Waziri Wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Na.Alex Sonna-Dodoma

Serikali imeandika historia mpya katika sekta ya uwekezaji baada ya kusajili miradi 915 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 10.95 mwaka 2025, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa usajili wa miradi ya uwekezaji mwaka 1996.

Hayo yameelezwa leo Aprili 16,2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri Wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Prof.Mkumbo amesema kuwa  mafanikio hayo yanaakisi ukuaji mkubwa wa sekta ya uwekezaji nchini, ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, idadi ya miradi imeongezeka kutoka 256 mwaka 2021 hadi 915 mwaka 2025—sawa na ongezeko la asilimia 257.4.

Amesema  hatua hiyo ni ishara ya kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji, sambamba na juhudi za makusudi za kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

"Tanzania pia imeanza kupanua uwekezaji wake nje ya mipaka. Takwimu za awali zinaonyesha kuwa kampuni za Kitanzania zimewekeza zaidi ya dola bilioni 3.1 katika nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Afrika Kusini, Japan na Qatar. Uwekezaji huo unalenga kupanua masoko, kuongeza ushindani na kuchochea uhamishaji wa teknolojia."amesema Prof.Mkumbo

Hata hivyo amesema kuwa Sekta zinazoongoza katika uwekezaji huo wa nje ni pamoja na viwanda vya chakula na vinywaji, nishati, usafirishaji, huduma za kifedha na vyombo vya habari.

Katika hatua nyingine, Serikali imekamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 na kuandaa sera mpya ya mwaka 2026 inayosubiri kuidhinishwa. Sera hiyo inalenga kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuweka mkazo kwenye upatikanaji wa ardhi, vivutio vya uwekezaji, ubunifu na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Sambamba na hilo, Mkakati wa Taifa wa Uwekezaji wa mwaka 2026–2031 umeandaliwa ili kutafsiri sera hiyo katika vitendo, kwa kuainisha vipaumbele na hatua mahsusi za kukuza uwekezaji wenye tija kwa uchumi wa taifa.

Katika kuimarisha ulinzi wa uwekezaji, Tanzania imeendelea kusaini mikataba ya kimataifa ya uwekezaji, ambapo hadi Machi 2026 jumla ya mikataba 20 ilikuwa imesainiwa, huku mingine ikiendelea kujadiliwa na nchi mbalimbali ikiwemo Japan, Canada na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Aidha, Serikali imeongeza kasi ya maendeleo ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ), ambapo miradi 19 yenye thamani ya dola milioni 331.51 imesajiliwa na kutarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 11,700 pamoja na kuongeza mauzo ya nje.

Katika maeneo hayo, uwekezaji umeelekezwa kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, uzalishaji wa bidhaa za chuma, dawa na hata uunganishaji wa magari kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Serikali pia imeendelea kuboresha huduma kwa wawekezaji kupitia Kituo cha Pamoja cha Uwezeshaji Uwekezaji (OSFC), ambapo idadi ya taasisi zinazotoa huduma imeongezeka na kurahisisha upatikanaji wa vibali na nyaraka muhimu kwa wawekezaji.

Katika jitihada za kuimarisha uchumi, mapato yasiyo ya kodi kutoka mashirika ya umma yameongezeka na kufikia shilingi bilioni 773.37 hadi Machi 2026, ikiwa ni asilimia 85 ya lengo la kipindi hicho. Serikali pia imeongeza uwekezaji wake katika mashirika ya umma hadi kufikia shilingi trilioni 90.61.

Pamoja na mafanikio hayo, Serikali imeendelea kufanya mageuzi ya kimuundo kwa kufuta na kuunganisha baadhi ya mashirika ya umma ili kuongeza ufanisi na tija.

Hatua nyingine muhimu iliyochukuliwa ni kuboresha mazingira ya biashara kupitia mpango wa MKUMBI, ambapo sheria 28 zimefanyiwa mapitio na tozo 245 zimeondolewa au kupunguzwa ili kupunguza gharama kwa wafanyabiashara.

Serikali imesisitiza kuwa mageuzi haya yanalenga kujenga mazingira rafiki, yenye ushindani na yanayovutia uwekezaji zaidi, huku yakichochea ukuaji wa uchumi na ajira kwa Watanzania.

Amesema kuwa mwelekeo wa sasa unaonyesha kuwa Tanzania inaendelea kujijenga kama kitovu muhimu cha uwekezaji barani Afrika, huku mikakati mipya ikiweka msingi imara wa kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu ifikapo mwaka 2050.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Alex Sonna

Post A Comment: