NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAHITIMU wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) (alumni) wametakiwa kutumia nafasi zao kuchangia maendeleo ya taifa kupitia taaluma, uzoefu na rasilimali walizonazo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Shule ya Mwalimu Nyerere Kibaha Prof. Marcellina Chijoriga wakati akizungumza katika hafla ya Alumni Breakfast iliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo alieleza kuwa alumni ni rasilimali muhimu ya kimkakati kwa maendeleo ya elimu na uchumi.
Amesema mafanikio ya taifa hayawezi kutegemea juhudi za Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo alumni wenye mchango mkubwa katika jamii.
“Alumni si wahitimu wa zamani tu, bali ni nguvu ya mabadiliko. Kila mmoja ana jukumu la kuendelea kutoa mchango wake katika kujenga taifa,” amesema Prof. Chijoriga.
Amebainisha kuwa alumni wana nafasi kubwa ya kusaidia maendeleo ya wanafunzi na taasisi kupitia ushauri wa kitaaluma, kuwezesha upatikanaji wa mafunzo kwa vitendo, ajira, pamoja na kushiriki katika tafiti na ubunifu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ujasiriamali kwa wahitimu, akiwahimiza kufikiria zaidi ya kuajiriwa na badala yake kuanzisha biashara zitakazochochea ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda Lwoga, amesema alumni wana nafasi ya kipekee ya kuwa daraja kati ya elimu ya darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira.
“Ushiriki wenu unaweza kubadilisha maisha ya wanafunzi wengi. Hata nafasi moja ya mafunzo kwa vitendo inaweza kuwa mwanzo wa mafanikio ya kijana,” amesema Prof. Lwoga.
Ameongeza kuwa ushiriki wa alumni katika shughuli za maendeleo ya chuo, ikiwemo kuchangia rasilimali, kusaidia ufadhili wa masomo na kutoa ushauri wa kimkakati, ni muhimu katika kuboresha mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la ajira.
Pia amesisitiza umuhimu wa mitandao na ushirikiano, akieleza kuwa kupitia alumni, chuo kinaweza kupanua wigo wa ushirikiano wa kitaifa na kimataifa pamoja na kukuza tafiti na ubunifu.
Kadhalika, alumni wanaojishughulisha na biashara wametakiwa kuhamasisha ujasiriamali kwa wanafunzi ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine.
Hafla hiyo iliwakutanisha wahitimu mbalimbali wa chuo hicho kutoka sekta tofauti, ambapo walipata fursa ya kubadilishana uzoefu, mawazo na kuweka mikakati ya pamoja ya kuchangia maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla.
Nao wahitimu waliomaliza katika Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) Ally Mayai Tembele na Jackline Michael wamesema Huwa wanakutana Kila mwaka lengo ni kutengeneza Umoja na kuitumia uzoefu waliopo nao ili kuwanufaisha wanafunzi walipo vyouni na Chuo kwa Ujumla

Post A Comment: