Na Jackline Minja, Dodoma
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kusaidia utekelezaji wa shughuli za Maendeleo na Ustawi wa Jamii nchini.
Akizungumza leo tarehe 15 Mei, 2026 wakati wa uwasilishaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Mahundi amesema mashirika hayo yamekuwa yakisaidia wananchi kupitia afua mbalimbali za kijamii na kiuchumi ambapo mchango wao mkubwa katika kusaidia juhudi za Serikali kuwafikia wananchi kupitia miradi ya maendeleo inayogusa maisha yao ya kila siku.
“Shirika la Hand in Hand Eastern Tanzania (TZ) ni Shirika la Kimataifa lenye Makao yake makuu jijini Arusha ambalo linajishughulisha na afua za kuwawezesha wananchi kiuchumi katika Mikoa saba (7) nchini ambayo ni Dodoma, Simiyu, Arusha, Singida, Manyara, Kilimanjaro na Iringa na Shirika hili linalenga kuinua jamii na kuiwezesha kupitia biashara na ajira endelevu.” amesema Mhe. Mahundi
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hand in Hand Eastern Africa Tanzania, Jane Richard Sabuni, amesema shirika hilo linaendelea kuweka nguvu katika kuwawezesha wananchi kujitegemea kupitia mafunzo ya ujasiriamali na ukuzaji wa biashara ndogondogo.
“Lengo letu ni kuona jamii inakuwa na uwezo wa kujitegemea kiuchumi kwa kuwapa wananchi maarifa, ujuzi na fursa za maendeleo zitakazoboresha maisha yao hivyo tutazidi kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha wanawake, vijana na makundi maalum wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali” amesema Jane.
Nao baadhi ya wabunge waliohudhuria semina hiyo wamepongeza mashirika hayo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuongeza ufanisi wa maendeleo ya jamii pamoja na kusaidia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Post A Comment: