Na OWM – TAMISEMI, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Bw. Sospeter Mtwale, ameongoza kikao kazi kati ya ofisi yake na Shirika lisilo la Kiserikali la World Vision Tanzania, kilicholenga kujadili Mkakati wa Jubilee 2026–2030 uliowasilishwa na World Vision Tanzania wa kuboresha ustawi wa watoto nchini.

Mkakati huo uliofanyika leo Julai 29, 2026 unalenga kuwafikia watoto moja kwa moja kupitia programu za afya, lishe, elimu, ulinzi wa mtoto, huduma za maji safi na usafi wa mazingira (WASH), pamoja na kuimarisha kipato cha kaya. 

Akifafanua kuhusu lengo la mkakati huo, Mkurugenzi wa Ubora na Mikakati wa World Vision Tanzania Bw. Simon Moikan amesema, mpango huo  unakusudia kushughulikia changamoto tatu zinazoendelea kuathiri mamilioni ya watoto nchini ambazo ni utapiamlo, utoro wa shule na ukatili dhidi ya watoto.

Mara baada ya Mkakati huo kuwasilishwa, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale alitoa fursa kwa wataalamu kutoka idara mbalimbali za Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI zinazoshughulikia masuala ya ustawi wa watoto pamoja na wataalamu kutoka World Vision Tanzania, kujadiliana kuhusu namna bora ya kuratibu ushirikiano katika utekelezaji wa mkakati huo iwapo mamlaka itaridhia, pindi utakapowasilishwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa hatua za uidhinishaji.

Majadiliano hayo  yanaakisi dhamira ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha watoto wa Tanzania wanapata huduma bora na mazingira salama yanayowezesha ukuaji, maendeleo na ustawi wao.
















Share To:

Post A Comment: