Na. WMA - DODOMA,

Wakala wa Vipimo (WMA) imesema matumizi ya vipimo sahihi ni msingi muhimu wa kuimarisha uzalishaji viwandani, kulinda haki za wafanyabiashara na walaji, na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Mwaka 2003 (Toleo la 2025), uliofanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma.

Akizungumza katika tukio hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Bw. Alban Kihulla, amesema vipimo sahihi vinajenga uaminifu katika biashara kwa kuhakikisha wanunuzi wanapata kiasi cha bidhaa kinacholingana na thamani ya fedha wanazolipa.

Amesema WMA inatekeleza jukumu hilo kwa kukagua bidhaa zilizofungashwa zinazozalishwa nchini pamoja na zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kupitia bandari na vituo vya mipakani, ili kuhakikisha kuwa uzito au ujazo ulioainishwa kwenye vifungashio unalingana na kiasi halisi cha bidhaa kilichomo.

“Mnunuzi wa ndani au wa nje ya nchi anapochukua bidhaa yenye nembo ya Made in Tanzania, anatakiwa kupata kile hasa kilichoandikwa kwenye kifungashio. Hiyo ndiyo kazi yetu, na ndiyo sababu tunaziona sera hizi kama fursa ya kuimarisha imani kwa bidhaa za Kitanzania,” amesema Bw. Kihulla.

Ameeleza kuwa WMA pia hushirikiana na taasisi na mashirika ya vipimo ya kikanda na kimataifa katika kuimarisha ulinganifu wa vipimo na kusaidia kupunguza vikwazo vya biashara vinavyohusiana na vipimo.

Akizungumzia biashara ya mazao, amesema WMA inaendelea kuhakiki mizani inayotumika katika vituo vya ununuzi na viwanda vya usindikaji ili kuhakikisha wakulima wanapimiwa kwa usahihi na kulipwa kulingana na uzito halisi wa mazao yao.

“Mkulima anapouza korosho, kahawa au pamba, mizani inayotumika lazima iwe sahihi ili alipwe kwa uzito halisi wa mazao yake. Tunaendelea kuhakiki mizani katika vituo vya ununuzi na viwanda vya usindikaji, na kupambana na ufungashaji wa lumbesa unaomnyima mkulima haki yake,” amesema.

Kwa upande wa wajasiriamali wadogo na wa kati, amesema matumizi ya vipimo sahihi huwasaidia kufungasha bidhaa kwa kiasi kilichoainishwa, kudhibiti upotevu na kujenga uaminifu kwa wateja.

Amesema WMA inaendelea kutoa elimu kupitia njia mbalimbali, zikiwemo redio na televisheni, ili kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara kuelewa na kuzingatia matakwa ya vipimo katika shughuli zao. Wakala pia hutumia klabu za vipimo mashuleni kujenga uelewa wa matumizi ya vipimo sahihi tangu umri mdogo.

Aidha, amesema ukuaji wa viwanda na uwekezaji unaongeza mahitaji ya huduma za vipimo, ikiwemo uhakiki wa mizani, mita za umeme na mita za gesi asilia, pamoja na idhini za miundo ya vipimo vinavyokusudiwa kutumika katika shughuli zinazodhibitiwa kisheria.

Ameongeza kuwa WMA inaendelea kuboresha mifumo ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, sambamba na kuimarisha ukaguzi wa bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazoagizwa kutoka nje, pamoja na uhakiki wa vipimo vinavyotumika viwandani na katika biashara.

“Tunawaomba wananchi wahakikishe mizani na vipimo wanavyotumia vina alama ya uhakiki ya WMA, na watoe taarifa pale wanapoona kipimo kisicho sahihi. Kipimo sahihi ni haki ya kila mwananchi,” amesisitiza.

WMA ni miongoni mwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara zilizoshiriki maonesho na kongamano lililoambatana na uzinduzi huo. Wananchi na wafanyabiashara waliotembelea banda la Wakala walipata elimu kuhusu matumizi ya vipimo sahihi na huduma zinazotolewa na WMA.

Sera hizo zinalenga kuimarisha maendeleo ya viwanda na ujasiriamali kwa kuongeza uzalishaji, thamani ya malighafi za ndani, fursa za ajira na upatikanaji wa mitaji na masoko kwa wajasiriamali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: