Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amewanasihi watumishi wa wakala kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kufuata miongozo ya utumishi wa umma kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo.
Ametoa rai hiyo Jijini Dodoma Mei 15, 2026 katika kikao kazi na watumishi wote wa Wakala ambapo amewanasihi kuimarisha usimamizi wa miradi na kuwa sehemu ya miradi sambamba na kuimarisha mawasiliano na viongozi wa Serikali maeneo ya mradi.
“Tusirudi nyuma, tusilewe sifa tufikirie mambo makubwa zaidi. Tuwe wabunifu, tuchape kazi kwa weledi na ushirikiano na hii ndiyo nguzo itakayofanya tuendelee kusonga mbele,” amesema Mha. Saidy.
Mha. Saidy amesema Wakala umejipanga kuhakikisha miradi yote ya kusambaza nishati vijijini inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakikana.
Katika kikao kazi hicho, watumishi walipata fursa ya kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha utendaji wa kazi, kukumbushana kuhusu miongozo mbalimbali ya utumishi wa umma pamoja na kupima afya zao kwa kuwa afya ni msingi wa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Wakati huohuo; Madaktari kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa mwaliko maalum wa Menejimenti ya REA wameendesha zoezi la upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza (moyo; homa ya ini na ugonjwa wa kisukari).
Zoezi hilo lilienda sambamba na utoaji wa chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya ini ambapo Zaidi ya Watumishi 100 walipata huduma hiyo ya kinga.

Post A Comment: