Na OWM (KAM) - Kigali
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Zuhura Yunus, amewataka wajasiriamali wa Tanzania wanaoshiriki Maonesho ya 26 ya Jua Kali nchini Rwanda kuongeza ubunifu katika uzalishaji wa bidhaa ili kukidhi mahitaji ya soko na kuvutia wateja wengi zaidi ndani na nje ya nchi.
Ametoa wito huo Novemba 5, 2026, alipotembelea mabanda ya Tanzania katika Viwanja vya Gikondo, Jijini Kigali, ambapo maonesho hayo yanaendelea.
Bi. Zuhura amesema ubunifu ni nyenzo muhimu katika kukuza biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa, hivyo amewahimiza kuzingatia matumizi ya teknolojia, ubora wa bidhaa, vifungashio vinavyovutia na kuboresha namna ya kuwasilisha bidhaa zao kwa wateja.
Aidha, amewahimiza kutumia fursa ya maonesho hayo kujifunza kutoka kwa wenzao wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao ya kibiashara itakayowawezesha kupata masoko mapya na kukuza mitaji yao.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Alana Nchimbi, amesema ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kutangaza bidhaa zao, kuwaunganisha na fursa za masoko na kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mjasiriamali Ali Suleimani amesema maonesho hayo yamemwezesha kupata tuzo ya Msafirishaji Bora wa Mwaka (Best Exporter of the Year) kwa ukanda wa Afrika Mashariki, kutokana na ubunifu aliouweka katika bidhaa zake zilizovutia wateja wengi.
Bahati Mnyasa kutoka Wilaya ya Bunda amesema ni mara yake ya kwanza kushiriki maonesho hayo, ambapo amefanikiwa kupata soko la dagaa zaidi ya kilo 70, na ameiomba Serikali iendelee kuwaratibu ili kupata fursa zaidi za masoko.
Khadija Fussi kutoka Tanga ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha wajasiriamali kufika Kigali, ambapo amesema wananchi wengi wa Rwanda wameonyesha kupenda bidhaa za Tanzania.
Jumla ya wajasiriamali 350 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanaendelea kushiriki maonesho hayo yanayotarajiwa kuhitimishwa Novemba 8, 2026.
Maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kutangaza bidhaa za Kitanzania, kujenga mahusiano ya kibiashara na kufungua fursa mpya za masoko katika ukanda wa Afrika Mashariki.





Post A Comment: