


NA OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA
MTOTO mwenye changamoto ya usikivu anaweza kukaa darasani bila kuelewa kinachofundishwa, mwingine mwenye usonji anaweza kutengwa na jamii kwa kudhani hawezi kujifunza, huku mwenye changamoto ya viungo akiachwa nyumbani kwa sababu familia haijui kuwa anaweza kupata elimu kulingana na uwezo wake.
Hata hivyo, hali hiyo inaanza kubadilika katika Jiji la Dodoma kupitia Kituo cha Utambuzi na Upimaji wa Kubaini Mahitaji Maalumu ya Ujifunzaji kwa Watoto (ESRAC), kilichopo Shule ya Msingi Nkuhungu.

Kituo hicho, kilichoanzishwa mwaka 2022 kwa gharama ya Sh milioni 48.6, kinalenga kuwabaini watoto wenye mahitaji maalumu mapema, kufanya tathmini na kuwaunganisha na huduma za elimu na afya kulingana na mahitaji yao.
Kuanzishwa kwa ESRAC kunatokana na maelekezo na mwongozo wa Serikali wa kuhakikisha watoto wenye changamoto za ujifunzaji wanatambuliwa mapema na kupata huduma stahiki badala ya kuachwa bila elimu au kufichwa majumbani.
KITUO KINAFANYA NINI?

Afisa Elimu Maalumu wa Jiji la Dodoma, Issa Kambi, anasema ESRAC inahusika na utambuzi, upimaji na upangaji wa fursa stahiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu, hususan katika eneo la elimu.
Anasema kituo hufanya kazi kila siku, huku Jumanne na Alhamisi zikitengwa kwa ajili ya kliniki ambapo wazazi huwaleta watoto kwa uchunguzi, pamoja na wanafunzi kutoka shule mbalimbali wanaohitaji tathmini au mapitio ya awali.
Kwa watoto wanaobainika kuwa na changamoto za kiafya, kituo hutoa rufaa kwenda hospitali na kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili Mirembe.
Kwa watoto wenye changamoto za macho, baadhi yao huunganishwa na huduma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa pamoja na ufadhili wa Light for the World.
Aidha, wataalamu kutoka Mirembe, wakiwemo speech therapists, occupational therapists, physiotherapists na madaktari wengine, hutoa kliniki kituoni hapo na huduma hizo hutolewa bila malipo.
WATOTO 1,756 WAMEPIMWA

Msimamizi wa Kituo cha Upimaji ESRAC Nkuhungu, Neema Mukama, anasema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022, jumla ya watoto 1,756 wamepimwa, wakiwemo wavulana 905 na wasichana 851.
Kwa mujibu wa Neema, takwimu hizo zinaonyesha ukubwa wa mahitaji ya huduma za utambuzi na upimaji wa watoto wenye mahitaji maalumu, huku kituo kikiendelea kuwafikia watoto walioko katika jamii.
Anasema kupitia upimaji huo, watoto wamekuwa wakibainishwa changamoto zao na kuunganishwa na huduma zinazolingana na mahitaji yao, ikiwemo elimu, matibabu na huduma nyingine za kitaalamu.
WANAANZA KATA KWA KATA
Kambi anasema wataalamu wa kituo hicho wamekuwa wakifanya ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu kata kwa kata, hatua inayolenga kuwafikia hata wale ambao hawajawahi kufikishwa kituoni.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Denis Gondwe, anaeleza kuwa jiji hilo lina kata 41 na mitaa 222, ambapo timu za wataalamu hushirikiana na watendaji wa kata na mitaa, wenyeviti pamoja na wadau wengine kuwafikia watoto waliopo kwenye jamii.
Lengo, anasema, ni kuwabaini watoto ambao huenda hawajafikishwa kituoni na kuwawezesha kupata upimaji pamoja na huduma wanazohitaji.
Kambi anasema idadi ya watoto waliobainika imeongezeka kutoka takribani 600 miaka minne iliyopita hadi zaidi ya 1,700, jambo analolihusisha na kuendelea kwa zoezi la ubainishaji na uhamasishaji wa jamii.
BAADHI YA WAZAZI BADO WANAFICHA WATOTO
Pamoja na uwepo wa kituo hicho, bado kuna changamoto ya uelewa miongoni mwa baadhi ya wazazi na jamii, hali inayochangia baadhi ya watoto kuchelewa kupata huduma.
Neema anasema baadhi ya wazazi hawatoi taarifa sahihi kuhusu historia ya watoto wao wakati wa uchunguzi, jambo linaloweza kuwafanya wataalamu kutumia muda zaidi kubaini changamoto iliyopo.
“Katika zoezi la ubainishaji linalofanyika katika kata mbalimbali, tunakutana na maeneo ambayo ushirikiano na jamii unakuwa mdogo sana,” anasema.
Mwalimu Mkuu wa Kitengo cha Mahitaji Maalumu katika Shule ya Msingi Mlezi, Hashim Msemo, anasema changamoto nyingine ni baadhi ya watoto kufichwa majumbani na kufikishwa shuleni wakiwa wamechelewa.
“Mtoto unamkuta tayari ana miaka minane, tisa, wakati kwenye mwongozo wa upimaji inatakiwa kuanzia miaka mitano,” anasema.
WALIMU: MTOTO AKIBAINIKA, ANAPELEKWA KWENYE FURSA INAYOMFAA
Msemo anasema baada ya mtoto kubainika kuwa ana changamoto, wataalamu hushirikiana na wazazi, jamii, walimu na madaktari kutambua aina ya changamoto aliyonayo kabla ya kumpangia mazingira ya elimu yanayomfaa.
Anasema walimu nao wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuwabaini watoto wenye mahitaji maalumu na kutumia mwongozo unaowaelekeza katika utambuzi na ubainishaji.
“Walimu pia tumepata mafunzo ya namna ya kuwabaini watoto wenye mahitaji maalumu na kutumia mwongozo unaotuelekeza kuhusu utambuzi na ubainishaji,” anasema.
Naye Mwalimu Digna Temba, anayefundisha wanafunzi wenye ulemavu wa macho, anasema walimu huangalia viashiria mbalimbali, ikiwemo changamoto za uoni, usonji na changamoto za ufahamu.
“Mtoto anapoonekana kuwa na changamoto, huwasiliana na wataalamu wa kituo cha Nkuhungu kwa ajili ya ubainishaji wa awali,” anasema.
SHULE YA MLEZI YAWAFIKIA WATOTO MITAANI

Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mlezi, Magreth Kisanga, anasema shule hiyo yenye huduma za elimu jumuishi imekuwa ikiwafikia watoto wenye mahitaji maalumu kwa njia mbalimbali.
“Walimu hufanya home visiting kila Ijumaa kwa ajili ya kuwabaini watoto waliopo mitaani au wale ambao wameacha kuja shule kutokana na changamoto mbalimbali,” anasema.
Anaongeza kuwa mahusiano kati ya shule na jamii yamekuwa njia nyingine ya kuwafikisha watoto shuleni hapo.
Kwa mujibu wa Kisanga, Shule ya Msingi Mlezi ina wanafunzi 120 katika eneo la elimu maalumu, huku walimu wenye mafunzo maalumu wakiendelea kuwahudumia.
Hata hivyo, anasema changamoto ya usafiri ni miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya watoto kutohudhuria shule mara kwa mara.
WALIMU: WATOTO WANAWEZA KUBADILIKA
Msemo anasema baadhi ya watoto waliokuwa wamefichwa majumbani wameonyesha mabadiliko baada ya kuanza kupata elimu.
“Mfano, wapo watoto ambao walifika shuleni hapa wakiwa hawawezi kufanya baadhi ya shughuli za msingi, lakini baada ya kufundishwa wameanza kujitegemea zaidi,” anasema.
Anasema baadhi ya wazazi wamekuwa wakitoa ushuhuda wa mabadiliko yanayoonekana kwa watoto wao baada ya kuanza shule.
Hata hivyo, anasema changamoto ya usafiri bado inazuia baadhi ya watoto kuhudhuria masomo yao kwa mwendelezo mzuri.
DAKTARI: UCHUNGUZI WA MAPEMA NI MUHIMU
Daktari wa Kituo cha Afya Nkuhungu na mshiriki wa timu ya ubainishaji, Dkt. Rehema Magesa, anasema uchunguzi wa mapema unasaidia kubaini changamoto za mtoto kabla hazijawa kubwa zaidi.
“Watoto wenye changamoto za usikivu, uoni au changamoto nyingine za kiafya wanapaswa kubainishwa mapema na kupelekwa katika maeneo sahihi ya huduma,” anasema.
Dkt. Magesa anasema mojawapo ya changamoto wanazokutana nazo ni baadhi ya wazazi kutambua kwa kuchelewa hali za watoto wao, hasa kwa watoto wenye usonji.
Anaongeza kuwa imani potofu katika jamii nazo zinaweza kuchelewesha wazazi kutafuta ushauri wa kitaalamu.
Kwa mujibu wa daktari huyo, mtoto mwenye ulemavu anaweza kuwa na uwezo mkubwa katika eneo fulani hata kama anakabiliwa na changamoto katika baadhi ya masomo ya darasani.
CHUMBA MAALUMU CHA UPIMAJI WA USIKIVU
Katika kituo hicho pia kuna chumba maalumu kinachotumika kufanya ubainishaji wa awali kwa watoto wenye changamoto za usikivu.

Mwalimu Elizabeth Katunzi anasema kituo kina vifaa vya kisasa, vikiwemo audiometer na digital otoscope, vinavyosaidia kufanya uchunguzi wa awali wa masikio.
“Baadhi ya watoto wanaofikishwa hapa kituoni hugundulika kuwa na changamoto zinazoweza kutibiwa, kama nta nyingi au vitu vilivyoingia kwenye sikio na watoto hao hupewa rufaa kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu,” anasema.
Anasema huduma ya uchunguzi wa awali kituoni hapo hutolewa bila malipo na baada ya mtoto kubainika kuwa na changamoto, hupangiwa shule kulingana na mahitaji yake.
WATOTO WAPELEKWA SHULE KULINGANA NA MAHITAJI
Kwa watoto wenye changamoto kubwa ya usikivu, wataalamu hutoa rufaa na baada ya kuthibitishwa na daktari hupangiwa shule zinazolingana na mahitaji yao.
Katunzi anasema baadhi yao hupelekwa Shule ya Msingi Dodoma Viziwi, wengine Hombolo na wengine katika shule jumuishi zilizo karibu na maeneo wanayoishi.
Lengo ni kuhakikisha mtoto hapotezi fursa ya elimu kutokana na aina ya changamoto aliyonayo.
WAZAZI: USAFIRI NI CHANGAMOTO
Kwa upande wa wazazi, changamoto kubwa iliyotajwa ni usafiri.
Farida Khamis, mzazi wa watoto mwenye mahitaji maalumu, anasema gharama za usafiri zimekuwa mzigo, hasa kwa familia zinazowapeleka watoto shuleni kutoka maeneo ya mbali.
“Nauli imekuwa ikifikia kati ya Sh3,000 hadi Sh5,000, hali inayotuwia vigumu sisi wazazi wenye kipato kidogo,” anasema.
Anaishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuweka usafiri maalumu au mabweni kwa watoto wenye mahitaji maalumu ili kupunguza mzigo kwa wazazi.
Licha ya changamoto hiyo, anasema anaridhishwa na huduma zinazotolewa kituoni, lakini anasisitiza umuhimu wa kutafutiwa majawabu changamoto ya usafiri kwa watoto wenye ulemavu.
“WATOTO HAWAPASWI KUFICHWA”
Wadau waliohojiwa wanatoa ujumbe unaofanana kwa jamii kwamba watoto wenye mahitaji maalumu hawapaswi kufichwa majumbani.
Msimamizi wa kituo hicho, Neema, anasema watoto wenye changamoto mbalimbali wanapaswa kufikishwa katika vituo vya upimaji ili kubaini fursa stahiki kulingana na uwezo wao.
Anasema hata mtoto mwenye usonji, changamoto ya usikivu, ulemavu wa viungo au changamoto ya ufahamu anaweza kupata elimu na kujifunza kulingana na uwezo wake.
Naye Dkt. Magesa anasisitiza kuwa watoto wenye ulemavu wana haki ya kupata elimu na huduma nyingine muhimu na wanapaswa kuonekana ili jamii iweze kuwasaidia.
SERIKALI YAOMBWA KUONGEZA VITUO NA MAFUNZO
Pamoja na mafanikio yaliyoelezwa, watendaji wa kituo wameainisha maeneo yanayohitaji maboresho, ikiwemo mafunzo ya mara kwa mara kwa wataalamu wanaotumia vifaa vya kisasa.
Mahitaji mengine ni kuongezwa kwa vituo katika halmashauri nyingine na kuimarishwa kwa bajeti ya shughuli za ubainishaji ili kuwafikia watoto wengi zaidi.
Neema anasema baadhi ya vifaa vya kidijitali vimepatikana, lakini mafunzo ya matumizi yake yanahitajika mara kwa mara ili kuongeza ufanisi wa huduma.
Anaongeza kuwa baadhi ya wazazi kutoka mikoa mingine, ikiwemo Manyara na Moshi, wamekuwa wakifika Dodoma kutafuta huduma za upimaji.
DODOMA YAENDELEA KUPANUA ELIMU JUMUISHI
Kwa mujibu wa Afisa Elimu Maalumu wa Jiji la Dodoma, Kambi, jiji hilo lina jumla ya shule 213, ambapo takribani shule 60 zimebainishwa kutoa huduma ya elimu jumuishi.
Aidha, takribani shule 11 zina vitengo vya watoto wenye mahitaji maalumu, huku halmashauri ikiendelea kutumia klabu za elimu jumuishi katika shule mbalimbali.
Kambi anasema klabu hizo ni sehemu ya kuwafundisha wanafunzi kuhusu elimu jumuishi na kuwasaidia kupeleka ujumbe huo katika jamii.
Takribani miaka minne tangu kuanzishwa kwa ESRAC Dodoma, kituo hicho kimekuwa sehemu ya utambuzi wa watoto wenye mahitaji maalumu na kuwaunganisha na huduma za elimu na afya.
Kupitia ubainishaji unaofanyika kituoni na katika jamii, watoto wanaobainika kuwa na changamoto wamekuwa wakipatiwa tathmini, huduma za awali, rufaa na kupangiwa mazingira ya elimu yanayolingana na mahitaji yao.
Hata hivyo, changamoto bado zipo, ikiwemo uelewa mdogo wa baadhi ya wazazi, watoto kufichwa majumbani, usafiri, upungufu wa walimu na wataalamu katika baadhi ya maeneo pamoja na mahitaji ya mafunzo na bajeti kwa ajili ya shughuli za ubainishaji.
Kwa wazazi na wataalamu, ujumbe wao ni mmoja: mtoto mwenye mahitaji maalumu hapaswi kubaki nyumbani kwa sababu ya changamoto aliyonayo. Anatakiwa kutambuliwa, kupimwa na kupewa fursa ya elimu inayolingana na uwezo na mahitaji yake.







Na: OWM–TAMISEMI, Tunduma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali kupitia TARURA imetenga shilingi bilioni 15 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za maingilio na mchepuko mkoani Songwe, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri pamoja na usafirishaji wa bidhaa. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 6 zitatumika Wilaya ya Momba, ambapo bilioni 3 zitatumika Tunduma na bilioni 3 kwa maeneo mengine ya wilaya hiyo, huku bilioni 9 zikielekezwa katika wilaya za Mbozi, Ileje na Songwe.
Prof. Shemdoe ameyasema hayo Oktoba 15, 2026, baada ya kupewa fursa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kueleza hatua zinazochukuliwa na OWM–TAMISEMI katika kutatua kero zilizowasilishwa na wananchi wa Tunduma wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika ziara ya Makamu wa Rais ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Songwe.
Amefafanua kuwa ujenzi huo utasaidia kupunguza msongamano katika barabara ya Tunduma–Mpaka wa Zambia, barabara kuu ya TANZAM inayounganisha Igawa–Songwe–Tunduma, pamoja na barabara ya Mpemba–Tunduma, hususan eneo la mizani ya Mpemba.
“Mhe. Makamu wa Rais, TAMISEMI tuko tayari. Katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kujenga barabara za maingilio na mchepuko mkoani Songwe,” amesema Prof. Shemdoe.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu na kupunguza changamoto za usafiri zinazowakabili wananchi na wafanyabiashara, hasa katika maeneo yenye shughuli nyingi za biashara na usafirishaji wa mizigo ya ndani na kuvuka mipaka.
Katika sekta ya afya, Prof. Shemdoe amemueleza Makamu wa Rais kuwa OWM–TAMISEMI imetekeleza maelekezo ya kutenga shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Ivuna, kilichopo katika Jimbo la Momba, ambalo Mbunge wake ni Mhe. Condester Sichalwe. Amesema uwekezaji huo utaboresha upatikanaji na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
Kuhusu elimu, Prof. Shemdoe amesema Serikali inakamilisha ujenzi wa shule ya saba ya ghorofa, huku shule sita zikiwa zimekamilika. Ujenzi huo umewezesha kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya nafasi wakati wa kupokea wanafunzi watakaoanza kidato cha kwanza mwaka 2028 kwa mfumo wa double cohort, utakaowahusisha wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na darasa la sita kutokana na utekelezaji wa mtaala mpya. “Halmashauri ya Mji wa Tunduma iko tayari kuwapokea wanafunzi hao,” amesema.
Aidha, Prof. Shemdoe amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa jengo la ghorofa katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduma kwa ajili ya wodi ya mama na mtoto, ili kuongeza uwezo wa hospitali hiyo kutoa huduma za afya ya uzazi. Tunduma, kama ilivyo Katoro, ni miongoni mwa maeneo yenye idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa, ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizopo, watoto 1,500 huzaliwa kila mwezi; 800 katika vituo vya Serikali na 700 katika vituo vingine.
Prof. Shemdoe amesema uwekezaji huo katika barabara, elimu na afya unaonesha dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za kijamii na miundombinu, kupunguza changamoto za wananchi na kuweka mazingira bora kwa shughuli za kiuchumi na kijamii mkoani Songwe.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ameitaka Menejimenti na watumishi wa Wizara hiyo kuimarisha utendaji, uwajibikaji na kuhakikisha shughuli zote zinazotekelezwa zinaleta matokeo yanayopimika kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Gwajima ametoa maelekezo hayo Oktoba 15, 2026, jijini Arusha, wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara katika Ukumbi wa PAPU International Conference Center (PICC).
Amesema huduma za maendeleo na ustawi wa jamii ni uwekezaji katika mtaji watu na uwezo wa Taifa, hivyo Wizara inapaswa kuimarisha sera za huduma za malezi na ulinzi wa mtoto, familia, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, ustawi wa wazee na makundi maalum. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha programu na huduma za Wizara na Jamii Ajenda 2050 ili wananchi wapate huduma zenye ubora na fursa zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo.
Akizungumzia utendaji wa watumishi, Dkt. Gwajima ameitaka Menejimenti kuimarisha mashauriano kazini, kuboresha mazingira ya kazi na kushughulikia changamoto za watumishi kwa haki na kwa wakati. Amewataka watumishi kutekeleza majukumu yao kwa bidii, weledi, uadilifu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, huku akisisitiza matumizi sahihi ya teknolojia, uratibu kati ya Idara na Vitengo, pamoja na uwajibikaji unaozingatia matokeo.
Kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri amesisitiza kuwa tathmini ya robo ya kwanza inapaswa kuangalia si fedha zilizopokelewa na kutumika pekee, bali pia shughuli zilizotekelezwa na matokeo yaliyopatikana kwa wananchi. Ameelekeza taarifa za utekelezaji ziwasilishwe kabla ya mwisho wa Oktoba 2026, huku Menejimenti ikitakiwa kufuatilia maendeleo kila mwezi, kutatua vikwazo mapema na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa tija na kwa madhumuni yaliyoidhinishwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema mafanikio ya Wizara yanategemea uwajibikaji, nidhamu ya kazi na ushirikiano wa watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano na kutatua changamoto za jamii kwa wakati ili kuharakisha utekelezaji wa DIRA2050 inalenga kujenga jamii yenye watu wenye uwezo wa kutatua changamoto na kuleta maendeleo endelevu.
Naye Naibu katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa kikao hicho Wakili Amon Mpanju, amesema Wizara imejikita katika kuboresha maslahi ya watumishi, mazingira ya kazi na upatikanaji wa vitendea kazi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kuongeza uwajibikaji na kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.






























