Mbunge wa Jimbo la Mbinga vijijini na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuleta mageuzi makubwa katika sekta za elimu na afya hasa maeneo ya Jimbo hilo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza Leo Mei 15, 2026 katika Kijiji cha Mapera, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi wa vyumba vinne vya madarasa uliofanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa.

Amesema Serikali imeendelea kutoa ruzuku kwa shule za msingi na sekondari jambo linalowezesha wanafunzi kupata elimu bila kulipa ada, huku ikiendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kupitia ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine muhimu.

“Serikali ya Rais Samia imeonyesha dhamira ya kweli ya kuwekeza katika elimu na maendeleo ya wananchi, hii ndiyo sababu miradi ya elimu inaendelea kutekelezwa kwa kasi katika maeneo mbalimbali.”

Aidha, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kutumia sehemu ya mapato yake ya ndani kugharamia ujenzi wa madarasa, ameeleza kuwa halmashauri hiyo hukusanya zaidi ya shilingi bilioni 13 kwa mwaka na hutenga kiasi cha fedha kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Pamoja na hilo, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto shule ili waweze kunufaika na fursa za elimu zinazotolewa na Serikali, pamoja na kuwasimamia watoto wao waende shule kupata elimu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kapinga amemshukuru Kiongozi wa Mbio za Mwenge kwa kukubali kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mbinga Vijijini wenye thamani ya shilingi bilioni 3.7.

Amesema Serikali imeahidi kuongeza shilingi bilioni moja katika mwaka wa fedha ujao kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma na mazingira ya hospitali hiyo.

Akiwa Kata ya Maguu, Mhe. Kapinga amewaomba wananchi wa Mbinga Vijijini kuendelea kuwa na imani na Serikali ya awamu ya sita, kutokana na maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta ya kilimo kwa kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati, hususan kwa zao la kahawa licha ya changamoto zilizopo, wananchi wanaendelea kuwa wanufaika wakubwa.

Kwa upande wake Wazo Michael Mwang’onda kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2026, amewapongeza viongozi wa Halmashauri pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, amehimiza upendo na mshikamano kama Taifa chini ya kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Tanzania ni yetu sote tushirikiane kwa pamoja kuleta Maendeleo”.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: