Na WyEST,Tianjin, China

Na WyEST,Tianjin, China

DAR ES SALAAM

.jpeg)






Na, Mwandishi wetu Pretoria - Afrika Kusini.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Ushirikiano wa Nchi Tatu za Tanzania, Msumbiji na Afrika Kusini, unaolenga kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu unaovuka mipaka.
Mkutano huo umefanyika , Oktoba 15, 2026, jijini Pretoria, Afrika Kusini, ukitanguliwa na kikao cha viongozi waandamizi kilichofanyika Oktoba 14, mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano huo, Profesa Kabudi amezitaka nchi hizo kuimarisha ushirikiano kwa kubadilishana taarifa za kiintelijensia ili kuwabaini wahalifu, kuvunja mitandao yao na kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka.
“Lengo la mkutano huo lilikuwa kujadili mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo katika kudhibiti usafirishaji haramu wa dawa za kulevya katika ukanda wa Bahari ya Hindi, pamoja na uhalifu mwingine unaojumuisha usafirishaji haramu wa binadamu, utekaji nyara na uhalifu wa kuvuka mipaka”amesema Profesa Kabudi
Amesema kuwa ushirikiano wa karibu kati ya vyombo vya usalama ni muhimu katika kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyotumia mianya ya mipaka na udhaifu wa mifumo ya udhibiti kutekeleza shughuli haramu.
Katika hatua nyingine, Profesa Kabudi amewakaribisha rasmi wanachama wa TPC nchini Tanzania, ambayo kwa kushirikiana na Kenya na Uganda inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika Juni na Julai 2027.
Alisisitiza nchi hizo kutumia fursa ya mashindano hayo kuimarisha mikakati ya kupambana na dawa za kulevya na uhalifu mwingine, akieleza kuwa matukio makubwa ya kimataifa yanaweza kutumiwa na wahalifu kutekeleza shughuli zao haramu.
Aidha, mkutano huo uliridhia maombi ya Angola na Uganda kujiunga na TPC, ambayo makao makuu yake yako nchini Msumbiji.
Kwa hatua hiyo, umoja huo sasa unaundwa na nchi tano ambazo ni Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Tanzania na Uganda, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka.
Mkutano huo uliwakutanisha pia viongozi waandamizi kutoka mamlaka za kudhibiti dawa za kulevya, vyombo vya polisi na wadau wa maendeleo, wakiwemo Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) na Umoja wa Ulaya.
Washiriki kutoka Angola, Uganda, Comoro, Shelisheli, Eswatini, Uingereza na Marekani pia walishiriki majadiliano kuhusu namna bora ya kukabiliana na changamoto za uhalifu, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

Na Mwandishi Wetu - Simanjiro
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mhe. Kaleya Melita Mollel ameitaka Kamati za Usimamizi wa Maafa wa Halmashauri hiyo kutekeleza yale yaliyomo kwenye Mpango wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa wa Halmashauri ya Simanjiro ili kuimarisha usimamizi wa maafa katika Wilaya hiyo.
Mhe. Mollel ameyasema hayo leo Oktoba 16, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya hiyo wakati akizindua Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa Wilayani ukiwa na lengo la kutoa miongozo na taratibu za kujiandaa na kukabiliana na maafa katika halmashauri ya wilaya na hasa katika kipindi hiki cha mvua za msimu.
“Nitoe wito nendeni mkatekeleze yaliyomo kwenye mpango huu, mpango huu usibaki kwenye makaratasi kwani ni nyezo muhimu ya usimamizi wa maafa katika halmashauri yetu” amesisitiza Mhe. Mollel.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Kanali Selestine Masalamado amesema kuwa, mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia matokeo ya tathmini ya vihatarishi na uwezo wa wilaya wa kukabiliana na maafa, pamoja na historia ya matukio ya maafa yaliyoikumba Wilaya ya Simanjiro.
“Mpango huu ni matokeo ya mchakato shirikishi uliohusisha taasisi na wadau mbalimbali wa usimamizi wa maafa katika ngazi ya wilaya hivyo tunatarajia mpango huu utawezesha masuala mbalimbali ikiwemo uratibu wa shughuli za usimamizi wa maafa katika hatua zote za usimamizi wa maafa (Kuzuia, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali)” amefafanua Kanali Masalamado.
Aidha, ameongeza kuwa, maandalizi ya mpango huo ni hatua muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 (Toleo la Mwaka 2025) pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022, kwa kuweka mikakati madhubuti ya kujiandaa na kukabiliana na maafa.
“Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Idara ya Usimamizi wa Maafa, itaendelea kushirikiana nanyi, Wilaya ya Simanjiro katika shughuli za usimamizi wa maafa kwani usimamizi madhubuti wa maafa ni jukumu letu sote, kila mmoja ashiriki sasa na achukue hatua katika eneo lake, ili kulinda maisha na mali” ameongeza Kanali Masalamado.
Tathmini ya vihatarishi, uwezekano wa kutokea na uwezo wa kukabili maafa iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro inaonesha kuwa, halmashauri hiyo inakabiliwa na majanga ya ukame, mafuriko, Migongano kati ya Wanyamapori na binadamu, moto magonjwa ya milipuko (binadamu, mifugo na wanyamapori) upepo mkali pamoja na mimea vamizi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Hawa Mchafu, akizungumza wakati kamati yake ilipokutana na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi Ajira na Mahusiano na Mfuko wa PSSSF, jijini Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu akizungumza katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii leo tarehe 16/10/2026 Bungeni, Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii leo Bungeni, jijini Dodoma
Mhe. Kangi Lugola, Mb akichangia hoja wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, leo tarehe 16/10/2026
✅ Yasema PSSSF imekuwa faraja kwa Wafanyakazi
Na, Mwandishi wetu - Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Hawa Mchafu, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wa kulipa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo PSSSF, hatua iliyosaidia kuimarisha mifuko hiyo na ustawi wa wastaafu nchini.
Mhe. Mchafu ametoa pongezi hizo leo Oktoba 16, 2026 jijini Dodoma wakati kamati hiyo ikipokea taarifa kuhusu mwenendo wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) katika kufuatilia michango ya watumishi wa Umma, mafanikio, changamoto na hatua za utatuzi.
Mhe. Mchafu amesema kulipwa kwa deni hilo imewezesha kuongeza kasi ya ulipaji mafao kwa wastaafu. Vilevile, amempongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, kwa usimamizi wa mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo ni mhimili muhimu wa ustawi wa wananchi nchini.
Kwa upande wake, Mhe. Sangu amesema Serikali imelipa kiasi cha shilingi trilioni 2.09 kupitia Hati Fungani ikiwa ni kwa ajili ya michango ya wanachama ambayo haikuwasilishwa katika mfuko kwa kipindi cha utumishi kabla ya mwaka 1999.
Aidha, amesema kuanzia Julai hadi Septemba 2026, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekusanya kiasi cha shilingi bilioni 839.98, hali inayoonesha juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa michango ya wanachama.
Kadhalika, amesema kuwa ongezeko la ufanisi katika ukusanyaji wa michango limechangiwa na matumizi ya mifumo bora ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwemo mfumo wa Billing Portal, unaorahisisha michakato ya utozaji na ufuatiliaji wa michango.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo, amesema Mfuko umeendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama wake kupitia mifumo ya kidijitali, inayolenga kuongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma.
Amesema, hatua hizo zinaonesha jitihada za Serikali na PSSSF katika kuimarisha usimamizi wa hifadhi ya jamii, kuboresha huduma kwa wanachama na kulinda maslahi ya wastaafu nchini.
MWISHO
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba amesema wananchi wanaoishi katika maeneo ya mijini yenye sura ya vijijini watanufaika na huduma ya umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), hatua inayolenga kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini kupata huduma hiyo kwa gharama nafuu.
Akizungumza leo Octoba 16, 2026 jijini Mbeya, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, Mhe. Salome amesema Serikali imefanyia kazi maelekezo kuhusu utaratibu huo, ambapo maeneo husika tayari yametambuliwa na hatua za awali za manunuzi ya vifaa zinaendelea.
Amesema utaratibu huo unalenga kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo kisheria ni ya mijini lakini yana hali inayofanana na vijijini wanapata fursa ya kuunganishiwa umeme kwa gharama nafuu, kwa kuzingatia hali zao za kiuchumi.
Aidha, ameeleza kuwa kwa wananchi wa mijini ambao hawana uwezo wa kulipa gharama za kuunganishiwa umeme za shilingi 320,000 kwa mara moja, Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, imezindua mfumo unaomwezesha mteja kuunganishiwa umeme kwanza na kulipa gharama hizo kidogokidogo kulingana na matumizi yake ya umeme.
Mhe.Salome amesisitiza kuwa, hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kurahisisha upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wananchi wa makundi mbalimbali, kwa lengo la kuongeza matumizi ya umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya jamii nchini.