Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Moremi Marwa, Julai 4, 2025, amefanya ziara maalum katika Banda la TTCL kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (SabaSaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Bw. Marwa alipokelewa na wataalamu waandamizi wa TTCL, ambao walimtembeza katika maeneo mbalimbali ya banda hilo na kumweleza kwa kina kuhusu huduma na teknolojia zinazotolewa na Shirika hilo.
Miongoni mwa huduma zilizowasilishwa ni pamoja na Faiba Mlangoni, inayowezesha upatikanaji wa intaneti ya kasi moja kwa moja majumbani na maofisini, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya TTCL kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za mawasiliano kwa gharama nafuu.
Pia alielezwa kuhusu Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), ambao tayari umesambazwa katika mikoa yote 26 na wilaya 112 kati ya 139 nchini. Mkongo huo umeunganisha Tanzania na nchi jirani na kuchochea matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Huduma nyingine alizotembelea ni pamoja na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Taarifa Kimtandao (NIDC), chenye uwezo wa kisasa wa kuhifadhi na kulinda taarifa muhimu za taasisi na kampuni mbalimbali, na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu alifahamishwa kuhusu huduma ya Call Center ya TTCL inayosaidia mashirika kuwasiliana kitaalamu na wateja wao, pamoja na WiFi ya Umma (Public WiFi) inayowawezesha wananchi kupata huduma ya intaneti kwa urahisi katika maeneo ya wazi.
Katika kuendeleza ushirikiano wa kimkakati, Bw. Marwa pia alitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali rafiki, ikiwemo Shirika la Posta Tanzania (TPC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), pamoja na Banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Katika kila banda, alielezwa kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano ili kufanikisha malengo ya pamoja ya kidijitali na kiuchumi kwa maendeleo ya Taifa.















