Na Mwandishi wetu- Dodoma
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu imeendelea na hatua ya tatu ya kujengewa uwezo wa namna ya kufanya tathmini za programu na miradi kupitia programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ili kuwawezesha watalaam wa ufuatiliaji na tathmini kupata uelewa na namna ya kutathmini miradi na programu mbalimbali zinazotekelezwa katika taasisi za umma.
Hayo yamesemwa leo tarehe 16 Machi 2026, jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bi. Sakina Mwinyimkuu wakati akifungua mafunzo yanayofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma yakihusisha washiriki kutoka wizara zinazotekeleza program ya ASDP II na washiriki kutoka nchini Zimbabwe na Malawi kwa lengo la kujifunza chini ya Twendembele Initiative ambapo Tanzania ni mshirika.
Bi. Sakina amewasisitiza washiriki kuzingatia mafunzo kwani yatawasaidia katika kuimarisha eneo la tathmini kwa ujumla yanayotolewa na Watathmini wazawa wa Kampuni ya Auxim na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine mkoani Morogoro huku yakiratibiwa na Clear Initiatives kwa ufadhili kutoka Global Evaluation Initiative iliyopo chini ya Benki ya Dunia.
“Mabadiliko ya sekta ya kilimo yanaendelea kuwa msingi wa mikakati ya maendeleo katika Afrika Mashariki na Kusini, ambapo mifumo ya kilimo cha wakulima wadogo ina jukumu muhimu katika kudumisha maisha ya vijijini, kuhakikisha usalama wa chakula, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kitaifa” amesema Mkurugenzi huyo.
Ameongeza kuwa, mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) unasimama kama mpango wa ushirikiano wa wadau wengi, ukiwa na lengo la kuongeza uzalishaji wa kilimo, kukuza ujumuishaji wa masoko, kuendeleza uendelevu wa mazingira, na kuimarisha ushiriki jumuishi wa kiuchumi miongoni mwa wakulima wadogo na jamii za vijijini.
“Mnamo Desemba 2024, Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Sera, Mipango na Uratibu (PMO-PPCD) iliingia katika ushirikiano na kituo cha kujifunza kuhusu tathmini na matokeo – Afrika ya Anglophone (CLEAR-AA) cha Global Evaluation Initiative (GEI) katika Wits School of Governance pamoja na Taasisi ya Ujerumani ya Tathmini ya Maendeleo (DEval) ili kufanya tathmini ya matokeo ya ASDP II,” ameongeza.
Vilvile amefafanua kwamba, ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya makusudi ya kuzingatia viwango vya kimataifa vya tathmini huku ukihakikisha kuwa mchakato wa tathmini unabaki katika umiliki wa kitaifa na unachangia kujifunza kwa taasisi.
“Mfumo huu wa ushirikiano umeundwa kuunganisha umakini wa kitaalamu, uimara wa mbinu, na mbinu bora za kimataifa, huku ukihakikisha kuwa serikali zinazoshiriki zinabaki na umiliki kamili wa mchakato na matokeo yake,” alieleza Mkurugenzi huyo.
Pia ameeleza kwamba, warsha hiyo inawaleta pamoja wawakilishi kutoka nchi mbalimbali. wakiwemo wadau wakuu wa kitaasisi ambao ni pamoja na Serikali ya Tanzania, inayowakilishwa na PMO-PPCD na Wizara zinazoongoza Sekta ya Kilimo zinazohusika katika utekelezaji wa program, Serikali ya Zimbabwe kupitia Ofisi ya Rais na Baraza la Mawaziri – Kurugenzi ya Tathmini, Kujifunza na Utafiti, na Serikali ya Malawi, inayowakilishwa na Wizara ya Fedha, Mipango ya Uchumi na Ugatuzi.
“Mtandao wa kikanda wa tathmini wa Twende Mbele unashiriki pia, ukichangia utaalamu wa kulinganisha na kuwezesha ujifunzaji wa pamoja kati ya mifumo ya tathmini barani Afrika. Muundo huu wa utawala wa wadau wengi unaonyesha dhamira inayokua ya kikanda ya kuingiza utamaduni wa tathmini ndani ya mifumo ya kitaifa,” amesema.
Aidha, ameeleza kwamba sifa mojawapo muhimu ya tathmini inayoongozwa na Nchi (Country-Led Evaluation) ni ujumuishaji wa makusudi wa maendeleo ya uwezo wa kitaasisi kama sehemu kuu ya mchakato, badala ya kuwa shughuli ya ziada kwani maendeleo endelevu katika utawala unaotumia ushahidi hayategemei tu uzalishaji wa matokeo ya tathmini, bali pia kuimarisha uwezo wa taasisi kuagiza, kusimamia na kutumia tathmini kwa muda mrefu.









Post A Comment: