Articles by "NEC"
Showing posts with label NEC. Show all posts

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu) Dkt. Rose Likangaga akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mjumbe wa Tume, Dkt. Zakia Mohamed Abubakar. 
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu) Dkt. Rose Likangaga akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mjumbe wa Tume, Dkt. Zakia Mohamed Abubakar.

Mwenyekiti wa Mafunzo, Bw. Khalid Khalif akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.

Na Mwandishi wetu, Songea
Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura mkoani Ruvuma wametakiwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao baadae mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Zakia Mohamed Abubakar kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu) Dkt. Rose Likangaga wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa watendaji hao mkoani Ruvuma.

“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao,” ilisema sehemu ya hotuba hiyo.

Dkt Likangaga akisoma hotuba hiyo alisema ni matarajio ya Tume kuwa, mara baada ya zoezi hili lililopo mbele yao kukamilika watu watakaokuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni Wapiga Kura Halali.

Aidha alisema, jukumu la uhamasishaji linawahusu moja kwa moja wao watendaji kwa kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yao kupitia nyenzo walizonazo.

“Ninasisitiza kwamba, mabango na vipeperushi mtakavyopewa na Tume mvisambaze mapema katika kata zote zilizopo katika halmashauri zenu. Kazi yenu kubwa ni kusimamia na kuendesha shughuli zote za uboreshaji katika halmashauri zenu,”ilisisitiza hotuba hiyo.

Watendaji hao wameatakiwa kuisoma kwa umakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sheria za Uchaguzi, Kanuni za Uboreshaji, Maelekezo na Miongozo yote inayotolewa na Tume ili kazi yao ifanyike kwa uadilifu na haki.

Pia wametakiwa kuwasiliana na Tume kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala yote yanayohusiana na utekelezaji wa majukumu yao pindi wanapokutana na changamoto zozote.

“Tume imetekeleza jukumu lake katika hatua ya mafunzo na hivyo nanyi mna wajibu wa kuhakikisha kuwa mnatekeleza kikamilifu majukumu yote mliyokasimiwa,” ilisema sehemu ya hotuba hiyo.

Pia Tume imewataka watendaji hao kuwa makini katika kila eneo la usambazaji na utunzaji wa vifaa na muda sahihi wa ufunguaji na ufungaji wa vituo vya kuandikishia wapiga kura.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unataraji kuanza Januari 12 hadi 18, 2025 katika mikoa ya Songwe, Njombe, Rukwa na Ruvuma kwenye Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Mbinga, Mbinga Mji, Wilaya ya Songea na Manispaa ya Songea ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

Mafunzo hayo yaliwahusisha Maafisa Waandikishaji,Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi, Maafisa TEHAMA wa Halmashauri.





Washiriki wakisikiliza hotuba ya kufunga mafunzo hayo.

Mafunzo yakiendelea



mmoja wa wakufunzi akitoa maelekezo wakati wa mafunzo kwa vitendo.



Washiriki wakifanya mafunzo kwa vitendo.

Mkazi wa Kata ya Ng'ambo aliyefika katika Kituo cha Kizigo Mzee Juma Rai  Juya, akionesha kadi yake ya mpiga kura mara baada ya kukamilisha taratibu za kuboresha taarifa zake kwenye daftari la wapiga kura na Kukabidhiwa kadi yake mpya.

Afisa Mtendaji wa kata  na  Mwandikishaji Msaidizi Kata ya Ng'ambo, Rehema Midelo akizungumza na mwandishi wetu katika kituo cha Masempele kata ya Ng'ambo mjini Tabora wakati akielezea namna zoezi hilo linavyoenda kwa ufanisi mkubwa.

Wakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kituo Cha Kaze Shule ya Sekondari, Bw. Brayson Dickson akielezea namna zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wazpiga kura linavyoendelea katika kituo cha Shule ya Sekondari Kaze mjini Tabora.

Bi Leila Muhaji Kaimu Mkurugenzi Masidizi Habari kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kulia akifuatilia zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika kituo cha Kizigo kata ya Ng'ambo mkoani Tabora.

...........................

Vyama vya Siasa pamoja na Wakazi wa Kata ya Ng'ambo, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora wameonesha ushirikiano mkubwa wa kushiriki katika zoezi la uboreshaji wa majaribio wa daftari la kudumu la wapiga kura linaloendelea katika Kata ya Ng'ambo.

Akifanya mahojiano na Mwandishi Wetu, Afisa Mtendaji na  Mwandikishaji Msaidizi Kata ya Ng'ambo, Rehema Midelo, amesema kuwa mwitikio ni mkubwa na wananchi wameendelea kujitokeza kujiandikisha katika zoezi la uboreshajia wa majaribio wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Bi. Midelo amesema kuwa katika zoezi hilo mpaka Novemba 26, 2023 kuna wapiga wengi wamejitokeza katika uboreshaji wa  daftari la kudumu la wapiga kura.

"Wananchi wa Kata ya Ng'ambo wana hamasa kubwa katika ushiriki wa shughuli za kijamii na maendeleo ikiwemo zoezi  hili la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambalo baadaye linawapa uhalali wa kushiriki kuchagua viongozi wao wakati wa uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani" amesema.

Amefafanua kuwa Kata ya Ng'ambo kuna mitaa 10, huku mtaa wa Kizigo ukiwa na  idadi kubwa ya watu ambao wanajitokeza  katika zoezi la uboreshajia wa  daftari la kudumu la wapiga kura, Hii imepelekea Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuongeza mashine mbili zaidi za BVR Kit na kufikisha tatu katika kituo hicho hata hivyo inapofika jioni bado kuna watu wanabaki ambapo wanaelekezwa kurudi kituoni kesho yake ili kumalizia taratibu zilizobaki.

"Mtaa huu kuna wapiga kura wengi, lakini kuna changamoto ya baadhi ya watu kutoka kata, jirani wamekuwa wakijiandikisha na tukiwabaini tunawapa elimu na kuwarudisha katika maeneo yao na kuwaelimisha kuwa  zoezi bado halijaanza rasmi  na likianza watatangaziwa" amesema

Wakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kituo Cha Kaze Shule ya Sekondari, Bw. Brayson Dickson, amesema kuwa wanachama wa CCM wamehamasika  kwa asilimia kubwa na walio wengi ni vijana ambao pamoja na kufanya mikutano ya kuwahamasisha lakini tulitenga muda wa kuwafuata vijana katika vijiwe vyao na kuwaelimisha kuhusu zoezi hili ndiyo maana unaona mwitikio ni mkubwa sana kwa vijana.

"Baada ya kutoa elimu mwitikio ni mkubwa sana, na kituo hiki hakuna changamoto yoyote, tuendelee kutoa elimu na kuhamasisha wananchi pamoja viongozi ili tuweze kufikia malengo kwa muda uliobaki," amesema  Dickson. 

Wakala wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  katika kituo cha Kizigo  Jumanne Kishimba,  amesema kuwa zoezi la uboreshaji wa  daftari la kudumu la wapiga linakwenda vizuri.

"Hamasa inakwenda vizuri, hakuna shida, sisi CHADEMA tumehamasisha wanachama wetu kwa kuwapigia simu pamoja na kutembea nyumba hadi nyumba kwa ajili ya kujiandikisha," amesema

Naye Mkazi wa Kata ya Ng'ambo aliyefika katika Kituo cha Kizigo Mzee Juma Rai  Juya, amesema kuwa zoezi linakwenda vizuri na kila mtu anayefika anapata huduma kwa wakati.

"Nimefika hapa kituoni wakaniuliza taarifa zangu na kujaza fomu za uboreshaji wa daftari, nikapigwa picha, pia nikachukuliwa alama za vidole kisha nikapewa kadi yangu mpya ya kisasa ya kupigia kura, naishukuru serikali kwa utaratibu huu mzuri wa kuboresha taarifa na nitaitunza kadi yangu mpaka uzeeni" amesema

Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufaa Mwanaisha Kwariko (wapili kushoto), akifuatiwa na Mhe. Jaji Asina Omar na Mhe. Magdalena Rwebangira wakiangalia namna Mpiga Kura anavyo boreshewa taarifa zake wakati Wajumbe hao wa Tume walipotembelea vituo vya uboreshaji katika Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Rorya mkoani Mara leo Novemba 27,2023.
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakiwa katika kituo cha Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Ikoma, wakati walipotembelea Vituo vya uboreshaji katika Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Rorya mkoani Mara leo Novemba 27,2023.
Mjumbe wa Tume, Mhe. Magdalena Rwebangira (kushoto) akizungumza jambo na 
Mwandishi Msaidizi katika Kituo cha Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Ikoma. 
Mjumbe wa Tume, Mhe. Jaji Asina Omar akishuhudia BVR Operator, Felician Meena akiingiza taarifa za Mpiga Kura Mariam Wankyo aliyefika katika Kituo cha Kuandikisha Wapiga Kura cha Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji Ikoma kujiandikisha kuwa Mpiga Kura. 
Mjumbe wa Tume, Mhe. Jaji Asina Omar akishuhudia BVR Operator, Felician Meena akimchukua alama za vidole Mariam Wankyo aliyefika katika Kituo cha Kuandikisha Wapiga Kura cha Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji Ikoma kujiandikisha kuwa Mpiga Kura. 
Mpiga Kura Mariam Wankyo akionesha Kadi yake ya Mpiga Kura mara baada ya kukamilisha taratibu za Uandikishwaji. 
Mpiga Kura akijaziwa taarifa zake.
Wajumbe wa Tume wakiwa katika ziara ya kutembelea vituo. 

