Na: OWM (KAM)
Tanzania imeshiriki kikao cha Kamati ya Utekelezaji wa Viwango vya Kazi kinachoendelea jijini Geneva, Uswisi, ikiwa ni sehemu ya Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Katika kikao hicho kilichifanyika leo Juni 2, 2026 wajumbe wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa viwango vya kazi, ikiwemo mjadala wa jumla kuhusu ripoti kuu ya Kamati ya Mkutano na maadhimisho ya miaka 100 ya ajenda ya Kazi zenye Staha, Tathmini ya Jumla, pamoja na wajibu wa nchi wanachama katika kuwasilisha taarifa na kutekeleza majukumu mengine yanayohusiana na viwango vya kazi.
Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho ulijumuisha Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina, Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Suzan Mkangwa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Usekelege Mpulla.
Tanzania, ambayo ni mwanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) na mjumbe wa Bodi ya Magavana inayowakilisha nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki, inaendelea kushiriki Mkutano Mkuu wa 114 wa shirika hilo unaowakutanisha wawakilishi wa Serikali, Waajiri na Wafanyakazi kutoka nchi wanachama 187.






Post A Comment: