Morogoro:
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) leo imeongoza kampeni ya kupanda miti mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani, inayofikia kilele chake kila mwaka tarehe 22 Machi, kwa lengo la kulinda vyanzo vya maji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati zoezi hilo, Wilfred Mwakalosi, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Bonde la Maji la Wami Ruvu na Wakala wa Huduma za Misitu ( TFS) wamefanikiwa kupanda miti zaidi ya 5,000 katika eneo linalozunguka mto Lukulunge, Kata ya Mzumbe, mkoani Morogoro.
Mwakalosi alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuhifadhi mazingira, vyanzo vya maji na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kqtika maeneo mbalimbali nchini. “Morogoro ni miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na vyanzo vingi vya maji hapo awali, lakini kwa sasa hali imebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, hivyo kutishia upatikanaji wa maji kwa wakazi wake” alieleza.
Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wa Wilaya ya Morogoro, Stanley Kweka, alisema uharibifu wa misitu umechangia kupungua kwa kina cha maji katika Bwawa la Mindu, huku mmomonyoko wa udongo ukiendelea kuwa tatizo kubwa hivyo upandaji wa miti ni suluhisho muhimu katika kulinda kingo za mito na kuhakikisha vyanzo vya maji vinabaki salama kwa matumizi ya sasa na baadaye.
Naye Meneja wa Uratibu wa Mazingira na Jumuiya za Watumia Maji kutoka Bodi ya Bonde la ya Maji la Wami/Ruvu Janeth Kisoma,alisema mto Lukulunge ni chanzo muhimu kinachochangia maji katika Bwawa la Mindu, ambalo linahudumia zaidi ya asilimia 75 ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro, hivyo uhifadhi wake unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.


Post A Comment: