Timu ya mpira wa miguu ya Chuo Cha Uhasibu Arusha IAA Sports Club imefanikiwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Championship msimu ujao 2026/2027 baada ya kufuzu kwa kupata sare ya goli 1-1 dhidi ya klabu ya African Sports kutoka Mkoani Tanga
Akizungumza baada ya kutamatika kwa mchezo Kocha Mkuu wa IAA SC Zulkifri Iddi amewapongeza wachezaji wake kwa kuipatia timu matokeo na kuthibitisha kuwa walifanikiwa kufuata maelekezo aliyowapa ndani ya dakika zote tisini, huku akiupongeza Uongozi wa Chuo IAA kwa sapoti kubwa walioitoa iliyopelekea kuandika historia hii kubwa kwa taasisi na jiji la Arusha
Akitoa pongezi Mwenyekiti wa mashindano chama cha soka Mkoa wa Arusha Emmanuel Antony ameisifu IAA SC kwa kuandika historia hii kubwa na kukiheshimisha chama cha soka Mkoa wa Arusha na kuahidi ushirikiano kwa timu kuhakikisha inafanya vizuri na kupiga hatua zaidi ili kufika hatua ya kushiriki Ligi kuu ya Tanzania
Kwa upande wake mchezaji wa IAA SC ambaye ndiye Mfungaji wa goli pekee la timu amewapongeza wachezaji wenzake, benchi la ufundi na Uongozi wa Chuo pamoja na mashabiki wao kwa kushirikiana kufanikisha kufikia mafanikio haya makubwa na kuahidi kuendelea kuipambania nembo ya IAA na jiji la Arusha msimu ujao kwenye mashindano ya Championship
IAA SC katika safari yake ya mafanikio haya ilifanikiwa kuibuka washindi wa ligi ya Wilaya ya Arusha, Ligi ya Mkoa, Ligi ya mabingwa wa Mikoa yote Tanzania na baadae Ligi daraja la pili (First League) na leo imefanikiwa kufuzu kutinga katika ligi daraja la kwanza (Championship) msimu wa mwaka 2026/2027

Post A Comment: