Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa utendaji kazi mzuri, maendeleo na mabadiliko makubwa yanayoonekana katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 16 Januari, 2026, katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb), baada ya Kamati kupokea Taarifa ya Muundo na Majukumu ya BRELA iliyowasilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa.
Mhe. Mwanyika amesema kuwa, licha ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na BRELA, bado kuna changamoto ya wafanyabiashara na wamiliki wa kampuni wengi kutohuisha taarifa za kampuni zao kupitia mfumo wa BRELA. Ameeleza kuwa tatizo hilo ni kubwa, lakini wananchi wengi hawalitambui ipasavyo.
“Hili tatizo ni kubwa lakini wengi hawalielewi; wengi wana kampuni lakini hawajahuisha taarifa za kampuni hizo,” amesema Mhe. Mwanyika.
Kutokana na hali hiyo, Mhe. Mwanyika ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kufanya utafiti na kutathmini namna ya kuboresha mfumo wa uhuishaji wa taarifa za biashara na kampuni, ili kuja na mfumo wezeshi, unaoongeza ufanisi na kuharakisha utoaji wa huduma.
Aidha, Mwenyekiti huyo amesisitiza umuhimu wa kuhuisha taarifa za biashara na kampuni, akitoa wito kwa wafanyabiashara kuchukua hatua hiyo kwa hiari na kwa wakati.
“Kuhuisha taarifa ni jambo jema, na ni muhimu tukalifanye,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, amesema kuwa Wakala itaendelea kutoa elimu kwa Waheshimiwa Wabunge kupitia Kamati hiyo ili kuwajengea uelewa mpana kuhusu majukumu ya BRELA pamoja na mifumo ya kidijitali inayotumika katika utoaji wa huduma.
Bw. Nyaisa ameeleza kuwa, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, uelewa mdogo wa wananchi kuhusu matumizi ya mifumo ya kidijitali bado ni miongoni mwa changamoto zinazokwamisha urasimishaji wa biashara na utoaji wa leseni.
Amefafanua kuwa mfumo wa BRELA ni rafiki kwa mtumiaji na unajieleza wenyewe, hivyo kumwezesha mwananchi kujisajili moja kwa moja bila usumbufu.
“Mfumo wa BRELA ni rafiki kwa mtumiaji na unajieleza wenyewe, hivyo humwezesha mtu kuingia moja kwa moja na kusajili kampuni yake bila usumbufu,” amesema Bw. Nyaisa.
Ameongeza kuwa BRELA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuwahamasisha kufahamu kuwa mchakato wa usajili wa biashara, kampuni na utoaji wa leseni si mgumu kama inavyodhaniwa.
Amebainisha kuwa katika mapitio ya sheria yanayoendelea, BRELA inapendekeza kutambuliwa rasmi kwa Mawakala wa Usajili wa Kampuni, ili kusaidia wananchi wanaokutana na changamoto wakati wa usajili.
“Lengo ni kuhakikisha mwananchi akikwama, anapata msaada kutoka kwa watu wanaotambulika na kuaminika,” amesisitiza Bw. Nyaisa.











.jpg)





.jpg)


