Benki ya Ushirika (Coop Bank) imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kukuza uchumi jumuishi kwa kuongeza kiwango cha mikopo kwa sekta ya kilimo, hususan kwa wakulima, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kupanua huduma za kifedha kwa makundi ambayo hayajafikiwa kwa urahisi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ng’urah, amesema hatua hiyo inalenga kuongeza tija kwa wakulima na kuchochea uzalishaji, huku benki ikijiweka kama mshirika muhimu katika maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Ng’urah ameeleza kuwa mafanikio ya benki hiyo ndani ya mwaka mmoja tangu kuzinduliwa kwake yamechangiwa na utekelezaji madhubuti wa mkakati wa muda wa kati, uliowezesha kuimarika kwa huduma na kuongezeka kwa imani ya wateja.
Kwa mujibu wa takwimu za robo ya kwanza ya mwaka 2026, kitabu cha mikopo kimefikia shilingi bilioni 101.02 kutoka bilioni 16.6 mwaka uliopita, sawa na ukuaji wa asilimia 506, hatua inayoonyesha kupanuka kwa wigo wa utoaji mikopo kwa sekta mbalimbali za uchumi.
Sambamba na hilo, benki imeonyesha ukuaji mkubwa katika viashiria vingine muhimu vya kifedha, ambapo jumla ya mali zimeongezeka hadi shilingi bilioni 178.7 kutoka bilioni 46.8 mwaka 2025, huku amana za wateja zikifikia shilingi bilioni 101.5 kutoka bilioni 12.5, ikiwa ni ongezeko la asilimia 709.
Aidha, idadi ya wateja imeongezeka hadi zaidi ya 37,000 kutoka 5,000 katika kipindi kama hicho, jambo linalodhihirisha kuongezeka kwa uaminifu na matumizi ya huduma za benki hiyo.
Katika kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, Ng’urah amesema benki imezindua huduma za kidijitali zikiwemo Coopesa, Coop Net na Coop Wakala ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengi zaidi.
Ameongeza kuwa benki inalenga kufikia familia milioni 10 zisizo na huduma rasmi za kifedha, huku mipango ya kufungua matawi mapya katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Kagera ikiendelea, sambamba na kuwekeza zaidi katika teknolojia kwa ajili ya upatikanaji wa huduma kwa urahisi na gharama nafuu.




Post A Comment: