Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP Centre) kimesema mafanikio ya utekelezaji wa ajenda ya ubia nchini yameongeza kwa kiasi kikubwa thamani ya miradi ya maendeleo, huku kikitoa wito wa kufanyiwa maboresho kwa Sheria ya Utumishi wa Umma ili kuongeza uwajibikaji na kulinda maslahi ya walipa kodi.
Akizungumza katika kikao cha kawaida cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika jana, uongozi wa PPP Centre uliwapongeza watumishi kwa mchango wao katika kuifanya ajenda ya ubia (PPP) kueleweka kwa kasi miongoni mwa umma na katika mfumo mzima wa Serikali.
Ilielezwa kuwa juhudi hizo zimeifanya PPP kutambuliwa rasmi kama moja ya nguzo muhimu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Muda Mrefu na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV).
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaanza, thamani ya miradi ya PPP ilikuwa dola za Marekani bilioni moja, sawa na takribani shilingi trilioni 2.5, kwa mujibu wa Mkakati wa Ugharamiaji wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26. Hata hivyo, ndani ya kipindi cha miaka minne, thamani hiyo imeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 8.5, hatua inayoashiria ukuaji mkubwa wa sekta hiyo.
Pamoja na mafanikio hayo, uongozi huo uliibua hoja kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma, ukieleza kuwa licha ya dhamira yake ya awali ya kulinda watumishi dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka, kwa sasa sheria hiyo imeonekana kuwa na changamoto zinazoweza kuathiri ufanisi na kuongeza gharama kwa walipa kodi.
Ilibainishwa kuwa mchakato wa kuwaondoa watumishi wasio na tija nchini Tanzania ni mrefu na mgumu, hali inayosababisha baadhi yao kuendelea kubaki katika mfumo wa utumishi kwa muda mrefu licha ya utendaji hafifu.
Katika kulinganisha, mfano ulitolewa wa nchi ya Botswana ambako mtumishi anayebainika kuwa na utendaji mbovu kwa miaka miwili mfululizo huondolewa kazini mara moja, na endapo atakata rufaa hubaki nje ya mfumo wa utumishi hadi rufaa itakapokamilika. Kwa Tanzania, mtumishi huendelea kubaki kazini hadi rufaa zote zitakapokamilika.
Aidha, ilielezwa kuwa mchakato wa kumfukuza mtumishi nchini unaweza kuchukua hadi miezi 22, ilhali katika nchi hiyo ya Botswana huchukua takribani miezi mitatu kukamilika.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Machi 2024, kati ya watumishi 1,124 waliothibitika kuwa na utendaji hafifu kwa miaka miwili mfululizo katika mwaka wa fedha 2022/23, ni watumishi 138 pekee sawa na asilimia 12 waliofukuzwa kazi. Hali hii inaelezwa kuchangiwa na mifumo ya rufaa inayowapa nafasi kubwa watumishi husika.
Kwa upande wa Botswana, katika kipindi hicho hicho, watumishi 214 kati ya 241 waliothibitika kuwa na utendaji hafifu, sawa na asilimia 88, waliondolewa kazini, hatua inayotajwa kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utumishi wa umma.
Uongozi huo ulisisitiza kuwa uwepo wa watumishi wasio na tija unaigharimu Serikali na walipa kodi kwa kiwango kikubwa, hivyo kuna umuhimu wa kuweka uwiano kati ya ulinzi wa haki za watumishi na uwajibikaji kwa umma.
Aidha, ulirejea ripoti ya Oxford Review ya mwaka 2014 inayoonesha kuwa takribani asilimia 25 ya ukuaji wa uchumi katika mataifa 13 makubwa duniani unatokana na ufanisi wa taasisi, ambao kwa kiasi kikubwa unategemea ubora wa rasilimali watu, hususan watumishi wa umma.
Kwa msingi huo, watumishi walihimizwa kuongeza uwajibikaji, nidhamu na tija katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wito ukitolewa kuhakikisha kuwa sheria zinazolinda watumishi haziwi kikwazo kwa maendeleo bali zinachangia ufanisi na utoaji bora wa huduma kwa wananchi.





Post A Comment: