Wanafunzi wa kidato cha Nne Shule ya Sekondari Semkiwa wilaya ya Korogwe mkoa wa Tanga wakiwa wamekalia meza na viti zilizotolewa msaada na benki ya NMB ikiwa ni sehemu ya benki hiyo kurejesha faida kwa jamii. Aliyesimama ni Mkuu wa Shule hiyo Bi. Deborah Singu.

Na Mwandishi Wetu

BAADHI ya Walimu Wakuu katika shule za sekondari na msingi Kanda ya Kaskazini wamevutiwa na utaratibu wa misaada wanaopata kutoka Benki ya NMB, kwa kuwa imekuwa na mguso mkubwa kwenye maendeleo ya elimu nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walimu hao kutoka mkoa wa Tanga, Kilimanjaro na Arusha wameeleza namna misaada kutoka NMB ilivyofika kwa wakati na kuwa sehemu ya mabadiliko kwenye kujifunza na kuwasaidia wazazi  jukumu la kupatikana madawati, madarasa na vifaa vya kufundishia.

Ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kurudisha kwa jamii asilimia moja ya faida inayopatikana kwa mwaka wa fedha, NMB wamekuwa na mfuko maalum ambao husaidia elimu, majanga na huduma za afya ambapo baada ya kukabidhi vifaa hivyo timu maalum huzunguka kuangalia ikiwa walengwa wamefikiwa na misaada husika.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msambiazi wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga, Selemani Kombo alisema shule yake ufaulu umeongezeka baada ya kupata msaada wa kumalizia darasa na ofisi ya walimu.

“Mgekuja miezi kadhaa kabla ya leo (Machi, 2021) mgeshuhudia maajabu sana, maana kwa kweli shule hii ilikuwa na hali mbaya kwa upande wa ofisi ya walimu, hata baadhi ya madarasa hayakuwa hivi mnavyoyaona,” alisema Mwalimu Kombo na kuongeza:

“Tulikuwa na kikao cha wazazi na viongozi wa shule, ndipo tulipopata taarifa kuwa Benki ya NMB inatoa misaada ya vifaa vya kuezekea na madawati, tukasema sisi shida yetu ni vifaa vya kuezekea. Ashanteni sana tulipokea mabati na mbao za kuezekea, tunashukuru fedha ambazo tulipanga kuzitumia kuezeka tulizielekeza kwenye kupaka rangi na vifaa vingine hadi jengo likakamilika.”

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Semkiwa iliyopo Korogwe, Deborah Singu akizungumzia msaada wa viti 55 na meza zake, alisema msaada huo umewaonyesha namna wanafunzi wao walivyokuwa na kiu ya kukaa sehemu nzuri.

“Kwanza niwahakikishie msaada tumeupokea kama tulivyoomba, kimsingi hivi viti na meza ni imara sana hata waafunzi wanavigombania. Cha kufurahisha hawa wanafunzi wa kidato cha nne baada ya kuona darasa lao ni zuri waliamua kuchangishana wakanunua saa ya ukutani ili wawe wa kipekee,” alisema Mwalimu Singu.

Naye Mwalimu wa Taaluma shuleni hapo, Mwalimu Bashir Abdu alisema kwa kiasi kikubwa shule yao ya Sekondari Semkiwa imekuwa na mabadiliko makubwa kitaaluma baada ya wanafunzi kupata nafasi nzuri za kukaa madarasani.

“Awali hata utoro ulikuwa mkubwa, mwanafunzi akija akikosa sehemu ya kukaa anatafuta sababu ya kutoroka shule, kesho pia haji. Lakini viti hivi vimewapa hata hamu ya kusoma kwanza vinavutia haka kuvitazama tu. Kwa kweli NMB ahsanteni sana mmetukomboa,” alisema Mwalimu Abdu.

Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Korogwe, Lugano Mwampeta alisema utaratibu wa kurudisha kiasi kidogo kinachopatikana kwenye faida ya benki hiyo inampa wepesi wa kupata wateja wengi, kwa kuwa namna jamii inavyoguswa na misaada hiyo huwajengea imani kuwa Benki ni NMB.

“Huwa tunapokea maombi mengi sana, hii inaonyesha ni kwa namna gani benki yetu inaaminiwa. Lakini pia hawa wanafunzi pamoja na walimu ni fursa nzuri si tu kibiashara bali hata kijamii kwa sababu sisi hatufanyi tu bishara lakini lazima tutoe huduma za kijamii kwa kuwa tunaishi nao,” alisema Mwampeta.

Aidha, kiasi cha zaidi ya Shilingi Bilioni 2 kimetengwa kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kurudisha kwa jamii, ambapo NMB inatoa huduma za kifedha na bidhaa kwa wateja binafsi, wakulima, wafanyabiashara ndogo, kati na wakubwa, taasisi pamoja na serikali.

Ina matawi 225, zaidi ya mawakala 8,000 (NMB Wakala), ATM zaidi ya 800 nchi nzima na imefika katika kila wilaya. NMB ina wateja zaidi ya milioni tatu na wafanyakazi zaidi ya 3,400.

Katika ziara hiyo ya kutembelea vituo vilivyonufaika na mradi wa CSR kutoka NMB, maofisa hao walitembelea shule za msingi, sekondari na chuo kimoja cha Polisi (CCP) pamoja na vituo vya afya ikiwemo Hospitali za Wilaya katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kwa Kanda ya Kaskazini ya NMB.

Share To:

Post A Comment:

Back To Top