Ujenzi wa mabweni ya wasichana katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli umefikia asilimia 58, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa ya makazi kwa zaidi ya wanafunzi 500 pindi mradi huo utakapokamilika.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo chuoni hapo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema kukamilika kwa mabweni hayo kutasaidia kulinda usalama wa wanafunzi wa kike na kuwawezesha kusoma katika mazingira salama na tulivu.

“Watoto wakike wako kwenye hatari zaidi wanapolazimika kuishi nje ya maeneo ya Chuo. Kukamilika kwa mabweni haya kutapunguza changamoto za kiusalama na kuwapa wasichana wetu nafasi ya kusoma kwa utulivu na kuzingatia ndoto zao,” amesema Mhe. Mahundi.

Mhe. Mahundi amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira rafiki ya kujifunzia, hususan kwa masomo ya ufundi na ujuzi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli, Boniface Daniel amesema fedha walizopokea hivi karibuni zitasaidia kuingia awamu ya nne ya ujenzi wa mabweni hayo, hatua itakayoharakisha kukamilika kwa mradi huo.

“Fedha tulizopokea zitatuwezesha kuendelea na awamu ya nne ya ujenzi. Lengo letu ni kuhakikisha mabweni haya yanakamilika kwa wakati ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike,” amesema Mkuu wa Chuo Boniface Daniel.

Nao baadhi ya wanafunzi wa Chuo hicho wamepongeza jitihada za Serikali katika ujenzi wa mabweni hayo, wakisema yatasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza morali ya masomo, hasa katika kozi za ufundi.

Katika ziara yake chuoni hapo, Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi ametembelea madarasa ya ushonaji, eneo la ujenzi wa mabweni hayo pamoja na kufanya mazungumzo na wanafunzi, akiwahimiza kuzingatia nidhamu na kutumia fursa za elimu ya ufundi zinazotolewa na Serikali.













 


Naibu Waziri wa Maendeleo ya jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya ameanza ziara ya kikazi Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha ukiwa ni muendelezo wa kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

Awali Mhandisi Maryprisca Mahundi amefika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM)Wilaya ya Monduli kwa ajili ya utambulisho.

Akiongea na uongozi CCM wa Wilaya ya Monduli Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi ameahidi kutekeleza majukumu kwa lengo la kumsaidia Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.

Waziri na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Wanawake na Makundi Maalumu wanafanya ziara nchi nzima kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mabweni ya wasichana katika vyuo vya Maendeleo ya jamii.












 


๐Ÿ“Œ Amshukuru Mhe.Rais Dkt Samia  kwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi

๐Ÿ“Œ Asisitiza usimamizi bora wa masuala ya haki za wafanyakazi na utoaji wa elimu kwa umma na kuboresha utoaji wa huduma za umeme nchini.

Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi, leo tarehe 22 Januari, 2026 amefungua rasmi Kikao cha 55 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kinachofanyika mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Waziri Ndejembi amemshukuru Mhe. Rais Dkt Samia kwa kuboresha maslahi na stahiki za wafanyakazi wa TANESCO, huku akisisitiza usimamizi madhubuti wa masuala ya haki za wafanyakazi na kuimarisha ushirikiano mahali pa kazi, pamoja na kuendeleza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu huduma ya umeme. 

"Natambua mmekutana hapa  kujadili kwa kina mambo yanayowahusu wafanyakazi naomba mhakikishe mnazungumza yote na kukubaliana ili kuendelea kuboresha utendaji wa shirika na maslahi ya wafanyakazi''.

Amehimiza pia umuhimu wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma bora na za uhakika za umeme kwa wateja wake nchini.

Akimkaribisha katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la umeme Bw. Lazaro Twange amemshukuru Mhe Waziri kwa kukubali wito wa kuja kufungua kikao hicho na kumuahidi kuwa wataendelea kusimamia haki za wafanyakazi na kuhakikisha wanakuwa na matokeo katika utendaji.

“Kipekee nikushukuru kwa kuitikia wito wa kuja kutufungulia kikao hiki, kama Mwenyekiti wa baraza hili nikuahidi kuwa nitaenda kuyasimamia yote tutakayojadili hapa kwa ajili ya kuleta tija na maendeleo ya Shirika hili na kuongeza ufanisi katika kuhudumia wananchi”, alieleza Twange. 

Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wa TANESCO, wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi (TUICO), Wakurugenzi wa Kanda, pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi kutoka kampuni tanzu na ofisi mbalimbali za mikoa nchini.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amemtaka Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, kuhakikisha anasimamia kwa karibu malipo ya wakulima wa kahawa ili kuwalinda dhidi ya ucheleweshaji wa fedha zao unaofanywa na baadhi ya kampuni zinazonunua zao hilo.

Mhe. Kapinga, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, ametoa maelekezo hayo mapema wiki hii alipokuwa akizungumza katika kikao na viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

Amesisitiza kuwa zao la kahawa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Wilaya ya Mbinga na chanzo kikuu cha maisha ya wananchi wengi, hivyo Serikali haitavumilia kuona watu wachache wanaitia doa kutokana na uzembe au kushindwa kusimamia ipasavyo sheria na kanuni ili wakulima walipwe fedha zao za mauzo ya kahawa kwa wakati.

Katika maelekezo yake, Waziri Kapinga amemwagiza Afisa Ushirika wa wilaya hiyo, kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati bila visingizio, huku akiwataka watumishi kutotumia masuala ya ukomo wa malipo kama kisingizio cha kuwakandamiza wakulima.

Kwa upande mwingine, Waziri Kapinga amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, kufanya tathmini upya ya kampuni ya Mamba Coffee ili kubaini kama inastahili kuendelea kupewa kibali cha kununua kahawa, kutokana na malalamiko ya ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, amesema kuchelewesha malipo ni sawa na kuwarudisha nyuma wakulima na maendeleo yao.

Vilevile, amewahimiza viongozi wa vyama vya ushirika kukaa vikao na kufanya maamuzi muhimu mapema kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo, ili kuzuia migogoro inayoweza kuepukika.

Pia ametoa onyo kali dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za ushirika, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kutumia fedha hizo kwa maslahi binafsi hatavumiliwa.

 



Tanga, Januari 21, 2026


Baada ya kustaafu nilishuhudia kitu kimoja, nilistaafu tarehe 1/7/2012 na baada ya wiki moja niliweza kupata Mafao yangu.


Hayo ni maneno ya Mzee Ndibalema Kisheru, mstaafu anayepokea pensheni kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Mzee Kisheru ambaye alitumikia nafasi mbalimbali serikali akimalizia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, ameyasema hayo kwenye banda la PSSSF kwenye Maonesho ya Tano ya Wiki ya Huduma ya Fedha, ambayo yamefunguliwa rasmi leo Januari 21, 2026 na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) kwaniaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamisi Mussa Omar, kwenye viwanja vya Usagara jijini Tanga.

Aidha, mzee Kisheru amesema, “Miaka 13 imepita nimeendelea kupata Mafao yangu bila kusita” Alisisitiza.

Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga amechangia vifaa vya ujenzi kwa Shule ya Msingi Ugano iliyopo Kata ya Kambarage na Shule ya Msingi Kibandai A iliyopo Kata ya Maguu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Mchango huo umehusisha bati 100 za geji 28 zenye thamani ya shilingi milioni 3.5 kwa ajili ya kuezeka vyumba viwili vya madarasa, mbao za kenchi zenye thamani ya shilingi milioni 1, pamoja na mifuko ya saruji na nondo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba katika Shule ya Msingi Ugano.

Akiwa katika Kijiji cha Kibandai A, Kata ya Maguu, Mhe. Kapinga amesema anatambua changamoto za uchakavu wa miundombinu ya shule ikiwemo madarasa, nyumba za walimu, nyumba ya mganga pamoja na ofisi za shule, na ameahidi kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuzitatua changamoto hizo, Katika hatua hiyo, Mhe. Kapinga amechangia mifuko 50 ya saruji pamoja na shilingi laki tano kwa ajili ya ununuzi wa mchanga, ili kuharakisha ukamilishaji wa miradi ya ujenzi.

Wakati huo huo, Mhe. Kapinga amewakumbusha wananchi wa jimbo hilo umuhimu wa kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kutumia kinga na kuwa waaminifu katika mahusiano yao na kujiepusha na vitendo vyote vinavyoweza kuchangia maambukizi. Amesema haikubaliki kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuendelea kutajwa miongoni mwa maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya UKIMWI kila ripoti za kitaifa zinapotolewa.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuchukua hatua binafsi na za kijamii ikiwemo kupima afya mara kwa mara, kutumia kinga, na kuepuka kuwaambukiza wengine, akibainisha kuwa maambukizi ya UKIMWI hayawezi kutambulika kwa kumuangalia mtu kwa sura.

Mhe. Kapinga amemshukuru Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa miradi ya maendeleo inayoendelea katika Jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma.

Akizungumza Dkt Salemani Jumbe Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, amesema zaidi ya madawati 2,000 yamekamilika kutengenezwa na yako katika hatua za mwisho za kusambazwa, na yatapelekwa katika shule zote zenye upungufu wa madawati ikiwemo Shule ya Msingi Ugano, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Dkt. Jumbe, ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, amesema Kijiji cha Kibandai A tayari kimefungua zahanati kwa ushirikiano na Mhe. Kapinga, ambaye alichangia kwa kiasi kikubwa vitanda na vifaa tiba, ameeleza kuwa kwa sasa watumishi wa afya 100 tayari wamewasili wilayani kwa ajili ya kupangiwa vituo vya kazi.

Kwa ujumla, mchango wa Mhe. Judith Kapinga umepokelewa kwa furaha na wananchi wa Kata ya Kambarage na Maguu, ambao wameeleza kuwa hatua hiyo itaongeza hamasa ya elimu, kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, na kuonesha dhamira ya dhati ya serikali katika kuimarisha sekta ya elimu na afya.

 



Na Mwandishi wetu, Dodoma

Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, kupitia Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali, imesaini Hati za Mashirikiano (MoU) na Vyuo Vikuu vinne ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha na Taasisi ya Uhasibu Tanzania kwa lengo la kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini unaotumia ushahidi katika kupanga na kutekeleza sera, mipango, programu na miradi ya maendeleo.  

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo Januari 21, 2026 jijini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi Waziri Mkuu (SBUU) Dkt. Jim Yonazi amesema kupitia mashirikiano hayo, Serikali na Vyuo Vikuu vitashirikiana katika kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini, kufanya tathmini za pamoja za miradi ya maendeleo, kuendeleza tafiti bunifu na kuhakikisha maarifa yanayozalishwa vyuoni yanatumika kuboresha utendaji wa Serikali. 

"Serikali imesisitiza kuwa, mafanikio ya MoU hizo yatapimwa kwa utekelezaji wake, kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye msisitizo wa matokeo yanayopimika na manufaa halisi kwa wananchi" ameongeza Dkt. Yonazi.