-Yafurahishwa na Mradi wa Kituo cha Gesi Asilia kwa matumizi ya Nishati Safi
Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Machano Othman Said, imezuru Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Agosti 20, 2026, kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Machano Othman Said, amesema wamefanya ziara NEMC kwa lengo la kuona namna taasisi hiyo inavyoendesha shughuli za kimazingira, kujifunza mafanikio na changamoto zake, pamoja na kubaini maeneo ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Akikaribisha ugeni huo, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo, amesema changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa mifumo ya ikolojia zinahitaji ushirikiano wa karibu kwa kubadilishana taarifa na uzoefu, kujenga uwezo wa wataalamu na kuandaa programu za pamoja za uhifadhi wa mazingira.
Akifafanua majukumu ya NEMC, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema NEMC inasimamia utekelezaji wa Sheria za mazingira, Tathmini ya Athari kwa Mazingira, udhibiti wa uchafuzi na ufuatiliaji wa uzingatiaji wa masharti ya mazingira.
Amesema Baraza linaendelea kuimarisha ukaguzi, mifumo ya kidijitali, elimu kwa umma na uwezo wa wataalamu katika kuhakikisha shughuli za maendeleo zinatekelezwa kwa kuzingatia mazingira.
Katika ziara hiyo, Kamati imetembelea Kituo Mama cha Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) cha TPDC, Ubungo, na kufurahishwa na mchango wa mradi huo katika matumizi ya nishati safi, kupunguza hewa ukaa na gharama za nishati, hivyo kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira.































Post A Comment: