Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imezindua p programu ya Elimu ya fedha kupitia mfumo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, ikiwa ni hatua inayolenga kuwajengea vijana uwezo wa kusimamia fedha zao kwa ufanisi na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha katika maisha yao ya sasa na baadaye.

Akizungumza leo Novemba, 9 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi huo, Gavana BoT, Emmanuel Tutuba, amesema programu hiyo ni matokeo ya ushirikiano wa taasisi hizo mbili ulioanzishwa kupitia makubaliano yaliyosainiwa mwezi Mei mwaka huu,

Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa ya kifedha yatakayowasaidia kutumia vizuri fedha wanazopata wakiwa vyuoni.

"Elimu ya fedha ni nyenzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla, hususan katika kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayotambua sekta ya fedha kuwa miongoni mwa sekta muhimu katika mageuzi ya uchumi na kufikia malengo ya maendeleo endelevu,"amesema.

Amesema programu hiyo imejikita katika maeneo muhimu ya usimamizi wa fedha binafsi, yakiwemo upangaji wa bajeti, uwekaji wa akiba, uwekezaji, ukopaji wenye tija, kujikinga na utapeli wa kifedha pamoja na kutafuta vyanzo halali vya kipato.

Gavana Tutuba ameeleza kuwa maudhui ya programu hiyo yameandaliwa na Benki Kuu na kuwekwa katika vitabu maalumu ambavyo vitapatikana kupitia tovuti ya BoT pamoja na mifumo ya kidijitali ya HESLB, ikiwemo SIPA, ili kuwawezesha wanafunzi wanufaika wa mikopo na wale wasionufaika kupata elimu hiyo kwa urahisi.

Amesisitiza umuhimu wa kupanga matumizi, amewataka wanafunzi kuzingatia vipaumbele vya msingi badala ya kuelekeza fedha wanazopata katika matumizi yasiyokuwa na tija. Amesema matumizi yasiyopangwa yanaweza kuathiri maendeleo ya kitaaluma na kuchelewesha ndoto za wanafunzi, hivyo ni muhimu kila mmoja kuwa na bajeti na kuifuata.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, amesema ushirikiano kati ya taasisi hizo ni hatua muhimu inayozidi kupanua wigo wa huduma za bodi.

Ameeleza kuwa jukumu la HESLB haliishii katika kutoa mikopo na ufadhili wa elimu ya juu, bali pia kuhakikisha wanufaika wanakuwa na uelewa wa namna bora ya kutumia fedha wanazopata.

"Elimu hii itasaidia wanafunzi kuelewa umuhimu wa mikopo kama nyenzo ya uwezeshaji na maendeleo, sambamba na kuwajengea uelewa kuhusu wajibu wa kurejesha mikopo kwa wakati ili kuhakikisha mfumo wa mikopo unaendelea kuwa endelevu na kutoa fursa kwa vizazi vijavyo,"amesema.

Ameongeza kuwa programu hiyo itatumia mfumo wa kugawa fedha kwa kuzingatia mahitaji muhimu, akiba na fedha za dharura, ili kuwasaidia wanafunzi kuepuka matumizi yasiyopangwa na changamoto za kifedha zinazoweza kuhatarisha masomo yao.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: