati na yatasaidia ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kwa lengo la kuimarisha maendeleo na uchumi wa Zanzibar. Sisi kama benki ya NMB tunatambua kuwa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ndio njia rahisi itakayosaidia kukamilisha miradi mingi kwa haraka. Tunaamini pia kuwa bila ushirikiano na sekta binafsi hatuwezi kufikia uchumi wa bluu kwa kasi inavyotakiwa,” Kimori alisema.
Aliongeza kuwa makubailiano hayo yanalenga kuimarisha miundombinu ya uwekekezaji, ili kuwajengea mazingira mazuri wawekezaji wenye nia ya kuwekeza visiwani Zanzibar nakuongeza kuwa benki yake inaamini kwa ushirikiano huo utanufaisha maelfu ya wakazi wa Zanzibar kupitia miradi mbali mbali yenye chachu ya ukuaji wa uchumi.
Kimori alibainisha kuwa Benki ya NMB itatumia mizania yake madhubuti kutoa huduma za dhamana ya zabuni kwa wananchi na makampuni yanayotaka kushiriki katika miradi mbali mbali ya kimkakati ya maendeleo visiwani Zanzibar na kuongeza kuwa benki hiyo inatoa bidha za kipekee kwa wateja wake zinazowawezesha kushiriki kikamilifu.
"Benki yetu kwa miaka mingi sasa imekuwa ikiongoza katika suala la faida na nikiri kuwa kwa sasa tuna mizania thabiti. Kutokana na mizania yetu tunatoa hadi shilingi milioni 420 kwa mkupuo kwa mkopaji mmoja ambaye anakidhi vigezo na masharti yetu,” alisisitiza.
Kimori aliongeza kuwa benki hiyo inaendelea kushirikiana na taasisi mbali mbali visiwani Zanzibar zikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Wakala wa Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ) huku akisistiza kuwa benki yake na itaendelea kufanya kazi na taasisi mbalimbali katika kufanikisha azma ya Zanzibar ya uchumi wa bluu.
Alibainisha kuwa benki hiyo itaendelea kutoa elimu ya kifedha na kubainisha kuwa zaidi ya watu 10,000 kutoka visiwani Zanzibar wanaojishughulisha na kilimo cha mwani, chumvi na tayari wamenufaika na mpango huo.
“Tunaimani kuimarika kwa uwekezaji Zanzibar kutasaidia kutoa fursa kwa vijana kupata ajira na serikali kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla,” Kimori aliongeza.
Naye Dk. Bill Kiwia, Kamishna wa Ukuzaji Uchumi na Miradi ya Mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) wakati wa hafla hiyo alisema makubaliano hayo ni ya kihostoria na kipekee huku akiongeza kuwa yatakuwa chachu ya maendeleo visiwani Zanzibar kuanzia ngazi za chini.
“Makubaliano haya ni ya kihistoria kwa kuwa yanabainisha kuwa sekta ya Umma na binafsi zinaweza kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya wananchi kwa jumla. Nimatumaini yangu kuwa miradi itakayotelelezwa kupitia makubaliano haya italeta ahueni kubwa kwa wananchi kuanzia ngazi za chini,” alisema.
Naye Mudrik Ramadhan Soraga,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar wakati wa hafla hiyo aliipongeza benki ya NMB kwa kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Zanzibar huku akisema benki hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo visiwani Zanzibar.
Soraga alisema Serikali yake chini ya Dkt. Hussein Mwinyi inaamini katika kushirikiano na sekta binafsi katika kukuza maendeleo visiwani Zanzibar na kusisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na sekta binafsi pale ambapo kuna tija na pale ambapo kuna mapungufu.
“Tumeanza mchakato wa kubainisha miradi ya kati ambapo tutashirikiana na sekta binafsi kuitekeleza. Miradi hii lazima iwe imekubalika na jamii husika na lazima iwe na lengo la kutatua changamoto zinazoikabili jamii,” alisema
Kesi ya kulawiti mwanafunzi
inayomkabili ofisa mwandamizi wa Benki ya NMB Tawi la Clock Tower jijini Arusha
,George Kifaruka {43} mkazi wa Kijenge Jijini hapa,iliyokuwa ianze kusikilizwa
leo,imeshindwa kuendelea kwa madai kwamba wakili wake ameshindwa kufika
mahakamani.
Kifaruka ambaye ni ofisa wa
mikopo wa benki hiyo alifikishwa mahakamani,Julai 27 mwaka huu 2023, na
kusomewa shitaka moja la kumweka kinyumba mwanafunzi wa kiume na kumlawiti mara
tatu nyumbani kwake.
Mbele ya Hakimu ,Heriet Marando
wa Mahakama ya wilaya ya Arusha , mshtakiwa Kifaruka aliiambia mahakama hiyo
kwamba wakili wake amepata udhuru hivyo hata weza kufika mahakamani hapo na
kuomba kesi hiyo kusogezwa mbele.
Hata hivyo mwendesha Mashitaka
wa serikali,Grace Madikenya alisema upande wa mashtaka hauna pingamizi na hoja
hiyo ndipo Hakimu Marando alipoahirisha kesi hiyo hadi Agosti 29,2023
itakapokuja kuanza kusikilizwa.
Baada ya kuahirishwa kwa kesi
hiyo mshtakiwa alitimua mbio kutoka nje ya lango kuu la kuingilia kukwepa
kupigwa picha huku akiwa anajifunika sweta na kutokomea kwenye gari jambo
lililowashangaza watu wengi waliofurika mahakamani hapo
Awali mbele ya Hakimu
Mwandamizi wa Mahakama ya wilaya ya Arusha,Heriet Marando ilidaiwa kuwa
mtuhumiwa alitenda kosa hilo julai 8 hadi 10 mwaka huu nyumba kwake Jijini
Arusha .
Madikenya alidai Mhanga ambaye
kwa sasa anahifadhiwa jina lake ,ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Olasiti
kidato cha pili na alikuwa akiishi naye kwa lengo la kumsomesha lakini alidai
fadhila kwa kumlawiti na kumharibu vibaya sehemu zake za siri.
Mtuhumiwa alikana shitaka hilo
na Mwendesha Mashitaka alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na
kuiomba mahakama kumsomea maelezo ya awali mbele ya Hakimu Marando
Katika maelezo ya awali
yaliyosomwa na Madikenya ilidaiwa kuwa mtuhumiwa ni mfanyakazi wa benki ya NMB
na mkazi wa kijenge na mhanga ni mtoto wa kiume mwanafunzi wa shule ya msingi
Olasiti Jijini Arusha na alimchukua akiwa mtoto wa mtaani akitokea mkoani Tanga
kwa lengo la kumsomesha masomo ya sekondari .
Mwendesha Mashitaka aliendelea
kudai kuwa mtuhumiwa akina na mhanga huyo nyumbani kwake kijenge alianza
kumwonyesha picha za ngono za video ili kumshawishi na baadaye alifanikiwa na
kuanza kumlawiti.
Madikenya alidai mahakamani
hapo kuwa, mhanga aligunduliwa na mmoja ya walimu katika shule hiyo baada ya
kumpatia adhabu kutokana na kosa la kuchelewa masomo na ndipo mwanafunzi huyo
alipomweleza kuwa anaishi katika mazingira magumu na alipomwita bembeni na
kumhoji zaidi ndipo alipomweleza wazi kuwa mfadhili wake anamlawiti.
Alidai baada ya kauli hiyo
Mwalimu wa shule hiyo{jina limehifadhiwa} aliamuwa kumchunguza na kumpeleka
polisi na baada ya polisi alipelekwa hospital kwa uchunguzi, na uchunguzi wa
awali wa Daktari ulibainika kuwa mhanga alishaharibika vibaya kwa kulawitiwa.
Baada ya kusomewa maelezo hayo
ya awali,mtuhumiwa alikiri jina lake,anwani yake na makazi anapoishi,pia
alikiri kumsomesha mhanga,na alikiri kukamatwa na hatimaye kufikishwa mahamani,
lakini alikana mashitaka mengine yanayomkabili.
Mwendesha mashtaka alieleza
kuwa upande wa Jamhuri utakuwa na mashahidi sita katika kesi hiyo
na vielelezo viwili na kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa agosti 10 mwaka
huu.
Hakimu Marando alimwambia
mtuhumiwa kuwa kesi hiyo ina dhamana ya watu wawili watumishi wa serikali wenye
utambulisho wa nakala ya barua kutoka kwa waajili wao lakini hadi tunakwenda
mtamboni bado mtuhumiwa alikuwa hajakamilisha taratibu za dhamana.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameipongeza benki ya NMB kwa kutenga fedha kwaajili ya mikopo ya machinga na pia kuweka huduma zitakazorahisisha utendaji kazi wa kundi hili la wafanyabiashara wadogo.
Waziri Gwajima ameyaeleza hayo alipotembelea soko la machinga la old airport jijini Mbeya na kujionea hali halisi ya Biashara za machinga katika soko hilo ambalo machinga wamehamia tangu mwaka 2020.
Mhe waziri aliipongeza benki ya NMB kwa kutenga kiasi cha Bilioni 200 kwaajili ya kuwakopesha machinga jambo ambalo litawasaidia kujikwamua kiuchumi.
Naye Mwenyekiti wa shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA), Ndugu Ernest Matondo Masanja aliishukuru Benki hiyo pia kwa kuanzisha rasmi kadi za ATM maalumu kwa machinga huku akiwasihi machinga wote nchini kuunga mkono juhudi za Benki hiyo kuwainua kiuchumi.
Lakini pia, Meneja wa Benki ya NMB kanda ya Nyanda za Juu, Straton Chilongola alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wamachinga kuwa licha ya huduma bora ambazo NMB inatoa, lakini pia, wanaweza kujikatia bima mbalimbali ikiwemo bima maalumu kwaajili ya Machinga ambayo itawafanya wafanye shughuli zao kwa kujiamini na kutokuwa na hofu kwani itokeapo janga lolote basi Bima itafidia.
Benki ya NMB imefunga mauzo ya Hati Fungani ya Jasiri (NMB Jasiri Bond) kwa mafanikio makubwa Iliyoweka rekodi ya makusanyo Afrika Mashariki na Kati ya Sh. Bil. 74.27 na kuvuka lengo la Sh. Bil. 25, ufungaji ulioenda sambamba na kuiorodhesha rasmi hati hiyo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Hafla hii ilihudhuriwa na Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu- Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru aliyemwakilisha Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, ametangaza rasmi kuorodhozeshwa kwa hati fungani ya Jasiri na sasa kuanza kununuliwa na kuuzwa kupitia soko la hisa la Dar es salaam.
Akizungumza Mafuru aliipongeza NMB kwa ubunifu chanya wa Jasiri Bond, hati fungani iliyolenga kukusanya fedha ili kutoa mikopo kwa biashara ndogo ndogo na za kati zinazo milikiwa au kuongozwa na wanawake na biashara ambazo bidhaa au huduma zake zinamgusa mwanamke moja kwa moja.
“Hii sio mara ya kwanza kwa NMB kuja na Hati Fungani na kuvuka lengo la makusanyo, hii ni mara ya nne na kwa hati hii ambayo ni ya kipekee, kama jina lake lilivyo, kumekuwa na ujasiri mkubwa sana, kwani jina Jasiri linaashiria mambo mengi sana.
“Ujasiri wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), ya kuiruhusu Hati Fungani hii kuingia sokoni kabla hata ya sheria zake hazijawa tayari, jambo linalothibitisha imani ya mamlaka hii kwa NMB ilivyokuwa kubwa.
“Lakini pia, NMB ikalenga kupata Sh. Bil. 25 na hatimaye inafunga mauzo ikiwa imepata zaidi ya mara tatu ya lengo, hii ni kuthibitisha kwamba kuna nguvu kubwa ya kiuchumi miongoni mwa wanawake, tunachotakiwa ni kuweka mazingira wezeshi ya kuwaamini kama wenzetu NMB walivyofanya,” alisisitiza Mafuru.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema NMB ilipokea maombi 1,630 yaliyowezesha kukusanya Sh. Bil. 74.27 badala ya Bil. 25 na kuwashukuru wateja na wawekezaji wote kwa kuiamini benki hio.
“Kuaminika kwa NMB katika hili kunathibitishwa na kuwa asilimia 96 ya waliotuma maombi ya kununua Hati Fungani, yamepitia katika matawi yetu, huku asilimia 4 tu yakifanyika kupitia Madalali wa Soko la Hisa waliosajiliwa”.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA), Nicodemus Mkama, aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa NMB, kwa kufanikisha uuzwaji wa ‘Jasiri Bond’ kwa Umma wa Watanzania na hatimaye kufikia hatua ya kuiorodhesha DSE, tayari kwa mauzo ya walionunua na manunuzi ya waliokosa katika mchakato uliofungwa.
Wengine waliohudhuria hafla hii ni Mkurugenzi Mkuu WA DSE, Moremi Marwa, pamoja na wawakilishi kutoka FSD Africa, Ubalozi wa Uingereza, International Finance Co-operation (IFC), UN Women na Orbit Securities Ltd.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Maalum Benki ya NMB, Getrude Mallya akimakabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh.milioni 25.5 Mwenyekiti wa Klabu ya Golf ya Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Michael Luwongo ikiwa ni udhamini wa Mashindano ya Mchezo wa Golf ya Mkuu wa Majeshi 'NMB CDF Trophy 2021'. Kulia ni Meneja wa Club ya Golf ya Lugalo, Luteni Kanali, Frank Kaluwa na Meneja Mwandamizi Wateja Maalum wa NMB, Emmanuel Mahodanga wakishuhudia. Benki ya NMB imetoa takribani milioni 60 kwa ajili ya udhamini wa mashindano hayo kiujumla kwa mwaka huu.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Maalum Benki ya NMB, Getrude Mallya (katikati) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) kwenye hafla ya kupokea mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 25.5 kwa ajili ya udhamini wa Mashindano ya Mchezo wa Golf ya Mkuu wa Majeshi 'NMB CDF Trophy 2021'. Kulia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Golf ya Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo pamoja na Meneja Mwandamizi Wateja Maalum wa NMB, Emmanuel Mahodanga (kulia) wakishuhudia.
Benki ya NMB imetoa Sh. 60 Milioni kwa ajili ya kudhamini Mashindano Maalumu ya mchezo wa Gofu ya Mkuu wa Majeshi (CDF ) ambayo yanatarajia kuanza Septemba 17 hadi 19 kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu vya Lugalo Jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo hufanyika kila mwaka lengo kuu ni kuuinua mchezo huo pamoja na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi ili kuja kuwa tegemezi siku zijazo.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi hundi Mkuu wa kitengo cha wateja maalumu wa NMB, Getrude Mallya, alisema wanajisikia furaha kuwa sehemu ya kufanikisha kufanyika kwa shindano hilo ambalo anaamini mwaka huu litafana kutokana na zawadi nono ambazo zimeandaliwa kwa washindi.
Mallya alisema kiasi hicho cha fedha kimetumika katika kununua vifaa mbalimbali vitakavyo tumiwa na washiriki wa shindano hilo ikiwemo fulana, kofia, bendera na zawadi za washindi ambazo zitatolewa siku ya mwisho.
“Sisi kama NMB tunajisikia furaha kuona shindano la mwaka huu linakwenda kufanyika kwa ubora na mafanikio ya juu kabisa nahii inathibitisha kwamba sisi ndio Benki ambayo inaijali jamii kwa ukaribu kutokana na kudhamini masuala mbalimbali ikiwo ya kimichezo,” alisema Mallya
Meneja huyo pia aliupongeza uongozi wa klabu ya Lugalo, kwa imani yao kwao na kuendeleza mchezo wa Gofu nchini kwa juhudi kubwa wanazozifanya za kuanzisha mashindano mbalimbali na kuwachagua wao kushirikiana nao kuyadhamini.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa klabu ya Gofu ya Lugalo Michael Luwango, alisema zaidi ya wachezaji 170, wanatarajia kushiriki mashindano ya mwaka huu ikiwemo vijana wadogo wa shule (Junior) ambao wao ndio watakao fungua mashindano hayo siku ya kwanza Septemba 17.
Alisema tofauti na miaka mingine mwaka huu wametoa nafasi ya watu mbalimbali kushiriki michuano hiyo wakiwemo watu binfsi na wachezaji wakulipwa pamoja na wageni endapo watajisikia kushiriki.
Kiongozi huyo alisema mpaka sasa mwitikio kwa watu wanaoomba kushiriki ni mkubwa ambapo zaidi ya watu 100 wameshathibitisha ushiriki wao na maandalizi yanakwenda vizuri ikiwemo ubora wa viwanja ambavyo vitatumika kwenye shindano hilo.
Naye Katibu wa Chama cha Gofu Tanzania Boniface Nyiti, alisema shindano hilo la Mkuu wa Majeshi lipo kwenye kalenda ya TGU na limekuwa na mchango mkubwa kwa taifa kutokana na kutoa wacheaji wengi ambao wanajenga timu ya taifa.
Nyiti aliwataka viongozi wa klabu za mchezo huo wanaoanzisha mashindano mengine kipindi ambacho shindano la Mkuu wa Majeshi linafanyika watawachukulia hatua ikiwemo kuwafungia kutoshiriki mchezo huo kwa kufuata sheria kwani kufanya hivyo nikuwanyima fursa wachezaji kuto onesha uwezo wao.
Mpaka sasa zaidi ya klabu 10 kutoka mikoa tofauti imethibitisha kushiriki michuano hiyo baadhi yao ni Morogoro, Zanzibar, Arusha, Moshi, Dar es Salaam Gymkhana Klubu na Lugalo .
Mkazi wa mkoani Morogoro katika Kijiji cha Kinore, Abdallah Mohmed Abdallah akionyesha mfano wa Funguo wa Gari aina ya Fortuner aliyojishindia kwenye Promosheni ya Bonge la Mpango iliyokuwa inaendesha na Benki ya NMB baada ya kukabidhiwa rasmi gari yake na Kaimu Afisa Mkuu Ukaguzi wa Ndani wa NMB, Benedicto Baragomwa wakati wa hafla iliyofanyika mkoani Morogoro
Furaha ya Ushindi kwa Familia. Mshindi wa Gari aina ya Fortuner, Abdallah Mohmed Abdallah akifurahia na mke wake, Khadija Hussein muda mfupi baada ya kukabidhiwa rasmi gari waliyoshinda na Kaimu Afisa Mkuu Ukaguzi wa Ndani wa NMB, Benedicto Baragomwa.
Mshindi wa Gari aina ya Fortuner kwenye Promosheni ya Kampeni ya Bonge la Mpango, Abdallah Mohmed Abdalla iliyokuwa inaendeshwa na Benki ya NMB akikabidhiwa mfano wa Funguo na Kaimu Afisa Mkuu Ukaguzi wa Ndani wa NMB, Benedicto Baragomwa katika hafla ya kukabidhi zawadi ya mshindi wa jumla wa promosheni ya Bonge la Mpango iliyofanyika mkoani Morogoro. wa kwanza kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya Mashariki, Dismas Prosper na Meneja Mwandamizi wa Idara ya Wateja Binafsi – Isaac Mgwasa.
Promosheni ya Benki ya NMB ya “Bonge la Mpango” imemalizika rasmi Jumatano wiki hii kwa mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Bw Abdallah Mohammed, kukabidhiwa zawadi nono ya gari la kifahari aliloshinda lenye thamani ya TZS million 169.
Gari hilo aina ya Toyota Fortuner alilolinyakua mshindi huyo kutoka kijiji cha Kinole ni jpya kabisa ambalo lilianza kutembea kilomita zake za kwanza jana baada ya Bw Abdallah kuiendesha familia yake kuelekea nyumbani mara shughuli ya makabidhiano ilipoisha.
“Hatimaye sasa nimeamini kabisa kuwa mimi ndiye kweli mshindi wa zawadi kubwa ya shindano hili ingawa nilipata taarifa ya ushindi wangu katikati ya mwezi jana,” mwanakijiji huyo mwenye umri wa miaka 50 na mzazi wa watoto watano alisema baada ya kuliwasha gari hilo la kisasa kwa mbwebwe za kiushindi.
Akitabasamu kwa furaha mkulima huyo ambaye pia ni mfanyabiashara alisema mpaka anakbidhiwa rasmi zawadi hiyo aliuchukulia ushindi wake kama ndoto kwa sababu kadhaa.
“Kwanza niliona uwezekano wa mimi kuishinda hii zawadi kubwa kama ndoto za alinacha. Pamoja na kuwa mteja mwaminifu wa NMB, kwanza mimi ni mwanakijiji harafu mfanyabiashara mdogo tu wakati benki hii ina zaidi ya wateja zaidi ya milioni nne wakiwemo matajiri wakubwa,” alifafanua.
“Ushindi wangu umenifunza jambo jingine kubwa kuhusu NMB. Kumbe ni benki ya kila Mtanzania bila kujali hadhi yake katika jamii na kiuchumi. Sizingekuwepo huduma za kibenki za kimtandao wala nisingekuwa hata mteja wake acha kuinyakua hii zawadi,” Bw Abdallah aliongeza kwa kicheko cha ushindi.
Aidha ameipongeza taasisi hiyo ya fedha kubwa kuliko zote kwa mikakati yake wezeshi kama kampeni ya Bonge la Mpango ambayo uzinduzi wake mwanzoni mwa mwaka huu
kuliweka viwango vipya kwa promosheni kutokana na zawadi zake lukuki zilizokuwa na thamani ya zaidi ya TZS million 500.
Alisema zawadi walizopata washindi zilikuwa pia ni mitaji hasa kwa watu wa kawaida na wajasiriamali wadogo kama yeye. Ili kuimarisha uhusiano na NMB, Bw Abdallah alisema anaenda kuwa miongoni mwa mawakala zaidi ya 9,000 wa benki hiyo.
Akizungumza kabla ya kumkabidhi zawadi yake kwenye Soko Kuu la Kingalu karibu na tawi la NMB la Wami, Kaimu Afisa Mkuu wa Ukaguzi wa Ndani wa benki hiyo, Bw Benedicto Baragomwa, alisema zawadi zilizonyakuliwa ni pamoja na pesa taslimu walizoshinda wateja 120. Nyingine ni pikipiki za miguu mitatu 24 aina ya LIFAN na Kirikuu tatu za muundo wa TATA Ace.
Pia NMB ilifanya uwekezaji huo kwa ajili ya kutambua mchango wa wateja katika mafanikio yake ikiwemo kuandika historia katika tasnia ya kibenki kwa kupata faida kubwa kuwahi kutengenezwa na benki nchini ya TZS bilioni 206 mwaka 2020.
“Mwezi Februari tulizindua kampeni maalumu yenye makusudi ya kurejesha faida kwa wateja pamoja na kuhamasisha utamaduni wa kujiwekea akiba kwa Watanzania, Bw Baragomwa alisema.
“Leo ndo tumefikia kilele cha Bonge la Mpango…Kampeni hii ya miezi mitatu ililenga kuwahamasisha wasio na akaunti ya benki nchini kuja kufungua na kutunza akiba zao kwa njia salama zaidi na Benki ya NMB,” aliongeza.
Meneja wa Tawi la Uluguru, Bi Lilian Abraham, alisema ana sababu kubwa mbili za kufurahia ushindi wa Bw Abdallah ambazo ni mshindi huyo kuwa mwanakijiji na kubwa zaidi kuwa mteja wa tawi lake ambapo ndipo kampeni ya Bonge la Mapngo ilipozinduliwa katika kanda ya Pwani.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna
Benki inayoongoza nchini Tanzania, NMB imeendeleza ufanisi wake kiutendaji katika robo ya kwanza ya mwaka 2021. Faida ya benki kabla ya kodi imeongezeka kwa asilimia 34 na kufikia shilingi Bilioni 93 wakati faida baada ya kodi imeongezeka kwa asilimia thelathini na tatu (33%) na kufika Shilingi bilioni 65 katika robo iliyoishia Machi 31 mwaka 2021.
Ufanisi huu umetokana na ongezeko la mapato, udhibiti wa gharama za uendeshaji, na umakini katika utoaji wa mikopo.
Mapato yaliongezeka kwa ailimia kumi na sita ( 16% ) na kufika shilingi bilioni 224 ikilinganishwa na shilingi bilioni 193 za robo ya kwanza mwaka 2020. Mapato hayo yalichangiwa na ongezeko la pato halisi la riba lililotokana na faida ya mikopo na ile ya kwenye amana za Serikali.
Vilevile, mapato yasiyotokana na riba yaliongezeka kwa 10% kutokana na ongezeko uimarishaji wa utoaji suluhishi za kibenki kwa njia ya kidijitali.
Benki bado ina ufanisi wa kutosha. Utekelezaji wa mikakati ya kupunguza gharama za uendeshaji unaendelea kutoa matokeo chanya kwani uwiano wetu wa gharama na mapato umeimarika mpaka 48% katika robo ya kwanza mwaka 2021 kutoka 52% katika robo ya kwanza mwaka 2020, chini ya kiwango kilichowekwa na msimamiszi wa mabenki yaani Benki Kuu ya Tanzania cha asilimia hamsini tano (55%).
Benki itaendelea kutekeleza mikakati ya kupunguza gharama na kuongeza ufanisi kwa mujibu wa malengo makuu ya kimkakati ya Benki huku tukiendelea kuwahudumia vyema wateja wetu.
Ubora wa mali zetu umeimarika kutokana na utoaji bora wa mikopo, kutathmini uwekezaji tunaofanya na juhudi za kukusanya madeni. Hii imesaidia kupunguza madeni sugu na tengo la mikopo isiyolipika kuongezeka kwa 5% na kushusha kiwango cha mikopo chechefu mpaka 5% hivyo kuwa ndani ya ukomo wa kikanuni kutoka 6.9% iliyokuwapo mwaka uliopita.
Mizania ya Benki imeendelea kuwa mizuri na imara na juhudi zetu za kuwafikia wananchi wengi zaidi. Mikopo ya benki iliongezeka kwa 11%.
Ubunifu wa huduma na bidhaa zinazokidhi matarajio ya wateja umechangia kuongeza amana za wateja kwa 9% na kufika TZS 5.3 trilioni katika robo ya kwanza mwaka 2021 kutoka TZS 4.8 trilioni katika robo ya kwanza mwaka 2020. Tunaendelea kuweka msisitizo katika ukopeshaji makini na endelevu tunapoianza robo ya pili mwaka 2021.
Katika kipindi hicho, tuliimarish amtaji wetu na kuufanya uwiano wa mtaji msingi kufika 19.61% kutoka 17.8% katika robo ya kwanza mwaka 2020, na uwiano wa mtaji wa ziada kufika 20.4% kutoka 18.5% wa robo ya kwanza mwaka 2020, hivyo yote miwili kuwa juu ya mahitaji ya kikanuni.
Akizungumzia ufanisi na uimara wa Benki, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna alisema “Tumeanza vizuri. Tunahakikisha ongezeko la thamani kwa wanahisa wetu na nchi kwa ujumla. Matokeo haya ya Q1 yanaakisi uwezo wa kuendelea vyema huko mbele katika utekelezaji wa mikakati yetu kwa kutumia wafanyakazi wetu wanaojitoa kuhudumia wateja wetu kwa ufanisi mkubwa”.
Ruth Zaipuna aliongeza, “Mtaji wetu bado ni mkubwa na unatupatia nafasi ya kuendelea kukua kama benki na kuongeza thamani kwa wanahisa na wateja wetu. Kutokana na msiingi imara tuliyo nayo, na kuimarika kwa matarajio ya uchumi wa dunia, tunaamini tutaendelea kukua katika robo ya pili ya mwaka.Tunawashukuru wateja wetu, wanahisa na wafanyakazi kutokana na matokeo haya mazuri ya robo mwaka. Tutaendelea kuzitumia fursa zilizo mbele yetu ipasavyo ili kuendelea kuwa Benki yenye ufanisi zaidi nchini.”
Wanafunzi
wa kidato cha Nne Shule ya Sekondari Semkiwa wilaya ya Korogwe mkoa wa
Tanga wakiwa wamekalia meza na viti zilizotolewa msaada na benki ya NMB
ikiwa ni sehemu ya benki hiyo kurejesha faida kwa jamii. Aliyesimama ni
Mkuu wa Shule hiyo Bi. Deborah Singu.
Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya Walimu Wakuu katika shule za sekondari na msingi Kanda ya
Kaskazini wamevutiwa na utaratibu wa misaada wanaopata kutoka Benki ya
NMB, kwa kuwa imekuwa na mguso mkubwa kwenye maendeleo ya elimu nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walimu hao kutoka mkoa wa Tanga,
Kilimanjaro na Arusha wameeleza namna misaada kutoka NMB ilivyofika kwa
wakati na kuwa sehemu ya mabadiliko kwenye kujifunza na kuwasaidia
wazazi jukumu la kupatikana madawati, madarasa na vifaa vya
kufundishia.
Ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kurudisha kwa jamii asilimia moja ya
faida inayopatikana kwa mwaka wa fedha, NMB wamekuwa na mfuko maalum
ambao husaidia elimu, majanga na huduma za afya ambapo baada ya
kukabidhi vifaa hivyo timu maalum huzunguka kuangalia ikiwa walengwa
wamefikiwa na misaada husika.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msambiazi wilayani Korogwe Mkoa wa
Tanga, Selemani Kombo alisema shule yake ufaulu umeongezeka baada ya
kupata msaada wa kumalizia darasa na ofisi ya walimu.
“Mgekuja miezi kadhaa kabla ya leo (Machi, 2021) mgeshuhudia maajabu
sana, maana kwa kweli shule hii ilikuwa na hali mbaya kwa upande wa
ofisi ya walimu, hata baadhi ya madarasa hayakuwa hivi mnavyoyaona,”
alisema Mwalimu Kombo na kuongeza:
“Tulikuwa na kikao cha wazazi na viongozi wa shule, ndipo tulipopata
taarifa kuwa Benki ya NMB inatoa misaada ya vifaa vya kuezekea na
madawati, tukasema sisi shida yetu ni vifaa vya kuezekea. Ashanteni sana
tulipokea mabati na mbao za kuezekea, tunashukuru fedha ambazo
tulipanga kuzitumia kuezeka tulizielekeza kwenye kupaka rangi na vifaa
vingine hadi jengo likakamilika.”
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Semkiwa iliyopo
Korogwe, Deborah Singu akizungumzia msaada wa viti 55 na meza zake,
alisema msaada huo umewaonyesha namna wanafunzi wao walivyokuwa na kiu
ya kukaa sehemu nzuri.
“Kwanza niwahakikishie msaada tumeupokea kama tulivyoomba, kimsingi
hivi viti na meza ni imara sana hata waafunzi wanavigombania. Cha
kufurahisha hawa wanafunzi wa kidato cha nne baada ya kuona darasa lao
ni zuri waliamua kuchangishana wakanunua saa ya ukutani ili wawe wa
kipekee,” alisema Mwalimu Singu.
Naye Mwalimu wa Taaluma shuleni hapo, Mwalimu Bashir Abdu alisema kwa
kiasi kikubwa shule yao ya Sekondari Semkiwa imekuwa na mabadiliko
makubwa kitaaluma baada ya wanafunzi kupata nafasi nzuri za kukaa
madarasani.
“Awali hata utoro ulikuwa mkubwa, mwanafunzi akija akikosa sehemu ya
kukaa anatafuta sababu ya kutoroka shule, kesho pia haji. Lakini viti
hivi vimewapa hata hamu ya kusoma kwanza vinavutia haka kuvitazama tu.
Kwa kweli NMB ahsanteni sana mmetukomboa,” alisema Mwalimu Abdu.
Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Korogwe, Lugano Mwampeta alisema
utaratibu wa kurudisha kiasi kidogo kinachopatikana kwenye faida ya
benki hiyo inampa wepesi wa kupata wateja wengi, kwa kuwa namna jamii
inavyoguswa na misaada hiyo huwajengea imani kuwa Benki ni NMB.
“Huwa tunapokea maombi mengi sana, hii inaonyesha ni kwa namna gani
benki yetu inaaminiwa. Lakini pia hawa wanafunzi pamoja na walimu ni
fursa nzuri si tu kibiashara bali hata kijamii kwa sababu sisi hatufanyi
tu bishara lakini lazima tutoe huduma za kijamii kwa kuwa tunaishi
nao,” alisema Mwampeta.
Aidha, kiasi cha zaidi ya Shilingi Bilioni 2 kimetengwa kwa mwaka huu
wa fedha kwa ajili ya kurudisha kwa jamii, ambapo NMB inatoa huduma za
kifedha na bidhaa kwa wateja binafsi, wakulima, wafanyabiashara ndogo,
kati na wakubwa, taasisi pamoja na serikali.
Ina matawi 225, zaidi ya mawakala 8,000 (NMB Wakala), ATM zaidi ya
800 nchi nzima na imefika katika kila wilaya. NMB ina wateja zaidi ya
milioni tatu na wafanyakazi zaidi ya 3,400.
Katika ziara hiyo ya kutembelea vituo vilivyonufaika na mradi wa CSR
kutoka NMB, maofisa hao walitembelea shule za msingi, sekondari na chuo
kimoja cha Polisi (CCP) pamoja na vituo vya afya ikiwemo Hospitali za
Wilaya katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kwa Kanda ya Kaskazini ya
NMB.