Samia Suluhu Hassan amesema idadi ya hospitali zinazotoa huduma za upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu (neurosurgery) imeongezeka kutoka hospitali mbili hadi saba kufikia Aprili 2026, hatua inayoakisi uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya.

Rais Samia ametoa kauli hiyo Aprili 16, 2026 wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu uliofanyika katika Julius Nyerere International Convention Centre.
 
Amesema ongezeko hilo linaashiria mabadiliko makubwa ya Tanzania kutoka kuwa na uwezo mdogo wa huduma za neurosurgery hadi kufikia mfumo imara, endelevu na unaojitegemea katika utoaji wa huduma za kibingwa.

“Hatua hii inaonesha mabadiliko ya Tanzania kuelekea katika mfumo imara wa huduma bora za upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu,” amesema Rais Samia.

 

Aliongeza kuwa uwekezaji huo umewezesha kuongezeka kwa idadi ya upasuaji unaofanyika nchini pamoja na kuboresha matokeo ya matibabu kwa wagonjwa katika hospitali mbalimbali.
Rais Samia alieleza kuwa Serikali imefanikiwa kuimarisha rasilimali watu katika sekta ya afya, ambapo idadi ya madaktari bingwa imeongezeka kutoka 1,038 mwaka 2020 hadi 1,338 Aprili 2026.

Aidha, wataalamu wa neurosurgery wameongezeka mara tatu kutoka 12 hadi 37, hatua inayochangia kuokoa maisha ya wananchi wengi zaidi, hususan wanawake na watoto wanaohitaji huduma za dharura.

Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuhimiza matumizi ya ujuzi wa kitaalamu na kuongeza fursa kwa wanawake katika sayansi, teknolojia na fani za kibingwa ili kuleta maendeleo jumuishi.

Alitaja mipango inayochangia mafanikio hayo kuwa ni pamoja na Samia Scholarship and Fellowship Programme pamoja na ushirikiano wa kimataifa kupitia CECTA na World Federation of Neurosurgical Societies.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema maboresho yaliyofanywa katika sekta ya afya yamechangia kurejesha imani ya wananchi.

Ameeleza kuwa uwekezaji huo umeboresha miundombinu ya afya, kuongeza vifaa tiba na kupanua huduma muhimu ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

“Sekta ya afya imepiga hatua kutoka mfumo wa kutibu magonjwa pekee hadi kuwa nguzo ya kulinda utu wa binadamu na kuchochea maendeleo ya taifa,” amesema Mchengerwa.

Ameongeza kuwa tathmini za hivi karibuni zinaonesha kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma hata katika maeneo ya mbali, kupungua kwa changamoto za tiba, na kuimarika kwa imani ya wananchi kwa watoa huduma za afya.


Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: