Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Julai 31, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa bodi   hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Na.Alex Sonna-DODOMA

BODI  ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imetangaza mafanikio makubwa katika mwaka wa fedha 2025/26 baada ya wakulima nchini kulipwa zaidi ya Shilingi trilioni 2.298 kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS), huku kiasi cha mazao yaliyouzwa kupitia mfumo huo kikiongezeka kwa asilimia 43.6 ndani ya mwaka mmoja.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 31,2026 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli za bodi  hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo wa mwaka 2026/2027.

Amesema mfumo huo umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima kupata masoko na bei zenye ushindani na malipo ya uhakika kupitia taasisi za fedha.

Bw.Bangu amesema  katika mwaka wa fedha 2025/26, jumla ya kilo bilioni 1.122 za mazao tisa, yakiwemo korosho, ufuta, kahawa, kakao, mbaazi, dengu, choroko, soya na chai, ziliuzwa kupitia minada ya kidijitali inayosimamiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), ikilinganishwa na kilo milioni 781.6 mwaka uliotangulia.

"Ongezeko hili linaonyesha kuwa wakulima wengi zaidi wameendelea kuuamini Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuuona kuwa njia salama na yenye manufaa ya kuuza mazao yao," amesema  Bw. Bangu.

Amefafanua kuwa kutokana na mauzo hayo, Serikali za Mitaa zilikusanya zaidi ya Shilingi bilioni 61 kupitia ushuru wa mazao (CESS), huku thamani ya biashara yote iliyofanyika kupitia mfumo huo ikifikia Shilingi trilioni 2.679, hali inayodhihirisha mchango mkubwa wa mfumo huo katika kukuza uchumi wa Taifa.

Kwa mujibu wa Bw. Bangu, mfumo huo sasa unatekelezwa katika mikoa 23 na unahusisha mazao na bidhaa 18, tofauti na mwaka 2006 ulipoanza na zao moja pekee la korosho.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika kuimarisha mfumo huo ambapo katika mwaka wa fedha 2025/26 ilitoa Shilingi milioni 950 zilizotumika kuboresha mifumo ya TEHAMA, kutoa elimu kwa wakulima, kuimarisha ukaguzi wa maghala na kununua vitendea kazi vya kuongeza ufanisi wa huduma.

Mbali na mafanikio hayo, WRRB ilibainisha kuwa mapato yake ya ndani yameongezeka kwa kasi kutoka Shilingi bilioni 1.998 mwaka 2023/24 hadi Shilingi bilioni 5.870 mwaka 2025/26, hatua iliyoifanya Bodi kujigharamia zaidi ya asilimia 67 ya bajeti yake na kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali.

Aidha, mfumo huo ulizalisha jumla ya ajira 31,875 kupitia shughuli mbalimbali za ukusanyaji wa mazao, uhifadhi maghalani, usafirishaji, upimaji wa ubora na huduma nyingine katika mnyororo wa thamani wa biashara ya mazao.

Katika hatua nyingine, WRRB imetangaza mpango wa kupanua Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kutoka kwenye mazao ya kilimo kwenda katika sekta nyingine za uzalishaji, ambapo kwa mara ya kwanza sekta ya mifugo itaingizwa kwenye mfumo huo katika mwaka wa fedha 2026/27.

Bw. Bangu alisema mnada wa kwanza wa mifugo kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unatarajiwa kufanyika katika Wilaya ya Mvomero, huku bidhaa nyingine zikiwemo mwani, ngozi na mazao ya bustani zikitarajiwa kuingizwa kadri maandalizi ya kisera na kiutendaji yatakavyokamilika.

Ameongeza kuwa WRRB itaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali kwa kuboresha mifumo ya WRMS na WRS-MIS, kuongeza matumizi ya stakabadhi za kielektroniki pamoja na kuunganisha huduma za leseni, ukaguzi, biashara na malipo katika mfumo mmoja.

Pia amesema Bodi itaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), NBC na taasisi nyingine za fedha ili kuongeza upatikanaji wa mikopo inayotumia Stakabadhi za Ghala kama dhamana, hatua itakayowawezesha wakulima na wafugaji kupata mitaji bila kuuza bidhaa zao kwa hasara.

Bw. Bangu amesema mafanikio hayo ni matokeo ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na usimamizi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, akisisitiza kuwa WRRB itaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania, kuimarisha masoko ya wakulima na kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Julai 31, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa bodi   hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Julai 31, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa bodi   hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Julai 31, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa bodi   hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: