Kariakoo, Julai 30, 2026

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa kikodi Kariakoo imeendesha semina maalum kwa wafanyabiashara ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kutoa elimu ya kodi na kuwajengea uelewa kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi yaliyoanza kutumika kwa mwaka 2026/2027.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Meneja wa Mkoa Bw. Khalid Mchuma ambaye ni Kaimu Meneja Msaidizi huduma kwa Walipakodi,aliwataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kujifunza kwa kina mabadiliko ya sheria hizo ili yawezeshe utekelezaji sahihi wa majukumu yao ya kikodi na kuongeza kiwango cha utii wa hiari.

“Lengo la semina hii ni kutoa elimu kuhusu masuala ya kodi na kuwajengea wafanyabiashara uelewa wa mabadiliko ya sheria za kodi ili waweze kutekeleza wajibu wao kwa usahihi. Ninawakaribisha sana kushiriki kikamilifu katika semina hii na kutumia maarifa mtakayoyapata kuwaelimisha wengine katika maeneo yenu ya biashara kwa kuwa mabalozi.” Alisema Mchuma.

Kwa upande wake, Meneja wa elimu kwa mlipakodi (muwasilishaji) Bw. Paul Walalaze alifafanua kwa kina marekebisho mbalimbali yaliyofanyika katika sheria hizo pamoja na namna yatakavyotekelezwa katika shughuli za kila siku za wafanyabiashara.

Aidha, aliwahimiza washiriki kuendelea kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na TRA ili kuhakikisha wanazingatia matakwa ya sheria mpya.

Akieleza kwa Upande wa Sheria ya Kodi ya Mapato moja ya marekebisho ni katika Jedwali la kwanza Aya 2(3) Kutoa unafuu wa Kodi kwa mfanyabiashara mdogo anaye anza biashara kwamba hatalipa kodi kwa kipindi cha miezi 12 tokea aliposajili biashara yake, ameendelea kueleza kuwa kigezo kikubwa kinachozingagiwa ni lazima awe mtu binafsi anaye anza biashara yenye mauzo kuanzia Tshs sifuri hadi Tshs Milioni mia mbili kwa miezi 12.

Aidha amesema kiwango ukomo cha kutambulika walikodi wadogo sasa ni mwenye mauzo yasiozidi Tshs 200mil. kwa mwaka.

Kwa Upande wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani VAT mojawapo ya Mabadiliko ni katika kifungu kile cha 71(5) Kimeweka Sharti kwa Wakala wa Kodi ya Zuio(Withholding Agent) kuwasilisha na kufanya malipo ya VAT alizozuia ndani ya siku 10 ya mwezi unaofuata. Ikimaanisha wale wote wanaozuia VAT kwenye malipo ya bidhaa (3%) na huduma (6%) kuwasilisha taarifa hizo na kufanya malipo katika tarehe hiyo mpya kwenye kalenda ya Kodi.

Amewaeleza pia moja wapo ya Mabadiliko katika Sheria ya Miamala ya Kieletroniki hasa kwa kupitia Agizo la Waziri wa Fedha la tarehe 30.06.2026 kutaka Malipo yote yanayofanywa kwa ajili ya Pango, Ununuzi wa Nyumba , Mashamba, magari, Malipo kwenye Maduka makubwa ya ununuzi, Malipo kwa ajili Malazi, Migahawani, Ada za Shule za Msingi mpaka Vyuoni, Manunuzi yote kwenye viwanja vya Saba saba na Nane nane lazima yafanyike kieletroniki.

“Katika mabadiliko mapya ya sheria za kodi, bajeti kuu ya Serikali ina thamani ya Tshs 62.3Tril na TRA tunatakiwa kukusanya Tshs 41.8 Tril katika kuwezesha bajeti hiyo. Mabadiliko haya yanalenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kurahisisha utekelezaji wa sheria za kodi na kuboresha mazingira ya ulipaji wa kodi kwa walipakodi."

Aidha, washiriki walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali yaliyohusu utekelezaji wa mabadiliko hayo ya sheria za kodi. Maswali hayo yalijibiwa kwa ufafanuzi wa kina na mwasilishaji, jambo lililowasaidia washiriki kuelewa vyema athari za mabadiliko hayo na namna ya kuyazingatia katika biashara zao.

Washiriki walieleza kuridhishwa na mafunzo hayo, wakisema yamewapa uelewa mpana kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kikodi kwa kujiamini zaidi.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: