Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema Serikali imetenga kiasi cha Sh Bilioni 3.2 kupitia kwa Wakala  wa Nishati Vijijini (REA) kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji vilivyopo ndani ya vijiji Tisa vya Kitewele, Kimata, Ndoa, Chanjale, Nkanda, Lumbila, Nsele na Kilondo vilivyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe ambapo mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 2026.

Mhe. Salome ameyasema hayo leo Aprili 17, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Ludewa, Mhe. Joseph Kamonga aliyehoji ni lini Vijiji hivyo vitawashiwa umeme.

" Kwa kutambua changamoto ya Jiografia na ugumu wa kufikisha vifaa katika maeneo hayo, tumempatia kazi hiyo Mkandarasi M/s SUMA JKT Electric Co. Ltd ambaye tumemuelekeza kufanya kazi kama Jeshi na kuhakikisha kuwa azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufungamanisha nishati na maendeleo ya kiuchumi inatimia," Amesema Mhe. Salome.

Aidha Mhe. Salome ameiagiza REA kumsimamia Mkandarasi huyo ili aweze kutimiza majukumu yake ili kuhakikisha wananchi wa Ludewa wananufaika na uwepo wa nishati imara na uhakika.

Share To:

Post A Comment: