Na Mwandishi Wetu,Arusha

 

Kesi ya kulawiti mwanafunzi inayomkabili ofisa mwandamizi wa Benki ya NMB Tawi la Clock Tower jijini Arusha ,George Kifaruka {43} mkazi wa Kijenge Jijini hapa,iliyokuwa ianze kusikilizwa leo,imeshindwa kuendelea kwa madai kwamba wakili wake ameshindwa kufika mahakamani.

Kifaruka ambaye ni ofisa wa mikopo wa benki hiyo alifikishwa mahakamani,Julai 27 mwaka huu 2023, na kusomewa shitaka moja la kumweka kinyumba mwanafunzi wa kiume na kumlawiti mara tatu nyumbani kwake.

Mbele ya Hakimu ,Heriet Marando wa Mahakama ya wilaya ya Arusha , mshtakiwa Kifaruka aliiambia mahakama hiyo kwamba wakili wake amepata udhuru hivyo hata weza kufika mahakamani hapo na kuomba kesi hiyo kusogezwa mbele.

Hata hivyo mwendesha Mashitaka wa serikali,Grace Madikenya alisema upande wa mashtaka hauna pingamizi na hoja hiyo ndipo Hakimu Marando  alipoahirisha kesi hiyo hadi Agosti 29,2023 itakapokuja kuanza kusikilizwa.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo mshtakiwa alitimua mbio kutoka nje ya lango kuu la kuingilia kukwepa kupigwa picha huku akiwa anajifunika sweta na kutokomea kwenye  gari jambo lililowashangaza watu wengi waliofurika mahakamani hapo

Awali mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya wilaya ya Arusha,Heriet Marando ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo julai 8 hadi 10 mwaka huu nyumba kwake Jijini Arusha .

Madikenya alidai Mhanga ambaye kwa sasa anahifadhiwa jina lake ,ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Olasiti kidato cha pili na alikuwa akiishi naye kwa lengo la kumsomesha lakini alidai fadhila kwa kumlawiti na kumharibu vibaya sehemu zake za siri.

Mtuhumiwa alikana shitaka hilo na Mwendesha Mashitaka alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba mahakama kumsomea maelezo ya awali mbele ya Hakimu Marando

Katika maelezo ya awali yaliyosomwa na Madikenya ilidaiwa kuwa mtuhumiwa ni mfanyakazi wa benki ya NMB na mkazi wa kijenge na mhanga ni mtoto wa kiume mwanafunzi wa shule ya msingi Olasiti Jijini Arusha na alimchukua akiwa mtoto wa mtaani akitokea mkoani Tanga kwa lengo la kumsomesha  masomo ya sekondari .

Mwendesha Mashitaka aliendelea kudai kuwa mtuhumiwa akina na mhanga huyo nyumbani kwake kijenge alianza kumwonyesha picha za ngono za video ili kumshawishi na baadaye alifanikiwa na kuanza kumlawiti.

Madikenya alidai mahakamani hapo kuwa, mhanga aligunduliwa na mmoja ya walimu katika shule hiyo baada ya kumpatia adhabu kutokana na kosa la kuchelewa masomo na ndipo mwanafunzi huyo alipomweleza kuwa anaishi katika mazingira magumu na alipomwita bembeni na kumhoji zaidi ndipo alipomweleza wazi kuwa mfadhili wake anamlawiti.

Alidai baada ya kauli hiyo Mwalimu wa shule hiyo{jina limehifadhiwa} aliamuwa kumchunguza na kumpeleka polisi na baada ya polisi alipelekwa hospital kwa uchunguzi, na uchunguzi wa awali wa Daktari ulibainika kuwa mhanga alishaharibika vibaya kwa kulawitiwa.

Baada ya kusomewa maelezo hayo ya awali,mtuhumiwa alikiri jina lake,anwani yake na makazi anapoishi,pia alikiri kumsomesha mhanga,na alikiri kukamatwa na hatimaye kufikishwa mahamani, lakini alikana mashitaka mengine yanayomkabili.

Mwendesha mashtaka alieleza kuwa  upande wa Jamhuri utakuwa na  mashahidi sita katika kesi hiyo na vielelezo viwili na kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa agosti 10 mwaka huu.

Hakimu Marando alimwambia mtuhumiwa kuwa kesi hiyo ina dhamana ya watu wawili watumishi wa serikali wenye utambulisho wa nakala ya barua kutoka kwa waajili wao lakini hadi tunakwenda mtamboni bado mtuhumiwa alikuwa hajakamilisha taratibu za dhamana.

 

Share To:

Post A Comment: