Articles by "KATIBA NA SHERIA"
Showing posts with label KATIBA NA SHERIA. Show all posts

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Franklin Rwezimula, amewataka watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuendelea kuzingatia weledi, maadili na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi wa huduma za kisheria na kulinda maslahi ya taifa.

Rwezimula aliyasema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wa mwaka 2025/2026 uliofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha, ambapo aliwataka watumishi kutumia mkutano huo kujijengea maarifa, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kazini.

Alisema kupitia mkutano huo, washiriki watapata mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku pamoja na kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ushindani wa kiuchumi na mahitaji ya sasa ya utumishi wa umma.

“Mbali na mafunzo na mada mtakazopata katika mkutano huu, ninaamini pia mtapata fursa ya kujadili masuala muhimu yanayohusu ustawi wa ofisi yetu, kujenga mshikamano, utu na umoja miongoni mwetu kama familia moja,” alisema Rwezimula.

Aidha, aliwataka watumishi kuendelea kujiendeleza kitaaluma kwa kutumia fursa mbalimbali za mafunzo zinazotolewa ndani na nje ya nchi, akisisitiza kuwa elimu na utaalamu ni msingi muhimu wa kulinda rasilimali za taifa.

Katika hotuba yake, Rwezimula alisema Serikali ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kuimarisha uwezo wa watumishi pamoja na kuandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji ya taifa katika sekta ya sheria na usimamizi wa mikataba.

Kwa upande wake,Wakili Mkuu wa Serikali Dk Ally Possi alisema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inaendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda maslahi ya taifa kupitia usimamizi wa mashauri ya serikali, ushauri wa kisheria na usimamizi wa mikataba mikubwa ya maendeleo.

Alisema mawakili wa serikali ni “askari wa kalamu” wenye jukumu kubwa la kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha fedha za umma zinalindwa kupitia usimamizi madhubuti wa mikataba na mashauri ya serikali.

“Ni muhimu taasisi zote za serikali kuwashirikisha mawakili wa serikali kuanzia hatua za maandalizi ya mikataba, majadiliano hadi utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Dk Possi.

Alibainisha kuwa kupitia usimamizi wa mashauri mbalimbali, ofisi hiyo imefanikiwa kuokoa fedha za serikali zinazokadiriwa kufikia trilioni 1.35, hatua aliyosema inaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha ofisi hiyo na watumishi wake.

Alisema mafunzo yaliyotolewa katika mkutano huo yamelenga kuwajengea watumishi uwezo katika maeneo mbalimbali ikiwemo maadili ya utumishi wa umma, mawasiliano kazini, afya ya akili, uwekezaji na ukuzaji wa vipaji mahali pa kazi.

Mkutano huo uliwakutanisha watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutoka mikoa 18 nchini ukiwa na kaulimbiu isemayo: “Mtumishi wa Umma Bora na wa Kisasa; Utaalamu, Ustawi na Mafanikio ya Kudumu.”














 


Na Magesa Magesa,Arusha


ZAIDI ya wananchi 1800 kutoka katika mokoa 22 hapa nchini wamepata msaada wa kisheria katika kampeni ya msaada wa kisheria ya mama samia ijulikano kama Samia Legal Aid inayoendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mkurugenzi wa kampeni ya Samia Legal Aid, Ester Msambazi amesema jana alipokuwa akuzungumzia kampeni hiyo katika maonyesho yanayoendelea jijini Arusha kuelekea siku ya mwanamke duniani, wameshapokea migogoro 677.

Amesema kuwa pia wamepkea migogoro 677 kati yake 136 imefanikiwa kutatuliwa kwa wenye migogoro kusameheana na kupeana mikono huku baadhi ya migogoro iliyoko ngazi ya mahakama wahusika wameandikiwa hati za mahakama na kutakiwa kufika mahakamani.

“Tumefanikiwa kupokea migogoro 677 na kupatia ufumbuzi migogoro 136, ambapo waliofika tumewaandikia makubaliano na kuwashauri kufika mahakamani wale wanaopaswa kufika huko,”amesema Msambazi

Amesema tofauti na migogoro ambayo wamekuwa wakiipokea kutoka katika mikoa mingine nchini, migogoro mingi ya Arusha inatokana na watu kudaiana mali, huku mikoa mingine migogoro ya mirathi imeonekana kuwa kinara namba mbili baada ya migogoro ya ardhi.

 

“Arusha kumekuwepo na changamoto kubwa ya migogoro ya madai baada ya migogoro ya ardhi na wanaofikisha madai wengi ni wanaume, tofauti na mikoa mingine tuliyotembelea, hata hivyo tumefanikiwa kutatua migogoro mingi na tunaendelea kuitatua,”amesema.

 

Msambazi amesema migogoro iliyobaki inaendelea kufanyiwa kazi na jopo la wanasheria walioko katika kampeni hiyo na endapo wahusika hawajaridhika na majibu wanayopatiwa huruhusiwa kwenda katika taasisi zingine kutafuta haki zaidi.

 

“Sisi tumekuja hapa kutoa haki, hakuna hata mmoja ambaye tunafanya upendeleo lakini kuna baadhi ambao wao huwa hawataki kushindwa wala kupatanishwa wakiona hawawezi kupatana sisi tunawaruhusu kwenda mbele kutafuta haki zaidi,”amesema.

 






 



Na Mwandishi Wetu, KIGOMA

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro ameongoza jopo la wataalamu wa msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) kutoa huduma na elimu ya uraia kwa wananchi wa Kata ya Kibirizi iliyopo Manispaa ya Kigoma, mkoani Kigoma.

Dk.Ndumbaro ambaye yupo mkoani humo jana walipiga kambi kwenye Kata hiyo na kusikiliza na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu changamoto za masuala ya kisheria.

Katika kampeni hiyo ambayo imeanza juzi mkoani humo na inalenga kuvifikia vijiji 240 mkoani humo, Waziri Ndumbaro alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza wananchi wapewe elimu hiyo sambamba na elimu ya sheria na Katiba, Haki za binadamu na msaada wa kisheria ili wajue sheria na kupata haki zao.

“Tanzania ni nchi nzuri yenye kuvutia wema na wabaya, yenye neema kedekede sisi tumejaa neema, ina amani na utulivu na mfumo mzuri wa maisha, kuna nchi hazina haya tuliyo nayo sisi, uzuri huu unawavutia wengi wengine wanakuja kwa kufuata taratibu rasmi za uhamiaji, wapo wanaokuja kwa njia za panya hawa ndio wanaotuponza,”alisema.

Alisema wananchi wa eneo hilo wanapaswa kuwa makini kwa kuwa tatizo la mipakani kuna kuingiliana kwa makabila na nchi jirani.

“Tusiwapokee watu kwasababu tuna share nao makabila, juzi tulikuwa na kesi moja kuna raia wa Burundi walikaa huku wakapewa uraia, mmoja aliyepewa uraia ameenda Burundi anaongoza chama cha siasa, huku tunamjua kama mtanzania lakini nchi Jirani anaongoza chama cha siasa hiyo ni sawa? Hapa ndipo mgogoro unapokuja,”alisema.

Alisema katika kampeni hiyo Kigoma watatoa elimu ya uraia kwa kuwa masuala ya uraia ni magumu hasa maeneo ya mipakani.

“Lazima tufahamu sheria, suala si kuzaliwa tu endapo ulizaliwa na mmoja wa wazazi sio mtanzania unapaswa ufanye nini kwa mujibu wa sheria, unakwenda uhamiaji unasema Baba yangu alikuwa Mrundi na mama yangu Mtanzania nimefikisha umri wa miaka 18 nachagua sasa kuwa Mtanzania naomba mnihalalishe,”alisema.

Alifafanua kuwa gharama za huduma za kisheria ni kubwa ndio sababu iliyomsukuma Rais Samia kubuni kampeni hiyo ili kuwasogezea wananchi huduma za kisheria popote walipo.

“Wataalamu hawa wapo kwenye Kata 80 na Vijiji 240 wanaendelea kusikiliza na kutatua kero za kisheria za wananchi wa Kigoma, huyu ni Rais mwenye uchungu na wananchi wake wanyonge, Mama huyu tuna kila sababu ya kusimama naye hasa mwaka huu 2025,”alisema.

Alieleza kuwa kampeni hiyo kwa awamu ya kwanza mwisho wake ni mwakani 2026 na ili kufanikisha ni muhimu wananchi kumchagua Rais Samia kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu ili aendelee kuwasogezea huduma za kisheria.

Awali, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda alisema ni maono ya Rais Samia wananchi wapate nafasi ya kusikilizwa na wapewe msaada wa kisheria kwenye changamoto zao.

“Wananchi hawa wana kadhia nyingi zinazotokana na mambo ya sheria kuhusu hukumu zinazotolewa na Mahakama, nakala za hukumu, namna ya kusikiliza mashtaka, upelelezi, kukaa muda mrefu rumande, umiliki wa viwanja,”alisema.

Alisema pamoja na matatizo mengine ya kisheria yaliyopo Kigoma Mjini kuna suala la utata wa uraia wa watu.

“Kuna watu mababu zao wamezaliwa Kigoma na wamefia Kigoma, msaada wa kisheria namba moja tunaohitaji ni kutatua utata wa uraia wa watu, watu wameomba namba za NIDA hawajapata, watu wamepeleka hadi wazazi wao lakini bado wameonesha na makaburi ya wazazi wao lakini bado wanapata misukosuko,”alisema.

Alisema kuna tatizo la watu kuhusisha kabila na Taifa na kwamba msaada huo wa kisheria utatoa tabasamu kwa wananchi ambao wamekosa watu wa kuwatetea kwenye changamoto zao za kisheria.       

 


Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro Leo tarehe 23 Januari, 2025 amewasili Mkoani Kigoma na kukutana na mwenyeji wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye, kwa ajili ya kushiriki katika Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia utakaofanyika tarehe 24 Januari, 2025 Mkoani Kigoma.

Akizungumza mara baada ya Mhe. Waziri kuwasili ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya salamu, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amesema kuwa ameipongeza Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila Mwananchi anapata Haki na kwa wakati kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Damas Ndumbaro amesema kuwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria Migogoro mbalimbali itakwenda kutatuliwa kupitia njia ya Amani, Usuluhishi, Mahakama, Kiutawala na kwa njia za Kiuchunguzi.

Mhe. Ndumbaro amesema kuwa, Kampeni ya Msaada wa Kisheria itatekelezwa kwa muda wa siku tisa katika Halmashauri tisa za Mkoa wa Kigoma na kuwafikia Wananchi katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha matatizo yote ya Kisheria yanapatiwa suluhu.