BVR Opareta akichukua picha ya Mpiga Kura aliyefika kuandikishwa. 
Mjumbe wa Tume, Mhe. Jaji wa Rufaa Mwanaisha Kwariko akizungumza jambo na Mpiga Kura aliyefika kituoni kuboresha taarifa zake.  
Mjumbe wa Tume, Magdalena Rwebangira akiangalia Mwandishi Msaidizi akimwandikisha Mpiga Kura. 
Na Mwandishi wetu, Mara
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wameonesha kuridhishwa na zoezi la Uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaoendelea katika Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara ambapo hadi kufikia jana Wapiga Kura 1,613 wamejitokeza.
 
Wajumbe hao wa Tume, Mhe. Jaji Asina Omar, Mhe. Jaji wa Rufaa Mwanaisha Kwariko na Mhe. Magdalena Rwebangira wametembelea vituo vya uboreshaji katika Kata ya Ikoma na kushuhudia ufanisi wa zoezi hilo.
 
Wakizungumza wakati wa ziara hiyo, Jaji Asina Omar amesema mwitikio wa wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ni mkubwa na mawakala wanashiriki kikamilifu katika zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuwabaini wananchi wasio na sifa za kuandikishwa kuwa Wapiga Kura.
 
“Zoezi linakwenda vizuri, tumeshuhudia katika vituo tulivyotembelea hakuna changamoto na zilizopo zimetatuliwa na wataalam kwa kushirikiana na makawala wa vyama waliopo vituoni jambo ambalo linaonesha lengo la zoezi hili kutimia kama ilivyo kusudiwa,” alisema Mhe. Jaji Asina.
 
Jaji Asina amesema, muda unaotumika kuandikisha au kuboresha taarifa za Mpiga Kura unazidi kuwa mfupi na kuimarika kwa huduma vituoni hivyo kuleta ufanisi zaidi siku hadi siku na kuonesha uwezo wa vifaa vinavyotumika.
 
Kwa upande wake Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Magdalena Rwebangira amesema ameridhishwa namna zoezi linavyofanyika hivyo lengo la zoezi hilo la kufanyia majaribio vifaa vya uboreshaji pamoja na mifumo ya uboreshaji wa Daftari linatimia kwani changamoto zinabainika na kutatuliwa mapema.
 
Akitoa taarifa ya siku nne za uboreshaji huo wa majaribio katika Kata ya Ikoma, Mkurugenzi wa Idaya ya Usimamizi wa Uchaguzi, Ndg. Grayson Orcado kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi alisema, zoezi hilo linakwenbda vizuri na kwa ufanisi mkubwa kwani hadi sasa wananchi 1,613 wamejitokeza vituoni ambapo kati ya hao 1,356 wamejiandikisha kuwa wapiga kura na wapiga kura 257 wameboresha taarifa zao huku hakuna walioondolewa katika Daftari.
 
Orcado amesema, mawakala wa vyama wanaonesha ushirikiano wa hali ya juu hasa katika changamoto za utambuzi wa wakazi wa maeneo yao kwa kuzingatia kuwa Kata ya Ikoma inamwingiliano wa raia wanchi jirani.
 
Kwa mujibu wa mawakala wa vyama waliokuwepo katika kituo cha kujiandikisha wapiga kura cha Shule ya Msingi Nyamasanda, walieleza kuwabaini raia 8 wakigeni kutoka nchi jirani ambao walikiri kuwa si watanzania na hivyo Mwandishi Msaidizi hakuweza kuwaandikisha kuwa wapiga kura.
 
Wakala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Silvanus Owan’ge aliyepo katika Kituo cha Ofisi ya Mtendaji Kata ya Ikoma amesema, wanarisdhishwa namna zoezi hilo lilivyo la uwazi na kupongeza Tume kwa namna inavyofanya kazi kwa kushirikiana nao.
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendesha zoezi la uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara na Kata ya Ng’ambo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.
Mkurugenzi wa Daftari na Tehama , Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC Bw. Geofrey Mpangala akishuhudia wakati msimamizi wa kituo cha Masempele katika Kata ya Ng'ambo , Bi. Mwatano  Juma Gervas, akimkabidhi kadi ya mpiga kura Wilson Shango mwananchi  wa Kata ya Ng'ambo Halmashauri ya Tabora mara baada ya kujiandikisha  katika kituo cha Masempele.
Mkurugenzi wa Daftari na Tehama , Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC Bw. Geofrey Mpangala akipata maelezo kutoka kwa msimamizi wa kituo cha Masempele katika Kata ya Ng'ambo , Bi. Mwatano  Juma Gervas wakati akichukua taarifa za Wilson Shango mpiga kura wa Kata ya Ng'ambo Halmashauri ya Tabora alipokuwa akijiandikisha  katika kituo cha hicho.
Afisa Tehama Mkuu Tume ya Uchaguzi NEC Bw. Lazaro Madembwe akishuhudia wakati Mwandishi Msaidizi Tume ya Uchaguzi Bw. Mwandishi Msaidizi NEC Bw. Emmanuel Madaha alipokuwa akichukua taarifa na mmoja wa wananchi waliofika kwenye kituo cha Masempele ili kujiandikisha kwenye daftari la Kudumu la Mpiga kura katika Halmashauri ya Tabora.
Gasper Kiswaga Msimamizi wa kituo cha Kizigo akiendelea kuchukua taarifa za mpiga kura Zuhura Masoud aliyefika kujiandikisha katika kituo cha Kizigo Halmashauri ya Tabora mkoani humo.
Akimu Gervas Kinyaga Mwandishi Msaidizi Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC akimuandikisha Bw. Simon Nicholas Mlimanazi katika kituo cha kujiandikisha  cha Kizigo Halmashauri ya Tabora. 
************
Na Mwandishi Wetu, Tabora.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema zoezi la uboreshaji wa majaribio wa daftari la kudumu la mpiga kura katika Kata za  Ikoma iliyoko wilayani Rorya mkoani Mara na Kata ya Ng'ambo iliyoko  Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora linaendelea vizuri, huku kukiwa na mwitikio mkubwa wa watu.

Akizungumzia zoezi la uboreshaji wa majaribio ya daftari la kudumu la wapiga kura katika kituo cha Masempele, Kata ya Ng'ambo Mkurugenzi wa Daftari na Tehama , Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC Bw. Geofrey Mpangala, amesema , kuwa zoezi linaendelea vizuri na hadi kufikia Novemba 24, 2023 mwitikio wa wananchi ni mkubwa.

Amesema Kata ya Ikoma kuna vituo sita na kata ya Ng'ambo vituo kumi ambapo kwa kata ya Ikoma  jumla ya wapiga kura 310 walijiandikisha na walioboresha taarifa zao walikuwa 71. Hata hivyo hakuna aliyeondolewa kwenye daftari la mpiga kura.

Ameongeza kuwa kwa Kata ya Ng'ambo jumla ya wapiga kura wapya 484 walijiandikisha, huku walioboresha taarifa zao wakiwa 309 na aliyeondolewa kwenye daftari  la mpiga kura alikuwa mtu 1 tu.

Takwimu za Jumla mpaka jana kwa kata zote mbili wapiga kura wapya waliojiandikisha walikuwa 704 na walioboresha taarifa zao walikuwa 380 huku aliyeondolewa kwenye daftari alikuwa mmoja.

"Tunao mfumo wa kuboresha taarifa za wapiga kura kwa njia ya mtandao (OVRS ) Lakini mpaka sasa hakuna aliyeboresha taarifa hizo kwa njia ya mtandao. Hivyo, kuna kila sababu ya kuelimisha zaidi wananchi ili wauelewe zaidi mfumo huo wa kuboresha taarifa zao kwa njia ya mtandao na waweze kuutumia", Amesema Mpangala.

Naye msimamizi wa kituo cha Masempele katika Kata ya Ng'ambo , Bi. Mwatano  Juma Gervas, amesema kuwa zoezi linaendelea vizuri kwani wapiga kura wote wanaofika katika Kituo hicho wanafuata taratibu zote za uandikishaji kwa kutoa taarifa zao  muhimu kwa ajili ya kuandikishwa au kuboresha taarifa zao.

Aidha, mpiga kura aliyefika katika Kituo  cha Kizigo kwa ajili ya kujiandisha Bw. Simon Mlimanazi, amesema kuwa zoezi linaendelea vizuri kwani katika kituo hicho amepata huduma kwa wakati na amekamilisha taratibu zote hatimaye amekabidhiwa kadi yake ya mpiga kura.

Ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kujitokeza  kwa wingi kujiandikisha kabla muda haujaisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la mpiga kura kwakuwa  hili ni jambo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi karibuni ilitangaza kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023 kuanza zoezi la uboreshaji wa majaribio wa daftari la kudumu la wapiga kura katika Kata ya Ng’ambo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara .