Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka mkazo katika kuimarisha matumizi ya mifumo rasmi ya malipo ya kielektroniki ili kupunguza utegemezi wa fedha taslimu na kujenga uchumi wa kisasa wenye usalama, ufanisi na ushindani katika shughuli za biashara nchini.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, wa kisasa na wa kipato cha juu, ambapo teknolojia na uchumi wa kidijitali vimetajwa kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za maendeleo.
BoT imesisitiza kuwa uchumi wenye matumizi madogo ya fedha taslimu haumaanishi kuondoa kabisa matumizi ya fedha hizo, bali kupunguza utegemezi wake kwa kuhamasisha wananchi na wafanyabiashara kutumia mifumo rasmi ya malipo ya kielektroniki.
Akizungumza Novemba 11, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa BoT, Lucy Shaidi, katika mkutano maalumu wa kuelimisha wafanyabiashara wa Kariakoo kuhusu matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali, amesema lengo ni kuwajengea uelewa kuhusu mifumo iliyopo, faida zake na namna ya kuitumia kwa usalama.
Amesema mkutano huo pia umelenga kutoa fursa kwa BoT kusikiliza maoni na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara katika matumizi ya mifumo hiyo ili kupata suluhisho na kuboresha huduma za malipo nchini.
“Mkutano huu pia umeandaliwa kutoa nafasi kwa BoT kusikiliza maoni na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara katika matumizi ya mifumo hiyo, ili kujadili kwa pamoja namna ya kuboresha huduma za malipo nchini,” amesema.
Shaidi ameeleza kuwa mifumo ya malipo inajumuisha njia, vifaa na taratibu zinazowezesha fedha kuhamishwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa usalama na uhakika.
Amezitaja njia hizo kuwa ni pamoja na kadi za benki, mashine za malipo (Point of Sale), simu za kiganjani, huduma za benki mtandao, lipa namba, misimbo milia (QR Code), hundi na uhamishaji wa fedha kutoka benki moja kwenda nyingine.
Amesema matumizi ya mifumo hiyo yana umuhimu mkubwa katika kulinda mitaji ya wafanyabiashara kwa kupunguza hatari za wizi, kupokea noti bandia na changamoto za kubeba kiasi kikubwa cha fedha taslimu.
Aidha, amebainisha kuwa kila muamala unaofanyika kwa njia ya kidijitali huacha kumbukumbu zinazomwezesha mfanyabiashara kufuatilia mauzo yake, kutathmini mwenendo wa biashara na kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza katika matumizi ya fedha.
Kwa mujibu wa Shaidi, kumbukumbu hizo zinaweza pia kuongeza fursa za wafanyabiashara kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kwa kuwa zinatoa taarifa zinazoonesha mwenendo na shughuli za biashara zao.
Ameongeza kuwa malipo ya kielektroniki yanaweza kupanua wigo wa biashara kwa kuwawezesha wafanyabiashara kuhudumia wateja wengi zaidi, wakiwemo wanaopendelea kufanya malipo bila kutumia fedha taslimu.
Katika kuimarisha matumizi ya mifumo hiyo, amesema BoT imejenga na kusimamia miundombinu ya malipo ya kidijitali, ikiwemo Mfumo wa Malipo ya Papo Hapo Tanzania (TIPS), unaowezesha kufanya malipo kupitia lipa namba na misimbo milia ya QR.
Amesema benki hiyo pia inaendelea kutoa leseni na kusimamia watoa huduma za fedha pamoja na kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma rasmi za kifedha na kunufaika na fursa zinazotokana na uchumi wa kidijitali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Donath Kibwana, akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, ameiomba BoT kuhakikisha mifumo ya malipo ya kidijitali inakuwa huduma yenye gharama nafuu badala ya kuonekana kama njia ya kuongeza mapato.
Amesema wafanyabiashara wanatambua faida za mifumo hiyo, ikiwemo kuwezesha miamala kufanyika papo hapo bila kulazimika kutumia muda kwenda benki kusubiri fedha taslimu, lakini wameomba makato yanayotozwa yaangaliwe kwa kuzingatia viwango vinavyotumika katika nchi nyingine.
Kibwana ametoa mfano wa Kenya, ambako amesema matumizi ya fedha taslimu yamepungua kutokana na kuimarika kwa mifumo ya malipo ya kielektroniki, akisisitiza umuhimu wa Tanzania kuweka mazingira rafiki yatakayowavutia wafanyabiashara kutumia huduma hizo.
Amesema jumuiya hiyo inathamini nafasi iliyopewa na BoT kujadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara, huku akiiomba benki hiyo kuendeleza vikao vya majadiliano ili kuimarisha mawasiliano, kutatua changamoto na kuweka mazingira bora ya matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali nchini.

Post A Comment: