Na Mwandishi Wetu, Muheza

Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Ayoub Sebabili, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika shughuli za mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2026, akisema ushiriki mkubwa wa wananchi utasaidia wilaya hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya Kitaifa ya Mwenge wa Uhuru.

Sebabili ametoa wito huo wakati wa zoezi la Jogging lililoandaliwa kama sehemu ya maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, ambapo aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki shughuli hiyo.

Alisema Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili wilayani Muheza Juni 23, 2026 ukitokea Wilaya ya Mkinga na kupokewa katika eneo la Kilapura, huku ukitarajiwa kulala katika Uwanja wa Jitegemee.

"Niwashukuru kwa namna mlivyojitokeza leo. Ushiriki wenu unaonyesha dhamira ya kuhakikisha Muheza inafanya vizuri katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru. Kila mmoja wetu awe balozi wa kuhamasisha wananchi wengine kujitokeza kwa wingi," alisema Sebabili..

Kwa upande wake, Mratibu wa Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Muheza alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kuwa viongozi katika ngazi zote wamepewa jukumu la kuhamasisha wananchi wa makundi mbalimbali, wakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli hizo.

Alisema Mwenge wa Uhuru utapitia maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuzindua na kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kutoa ujumbe wa umoja, uzalendo na mshikamano wa kitaifa.

Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa, Mwenge wa Uhuru utaanzia Kata ya Mlingano kabla ya kuelekea Machemba kwa uzinduzi wa mradi na ukaguzi wa banda la lishe litakaloonyesha juhudi za Halmashauri ya Muheza katika kupambana na utapiamlo, malaria na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Baadaye utaelekea katika Shule ya Venance Mabeyo na Kata ya Mpapayu kwa ajili ya uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katika Kata ya Genge, Mwenge wa Uhuru utazindua maabara katika Shule ya Sekondari Chief Mang'enya iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa madarasa mapya kwa ajili ya maandalizi ya wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2027.

Mratibu huyo alisema pia kutakuwa na shughuli za Klabu ya Wapinga Rushwa pamoja na programu mbalimbali za elimu kwa jamii.

Katika Kata za Magila na Majengo, Mwenge wa Uhuru utatembelea kikundi kilichonufaika na mkopo wa asilimia 10 wa Halmashauri unaotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo kikundi hicho kimepata Sh25 milioni kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, katika eneo la Mikwamba kutakuwa na maonesho ya fursa za zabuni kupitia PPRA, yakilenga kuhamasisha vikundi maalumu kushiriki katika zabuni zinazotengwa kwa makundi hayo.

Ratiba hiyo itahitimishwa kwa shughuli mbalimbali katika Kata ya Tongwe na eneo la Mpaa, ikiwemo uzinduzi wa daraja la karavati, uzinduzi wa Jengo la Havest Inn na mkesha wa Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa Jitegemee.

Viongozi hao wamewataka wananchi kuzingatia amani, utulivu na usalama katika kipindi chote cha shughuli hizo, huku wakisisitiza kuwa vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani havitavumiliwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) wa Muheza, Mohamed Mfaki, aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao katika maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na kuwataka kuendelea kushiriki kikamilifu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Dk Juma Mhina, alisema wilaya hiyo imejipanga kufanya vizuri zaidi mwaka huu na inalenga kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru


Alisema maandalizi yaliyoanza mapema chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya yanalenga kuongeza ushiriki wa wananchi na kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa mafanikio makubwa.

"Malengo yetu ni kuona wananchi wanajitokeza kwa wingi katika shughuli zote za Mwenge wa Uhuru. Tunataka Muheza iwe mfano wa mafanikio na ushirikiano katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2026," alisema Dk Mhina.


Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: