Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa shilingi bilioni 73.8 wa kusambaza umeme katika vitongoji 527 mkoani Tanga.
Hayo yamebainishwa leo Januari 29, 2026 Jijini Tanga na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy wakati wa kuwatambulisha Wakandarasi waliuoshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo, Kampuni ya Giza cable industries pamoja na Energy service Limited katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
“Leo tuko hapa kwako kutambulisha Wakandarasi ambao watakuja kutekeleza mradi mkubwa wa kupeleka umeme katika vitongoji 527 katika Mkoa wa Tanga.
Wakati tunafanya nao majadiliano kuna maagizo mahususi tuliwapa na tungependa kama kiongozi wetu wa Mkoa uyafahamu. Moja tumewaelekeza wawe na timu ya kufanya kazi karibu kila Wilaya,” ameainisha Mhandisi Saidy.
Ameongeza pia, Wakandarasi hao wanatakiwa kujiepusha na vitendo vya kutoa lugha chafu, pamoja na vitendo vya rushwa wakati wanatekeleza miradi hiyo kwa wananchi.
“Ukifanya kazi kwenye mradi wa serikali unatakiwa kufanya kama mtumishi wa umma. Lugha chafu hazikubaliki. Kurubuni wanakijiji ni kitu ambacho kitapelekea kuvunja mkataba wako,” amessisitiza Mhandisi Saidy.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dadi Kolimba ameipongeza serikali kwa utekelezwaji wa mradi huo na kusema kuwa utakwenda kufungua zaidi fursa za uchumi vijijini.
“Ukiangalia kwa wakandarasi hawa wawili ambao wametambulishwa leo ambao wanaenda kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 527, jumla ya shilingi Bilioni 73.8. Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kutoa fedha za kuwezesha kutekelezwa kwa mradi huu,” amesema Mhe. Kolimba huku akiwataka Wakandarasi hao kuhakikisha wanamaliza mradi huo ndai ya muda uliopangwa.
Aidha, Mhe. Kolimba ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi hao pindi watakapoanza kutekeleza mradi huo ili malengo yaliyowekwa na serikali yaweze kufikiwa.

































