Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt.Mosses Kusiluka amesema kuwa serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Raisi Daktari Samia Suluhu Hassan imeipa kipaumbele cha kwanza sekta ya TEHAMA nchini kwa kuendeleza mifumo mbalimbali na kuhakikisha huduma zinapatikana kirahisi.
Katika kufanikisha hilo pia serikali imeendelea kuwekeza katika sekta hiyo na kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuweka rekodi nzuri ya kutambuliwa kimataifa katika kutoa huduma nzuri ya serikali mtandao.
Ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Sita cha Serikali Mtandao (eGA) kinachoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC) mkoani Arusha.
"Kuwepo kwangu hapa leo ni kuonyesha umuhimu wa serikali ya awamu ya Sita ambayo imeipa umuhimu wa kipekee TEHAMA,Mheshimiwa Raisi wetu Daktari Samia Suluhu Hassan anaishi TEHAMA na anaitumia kwa kiasi ambacho watu wengi hawawezi kufahamu kwahiyo TEHAMA ni kipaumbele cha kwanza kwenye Utekelezaji wa Ajenda ya serikalimtandao"Alisisitiza Balozi Kusiluka
Aidha amesema kuwa Tanzania ni nchi yenye mafanikio makubwa duniani kwenye matumizi ya TEHAMA,hatua kubwa imepigwa na mafanikio ya eGa ni kielelezo kizuri cha azma ya serikali kutumia teknolojia kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi hali ambayo inapelekea huduma kupatikana kwa wakati.
Nae Mhandisi Benedict Ndomba ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) amesema kuwa kikao hicho ni muhimu kwa kuwa kitakuja na maazimio ya pamoja ya kuboresha huduma ya serikali mtandao, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi na kujenga serikali mtandao.
Mhandisi Ndomba amewahikikishia washiriki eGA itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa kuendelea kuijenga serikali Mtandao.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Daktari Mussa Kissaka amesema kuwa serikali ilianzisha mamlaka hiyo ili kuratibu na kusimamia jitihada za serikali mtandao pamoja na kuhakikisha kuwa uzingatiaji wa sera,sheria,kanuni na miongozo na viwango ya serikali mtandao kupitia taasisi za umma huku lengo likiwa ni kujenga serikali mtandao kupitia teknolojia za kisasa kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Jumla ya washiriki 1400 wanashiriki mkutano huo ambao unajumuisha wadau mbali mbali kutoka serikalini na sekta binafsi kwa lengo la kuboresha serikali mtandao.










Post A Comment: