NA EMMANUEL MBATILO, PWANI
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, amewapongeza wanachama wa Umoja wa Maendeleo ya Kiluvya (KIUMA) kwa kudumisha umoja na mshikamano unaowawezesha kusaidiana katika changamoto za kijamii.
Magoti ametoa pongezi hizo leo Oktoba 14, 2026 wakati wa maadhimisho ya miaka mitatu ya KIUMA yaliyofanyika Kiluvya, ambapo amewashauri wanakikundi kuanzisha akaunti maalumu ya kuweka akiba kwa ajili ya kutekeleza mipango yao ya maendeleo.
Amesema umoja huo ni mfano wa ushirikiano katika jamii na kusisitiza umuhimu wa wanachama kuendelea kulinda mshikamano wao ili uweze kuzaa matunda zaidi katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
“Mkifungua akaunti hata kesho, nitachangia Sh. 500,000 kuwaunga mkono ili muendelee na mshikamano mlionao,” amesema Magoti.
Aidha, amesema ziara ya Waziri wa Ujenzi imezaa matunda kwa kuwa eneo hilo limehakikishiwa kuanzishwa kwa huduma za daladala katika njia ya Kisarawe–Kiluvya, sambamba na mpango wa kukarabati na kuboresha barabara hiyo ili kurahisisha usafiri kwa wananchi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutafuta eneo la kujenga kituo cha huduma za pamoja (One Stop Centre) kitakachowezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za Serikali karibu na makazi yao, badala ya kusafiri hadi Kisarawe mjini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa KIUMA, Mathew Msami, amesema umoja huo ulianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha watu wenye dhamira ya kusaidiana, kushirikiana na kujenga maendeleo ya pamoja, hasa wakati wa misiba na changamoto nyingine za kijamii.
Amesema kaulimbiu ya umoja huo, “Jirani Yako ni Ndugu Yako,” inaakisi falsafa ya upendo, mshikamano, uaminifu na kujitolea kwa wanachama katika kuhakikisha hakuna mwanachama anayekabiliwa na changamoto peke yake.
Msami amesema katika kipindi cha miaka mitatu, KIUMA imepata mafanikio mbalimbali, yakiwemo kuimarika kwa uwezo wa kuchangia, uwazi katika usimamizi wa fedha na kujenga mahusiano mazuri miongoni mwa wanachama.
Ameeleza kuwa kiwango cha michango kilichokuwa takribani Sh. 335,000 katika hatua za mwanzo kimeongezeka hadi zaidi ya Sh. milioni 1.8, hali inayoonesha kuimarika kwa ushirikiano na moyo wa kujitolea miongoni mwa wanachama.
Amesema tangu kuanzishwa kwa umoja huo, jumla ya Sh. 51,345,998 zimekusanywa, ambapo Sh. 2,781,000 zilitumika kwa matumizi mbalimbali yanayohusiana na shughuli za umoja huo, huku Sh. 48,564,998 zikiwasilishwa kwa wafiwa.
Hata hivyo, amesema KIUMA inakabiliwa na changamoto zinazohusisha kuongezeka kwa mahitaji ya msaada, gharama za shughuli za kijamii na changamoto za mawasiliano, hivyo kuwataka wanachama kuendelea kuimarisha nidhamu, uwazi na uwajibikaji.
Msami pia ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga kituo kikubwa cha polisi katika eneo hilo na kuboresha barabara za mitaani ili kurahisisha usafiri na kuimarisha usalama wa wananchi.
Katika maadhimisho hayo, KIUMA pia iliandaa zoezi la upimaji wa afya na uchangiaji wa damu kwa hiari, likilenga kuhamasisha wananchi kujali afya zao na kusaidia kuokoa maisha ya wenye uhitaji.
Akizungumza katika zoezi hilo, mwanachama wa KIUMA, Ezekiel Simon, amesema kabla ya kuanza kuchangia damu, wananchi wamepata elimu kutoka kwa wataalamu kuhusu umuhimu wa kupima afya na kuchangia damu salama.
Amesema huduma hizo zimewapa wananchi fursa ya kufahamu hali zao za kiafya na kupata elimu inayoweza kuwasaidia kuchukua hatua mapema wanapobaini changamoto za kiafya.
Naye mkazi wa Kiluvya Madukani, Upendo Halisi, amesema amefurahishwa na mwitikio wa wananchi waliojitokeza kwa hiari kupima afya zao na kuchangia damu.
Amesema utoaji wa huduma hizo bila malipo umewasaidia wananchi kupata fursa ya kupima afya zao, ikiwemo shinikizo la damu na kiwango cha sukari, huduma ambazo baadhi yao huenda wasingezifuata wenyewe katika vituo vya afya.
Kwa upande wake, mtaalamu wa maabara kutoka Manispaa ya Ubungo, Paulo Moto, amesema zoezi hilo limefanyika kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa lengo la kukusanya damu itakayosaidia wagonjwa wenye mahitaji mbalimbali.
Amesema damu inayopatikana kupitia uchangiaji wa hiari husaidia kuokoa maisha ya wajawazito wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua, watoto wenye magonjwa kama selimundu, majeruhi wa ajali pamoja na wagonjwa wa saratani na magonjwa mengine yanayosababisha upungufu mkubwa wa damu.
Amesisitiza kuwa licha ya maendeleo ya teknolojia ya tiba, bado hakuna teknolojia inayoweza kuzalisha damu ya binadamu kwa matumizi ya wagonjwa, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kujitokeza kuchangia damu kwa hiari ili kuhakikisha inapatikana kwa wakati wote.
Amevitaka vikundi vya kijamii kuiga mfano wa KIUMA kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama katika kuhamasisha uchangiaji wa damu na kuimarisha afya za wananchi.
Maadhimisho ya miaka mitatu ya KIUMA yanaweka msisitizo katika kuendeleza mshikamano wa kijamii na kupanua shughuli za umoja huo ili usibaki katika kusaidiana wakati wa misiba pekee, bali pia ushiriki katika miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wanachama na jamii inayowazunguka.

Post A Comment: