Wananchi wa Jimbo la Same Mashariki, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari na kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu, huku wataalamu wakitoa tahadhari juu ya uwezekano wa kutokea kwa mafuriko, mmomonyoko wa udongo na changamoto nyingine zinazoweza kuhatarisha maisha na mali za wananchi.

Rai hiyo imetolewa katika semina maalumu iliyolenga kutoa elimu kuhusu El Niño, namna inavyoweza kuathiri jamii pamoja na hatua muhimu za kuchukua kabla na wakati na baada ya mvua hizo, semina hiyo imeandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, na kuwakutanisha Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Madiwani pamoja na wataalamu kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Akizungumza mara baada ya semina hiyo, Mbunge Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango, ameishukuru GST kwa kutoa elimu hiyo, akisema atahakikisha elimu na taarifa za tahadhari zinazohusiana na El Niño zinawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo kwa wakati, ili kuwawezesha kuchukua hatua za kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.


Kwa upande wake, Mjiolojia Mwandamizi kutoka GST, Gabriel Mbogoni, amesema maeneo mbalimbali waliyoyatembelea katika Wilaya ya Same yanakabiliwa na changamoto zinazofanana.


Mbogoni amesema baadhi ya shughuli za kilimo zinazofanyika katika maeneo hatarishi zinaweza kuchangia mmomonyoko wa udongo na kupasuka kwa ardhi, hali ambayo inaweza kuongeza madhara wakati wa mvua kubwa hasa kipindi hiki cha mvua za El Niño. 


Aidha, semina hiyo iliambatana na ziara fupi ya kutembelea eneo hatarishi la Mto Saseni, Kata ya Kihurio, ambapo wataalamu walibaini kuwa mto huo umeacha njia yake ya asili, GST imeshauri mto huo kurejeshwa katika njia yake ya asili ili kupunguza uwezekano wa kutokea kwa madhara kwa wananchi na mali zao, hususan endapo mvua kubwa zitanyesha kwa wingi.


Ushauri huo unatolewa wakati mamlaka za hali ya hewa zikiendelea kutoa taarifa na tahadhari kuhusu mwenendo wa mvua zinazotarajiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: