Na Denis Chambi, Tanga.
WAKATI Kliniki ya Ardhi ikiwa bado inaendelea katika Mikoa yote hapa nchini, ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga imefanikiwa kutoa hatimiliki 254 huku wananchi zaidi ya 546 wakijitokeza kupatiwa huduma..
Hayo yameelezwa na Msajili msaidizi wa hati mkoa wa Tanga Mwajuma Kihiyo wakati akitoa tathmini ya uzinduzi wa Kliniki hiyo iliyofanyika wilayani Muheza ambapo ndani siku 4 walizokaa Wilayani humo muitikio wa wananchi umekuwa ni mkubwa asilimia 99 wakiwa wanahitaji kupata hati miliki za maeneo yao.
Akizungumza na waandishi wa Habari wakati zoezi hilo likiwa linaendelea katika ofisi za Ardhi wilaya ya Tanga ameeleza kuwa asilimia kubwa ya wananchi wenye maeneo tayari yameshapimwa hivyo kilichosalia ni kuwapatia hatimiliki ambazo zitawapa uhalali na kibali cha kuweza kuendelea maeneo yao.
"Kwa muda wa siku 4 tangu tumezindua Kliniki ya Ardhi wilaya ya Muheza tumeweza kuhudumia zaidi ya wananchi 546 waliweza kufika na kupata huduma na wengi kero yao kubwa ilikiwa ni hati kupata miliki kati yao 253 waliweza kupata hati zao pale pale" amesema Kihiyo.
Akizungumzia upande wa migogoro amesema kuwa kutokana na elimu waliyokuwa wanaendelea kuitoa kwa wananchi hali ya migogoro kwa mkoa wa Tanga imepungua kwa kiasi kikubwa tofauti na kipindi cha nyuma ambapo kwenye Kliniki hiyo hadi sasa wameweza kutatua migogoro 7 pekee.
" Kwa upande wa wa migogoro tuliyoipokea ilikuwa 7 ya wananchi ambao tayari walikuwa wameshasikilizwa awali lakini hawakuridhika hivyo walifika tukawasikiliza Tena na tukawapa majibu yao mtazamo wetu ni kurudi tena kuweka kambi ili kuhudumia wananchi wengi zaidi" amesema Msajili huyo.
Kliniki hiyo ambayo hufanyika kila mwaka ikiwa na lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi kutoka ofisi za Ardhi kila mkoa inatarajia kuhitimishwa October 3 2026 ikiwa imedumu kwa takribani siku 10.

Post A Comment: