Na Mwandishi Wetu
Halmashauri ya Mji Handeni imetoa mafunzo maalum ya Mfumo wa Kidigitali wa Taarifa za Shule (School Information System – SIS) kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi, Wakuu wa Shule za Sekondari pamoja na baadhi ya walimu, huku ikielezwa kuwa mfumo huo utasaidia kuongeza uwajibikaji kwa walimu na kudhibiti tatizo la utoro shuleni.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Januari 9, 2026, mjini Handeni, Kaimu Afisa Elimu Idara ya Sekondari ambaye pia ni Afisa Elimu Vifaa na Takwimu wa Halmashauri ya Mji Handeni, Montan Mathew, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Walimu Wakuu wa Shule za Msingi, Wakuu wa Shule za Sekondari pamoja na mwalimu mmoja kutoka kila shule ili waweze kutumia mfumo huo kwa ufanisi.
Amesema mfumo wa SIS utatumika kukusanya, kuhifadhi na kuchambua taarifa zote muhimu za shule na kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI imeelekeza mfumo huo kuanza kutumika rasmi mara shule zitakapofunguliwa Januari 13, 2026.
“Walimu hawa wanapaswa kuanza kutumia mfumo huu mara moja ili kuweka taarifa za shule zao. Sisi kama Halmashauri ya Mji Handeni tuna wajibu wa kuhakikisha mfumo unatumika kama ilivyoelekezwa, na tutafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara,” amesema Mathew.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mshikamano, Beatrice Chaeka, amesema mfumo huo utasaidia kuwa na takwimu zenye mpangilio mzuri ikilinganishwa na awali walipokuwa wakitumia karatasi ambazo wakati mwingine zilipotea au kuharibika.
Ameongeza kuwa mfumo wa SIS utakuwa suluhisho la changamoto mbalimbali ikiwemo utoro wa wanafunzi na walimu.
“Katika mfumo huu, mwanafunzi anapowekewa alama ya hayupo mara tatu mfululizo, ujumbe hutumwa moja kwa moja kwa mzazi. Hii itawasaidia wazazi kufuatilia mahudhurio na maendeleo ya watoto wao, kwani kuna baadhi ya wanafunzi wanatoka nyumbani lakini hawafiki shuleni,” amesema Chaika.
Naye, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwenjugo, John Rajabu, amesema hapo awali kulikuwa na changamoto katika mipangilio ya taarifa za shule, lakini ujio wa mfumo wa SIS utaboresha usimamizi wa shule kwa ujumla.
Amesema mfumo huo utaongeza uwajibikaji kwa walimu katika ufundishaji pamoja na kuwahusisha wazazi kikamilifu katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao kielimu.





























