Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeandika historia mpya mkoani Manyara kwa kuzindua rasmi utoaji wa programu Shahada (Degree) katika Kampasi ya Babati. 

Hafla hiyo ya uzinduzi wa 'Bachelor of Accountancy with Information Technology' na "Bachelor of Computer Science' imeongozwa leo Agosti 24, 2026 na Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Sillo.

Mhe. Sillo amesema wahitimu wa programu hizo watakuwa sehemu ya kizazi kipya cha wabunifu watakaosadia kuimarisha matumizi ya Teknolojia katika sekta ya fedha, elimu, afya,biashara, kilimo, utalii, viwanda na utoaji wa huduma za serikali.

Mkuu wa Chuo IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema" hatua hii ni mkakati wa IAA kuunga mkono juhudi za Serikali kusogeza elimu bora kwa wananchi na kuhakikisha wanapata elimu inayokidhi mahitaji ya dunia ya sasa na baadaye".

Aidha, Prof. Eliamani Sedoyeka ametangaza kuwa wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza watapatiwa huduma ya hosteli bure  hatua inayolenga kupunguza gharama kwa wazazi na kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira salama na tulivu.

Kampasi ya Babati ilianza mwaka 2014 ikiwa na wanafunzi 272, sasa ina wanafunzi 728 na IAA  inalenga kuongeza idadi ya wanafunzi Babati hadi 6,000 ifikapo mwaka 2031.

Aidha, IAA inaandaa mkakati wa kuanzisha programu za  elimu inayozingatia ujuzi (skills-based curriculum) katika maeneo kama Kilimo biashara, Uchakataji wa chakula,Uchakataji wa ngozi,Uhandisi wa uchomeleaji.Lengo ni kuwaandaa vijana wenye ujuzi wa vitendo, kuongeza fursa za kujiajiri na kuajiriwa, na kuendana na mahitaji ya soko la ajira.















Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: