Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Kassim Mchatta, amesema chanjo zinazozalishwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) zimeendelea kuthibitisha ubora wake kwa kusaidia kudhibiti magonjwa mbalimbali ya mifugo na kuongeza tija kwa wafugaji nchini.

Bw. Mchatta alitoa kauli hiyo tarehe 9 Julai 2026 alipotembelea banda la TVLA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, Dar es Salaam, ambapo alipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TVLA pamoja na kuona aina za chanjo zinazozalishwa kwa ajili ya kuboresha afya ya mifugo.

"TVLA inaendelea kufanya kazi kubwa ya kulinda afya ya mifugo. Chanjo zake ni bora na zimeonyesha matokeo mazuri kwa wafugaji wengi, hivyo ni muhimu wananchi waendelee kuzitumia ili kuongeza uzalishaji na kuchangia maendeleo ya sekta ya mifugo."

“Serikali itaendelea kuhamasisha wafugaji kutumia chanjo zetu za mifugo kwa kuwa zimefanyiwa tafiti za kisayansi, zina ubora unaokidhi viwango na zimekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza milipuko ya magonjwa ya mifugo nchini” amesema Bw. Mchatta.

Akimkaribisha Katibu Tawala katika banda la TVLA, Mtaalamu wa Maabara wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania, Bw. Henry Mlundachuma, alisema TVLA ina jukumu la kufanya uchunguzi wa magonjwa ya mifugo, kuzalisha na kusambaza chanjo, kufanya tafiti za mifugo, kusajili na kuhakiki ubora wa viuatilifu vya mifugo pamoja na kutoa huduma za ushauri na mafunzo kwa wadau wa sekta hiyo.

Alieleza kuwa katika maonesho hayo, TVLA imekuwa ikitoa elimu kwa wafugaji na wananchi kuhusu matumizi sahihi ya chanjo, umuhimu wa uchunguzi wa magonjwa kabla ya tiba, pamoja na huduma za maabara zinazosaidia kubaini magonjwa mbalimbali ya mifugo kwa wakati.

Bw. Mlundachuma aliongeza kuwa matumizi ya chanjo bora na huduma za kitaalamu za TVLA ni nguzo muhimu katika kuimarisha afya ya mifugo, kuongeza uzalishaji wa nyama, maziwa na mayai, pamoja na kuimarisha usalama wa chakula na uchumi wa wafugaji.

Banda la TVLA limeendelea kuvutia idadi kubwa ya wageni wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba, ambapo wamekuwa wakipata elimu kuhusu huduma mbalimbali za Wakala na namna zinavyochangia maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.

Matukio mbalimbali katika picha: Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Kassim Mchatta, akitembelea banda la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, Dar es Salaam, tarehe 9 Julai, 2026. Katika ziara hiyo alipokea maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TVLA, ikiwemo uzalishaji wa chanjo za mifugo, uchunguzi wa magonjwa ya mifugo, huduma za maabara, uhakiki wa ubora na usajili wa viuatilifu vya mifugo, pamoja na tafiti zinazolenga kuboresha afya za mifugo nchini.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: