Na OWM - TAMISEMI, Arusha

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, Mhe. Florent Kyombo ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (OWM- TAMISEMI), kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi ya TACTIC katika Jiji la Arusha, miradi ambayo imeweka kiwango bora cha utekelezaji wa miradi ya aina hiyo ambayo inatekelezwa katika miji na majiji 45 nchini.

Mhe.  Kyombo ametoa pongezi hizo leo Machi 17, 2026 mara baada ya kamati yake kutembelea, kukagua na kuridhishwa na usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani (Bondeni City Bus Terminal), ujenzi wa soko la Mrombo, ujenzi wa soko la Kilombero pamoja na ujenzi wa mradi wa uboreshaji wa bustani ya mapumziko Themi.

“Naungana na wajumbe wenzangu kutoa pongezi za dhati kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya TACTIC katika jiji la Arusha, hakika utekelezaji wa miradi hii umeweka kiwango bora cha namna ya kutekeleza miradi ya aina hii nchini,” amesistiza Prof. Shemdoe.

Aidha, Mhe. Kyombo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha za utekelezaji wa miradi pamoja na kumpa dhamana ya usimamizi wa miradi hiyo Prof. Shemdoe na watendaji wanaomsaidia, ambao wanaitendea haki dhamana waliyopewa na Mheshimiwa Rais.

Sanjari na hilo, Mhe. Kyombo amempongeza Mkandarasi wa Kampuni ya M/S MOHAMMEDI BUILDERS LIMITED kwa kiwango kizuri cha utekelezaji wa miradi yote minne ya TACTIC inayotekelezwa katika jiji la Arusha, ambayo itachochea ukuaji wa uchumi ndani ya jiji hilo.

Akizungumzia suala la ushirikishaji wa wadau katika miradi hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa kabla ya kuanza kutekelezwa miradi hiyo,  timu ya kuandaa mazingira ya utekelezaji wa mradi hupita ikiwa na fomu maaluum ya kupokea maoni ya wadau kuhusiana na mradi husika, na kuongeza kuwa maoni ya wadau yalizingatiwa kwani hicho ni kigezo muhimu cha miradi yote inayotekelezwa na Benki ya Dunia.

Naye mmoja wa Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge ya Kudumu ya TAMISEMI Mhe. Hawa Mwaifunga, amesema amefarijika kuona hatua nzuri iliyofikiwa ya Ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani  na kuongeza kuwa kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa na manufaa kwa wananchi wa Jiji la Arusha.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI Mhe. Jafari Chege ameupongeza uongozi wa mkoa na Jiji la Arusha kwa kutekeleza vizuri miradi ya TACTIC ambayo imelenga kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kukuza uchumi wa wananchi wa Jiji la Arusha.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Themi Mhe. Melance Kinabo, amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulijali Jiji la Arusha kwa kuliletea fedha za utekelezaji wa miradi minne ya TACTIC, ambayo ikikamilika itaongeza wigo wa wananchi kupata ajira zitakazowaingizia kipato.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: