Benki ya NMB imefunga mauzo ya Hati Fungani ya Jasiri (NMB Jasiri Bond) kwa mafanikio makubwa Iliyoweka rekodi ya makusanyo Afrika Mashariki na Kati ya Sh. Bil. 74.27 na kuvuka lengo la Sh. Bil. 25, ufungaji ulioenda sambamba na kuiorodhesha rasmi hati hiyo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Hafla hii ilihudhuriwa na Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu- Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru aliyemwakilisha Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, ametangaza rasmi kuorodhozeshwa kwa hati fungani ya Jasiri na sasa kuanza kununuliwa na kuuzwa kupitia soko la hisa la Dar es salaam.

Akizungumza Mafuru aliipongeza NMB kwa ubunifu chanya wa Jasiri Bond, hati fungani iliyolenga kukusanya fedha ili kutoa mikopo kwa biashara ndogo ndogo na za kati zinazo milikiwa au kuongozwa na wanawake na biashara ambazo bidhaa au huduma zake zinamgusa mwanamke moja kwa moja.

 “Hii sio mara ya kwanza kwa NMB kuja na Hati Fungani na kuvuka lengo la makusanyo, hii ni mara ya nne na kwa hati hii ambayo ni ya kipekee, kama jina lake lilivyo, kumekuwa na ujasiri mkubwa sana, kwani jina Jasiri linaashiria mambo mengi sana.

“Ujasiri wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), ya kuiruhusu Hati Fungani hii kuingia sokoni kabla hata ya sheria zake hazijawa tayari, jambo linalothibitisha imani ya mamlaka hii kwa NMB ilivyokuwa kubwa.

 “Lakini pia, NMB ikalenga kupata Sh. Bil. 25 na hatimaye inafunga mauzo ikiwa imepata zaidi ya mara tatu ya lengo, hii ni kuthibitisha kwamba kuna nguvu kubwa ya kiuchumi miongoni mwa wanawake, tunachotakiwa ni kuweka mazingira wezeshi ya kuwaamini kama wenzetu NMB walivyofanya,” alisisitiza Mafuru.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema NMB ilipokea maombi 1,630 yaliyowezesha kukusanya Sh. Bil. 74.27 badala ya Bil. 25 na kuwashukuru wateja na wawekezaji wote kwa kuiamini benki hio.

“Kuaminika kwa NMB katika hili kunathibitishwa na kuwa asilimia 96 ya waliotuma maombi ya kununua Hati Fungani, yamepitia katika matawi yetu, huku asilimia 4 tu yakifanyika kupitia Madalali wa Soko la Hisa waliosajiliwa”.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA), Nicodemus Mkama, aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa NMB, kwa kufanikisha uuzwaji wa ‘Jasiri Bond’ kwa Umma wa Watanzania na hatimaye kufikia hatua ya kuiorodhesha DSE, tayari kwa mauzo ya walionunua na manunuzi ya waliokosa katika mchakato uliofungwa.

Wengine waliohudhuria hafla hii ni Mkurugenzi Mkuu WA DSE, Moremi Marwa, pamoja na wawakilishi kutoka FSD Africa, Ubalozi wa Uingereza, International Finance Co-operation (IFC), UN Women na Orbit Securities Ltd.

Share To:

Post A Comment: