Na. Josephine Majura, WF, Dodoma
Wizara ya Fedha imezitaka kampuni na taasisi zinazotoa bidhaa na huduma kwa Wizara kuendelea kuzingatia viwango vya ubora, uaminifu, uwazi na masharti ya mikataba ili kuhakikisha Serikali inapata thamani halisi ya fedha katika matumizi ya rasilimali za umma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tathmini ya Mwaka 2025/26 cha Utendaji wa Wazabuni na Watoa Huduma kwa Wizara ya Fedha kilichofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda, alisema kuwa Wizara inatarajia kuona maboresho makubwa katika utoaji wa bidhaa na huduma, hususan katika maeneo ya ubora, ufanisi na matumizi ya teknolojia za kidijitali.
Alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mikataba mbalimbali, bado kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara na watoa huduma ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza na kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
“Tunatarajia wazabuni na watoa huduma kuendelea kuzingatia viwango vya ubora vilivyokubalika, kuwasilisha bidhaa na huduma kwa wakati, pamoja na kuzingatia maadili ya kitaaluma na taratibu zote za ununuzi wa umma,” alisema Bw. Mwenda.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kujenga na kudumisha uhusiano wa kikazi unaozingatia uaminifu na uwazi, akieleza kuwa misingi hiyo ndiyo msingi wa mafanikio katika utekelezaji wa mikataba ya Serikali.
Wizara pia imeeleza kuwa itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wazabuni na watoa huduma ili kuhakikisha mikataba inatekelezwa kwa ufanisi na changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Wizara ya Fedha, Bw. Boaz Ntembanda, alisema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikataba ya wazabuni na watoa huduma, kubaini changamoto zilizojitokeza na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utoaji wa bidhaa na huduma kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia masharti yaliyokubaliwa.
Naye mmoja wa wwaakilishi wa wazabuni wanaotoa huduma Wizara ya Fedha, Bi. Happiness Kategile, aliipongeza Wizara kwa kuwakutanisha pamoja wazabuni na watoa huduma, akisema hatua hiyo imefungua fursa ya kujadiliana kwa uwazi, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa mikataba.
Katika kikao hicho, washiriki walipata fursa ya kujadili utekelezaji wa mikataba, ubora wa huduma zilizotolewa, matumizi ya TEHAMA katika mifumo ya ununuzi na ugavi, pamoja na masuala ya mazingira, jamii na utawala bora katika shughuli za ununuzi wa umma.









Post A Comment: