Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu  Mkoani Arusha kuanzia Februari 22-24, 2026,akitokea mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake leo Jumamosi Februari 21, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Gabriel Makalla amesema Mhe. Waziri Mkuu kesho Jumapili ataweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa bweni la kisasa la Chuo kikuu cha Kimataifa cha sayansi cha Nelson Mandela,kisha  kukagua upanuzi wa Miundo mbinu ya Hospitali ya Oltrumet pamoja na kuzungumza na wananchi eneo la Ngaramtoni.

"Tarehe 23, Mhe. Waziri Mkuu atakuwa Wilaya ya Longido na atatembelea na kupokea taarifa ya mradi mkubwa wa maji Kata ya Sinya, atazindua mradi wa Upanuzi wa shule ya Sekondari Sinya iliyopanuliwa na kuwa na Kidato cha tano na sita na baadae kutembelea kituo cha utoaji wa huduma za Pamoja (One stop Border Post), Namanga na kisha kuzungumza na wananchi kwenye Viwanja vya shule ya msingi Namanga." Amesema CPA Makalla.

Mhe. Makalla  ametumia fursa hiyo kuwaalika wananchi wote kushiriki katika ziara hiyo,ambapo  amesema kwa siku ya tatu Mhe. Waziri Mkuu atafanya ziara yake Wilaya ya Arusha akitarajiwa kukagua maendeleo ya Ujenzi wa kituo Kikuu cha mabasi Jiji la Arusha eneo la Bondeni City, na kisha kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa soko la Kilombero pamoja na kuzungumza na wananchi kupitia Mkutano wa hadhara kwenye eneo hilo la soko Jijini Arusha.

"Naomba niwaalike waananchi wote wa mkoa wa Arusha kuhudhuria kwa wingi katika ziara hiyo na ambaye anahisi anaweza kutumia fursa hiyo kutoa kero yake anakaribishwa sana sisi kazi yetu ni kusimamia wananchi na kuwasaidia."Amesisitiza CPA Makala

Aidha mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa mheshimiwa Waziri Mkuu atatembelea wilaya tatu tu na kisha kuelekea mkoani Dodoma kwa ajili ya Vikao vya Chama kisha baadae atarejea kuendelea na ziara hiyo katika wilaya ya Karatu,Monduli na Ngorongoro.

Miradi hiyo  sita  ina  thamani ya shilingi Bilioni 194.2 kwenye Wilaya  za Arumeru, Arusha na Longido ambapo pia atazungumza na wananchi eneo la ngaramtoni Mkoani Arusha.





Share To:

Post A Comment: