
Wananchi na wakazi wa Hydom wilayani Mbulu mkoa wa Manyara wamemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia Wizara ya Maji kupitia RUWASA kutekeleza mradi mkubwa wa Majisafi ya bomba wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 41 na tayari vijiji vinne vimeshaanza kunufaika na mradi huo.
Wametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira alipotembelea na kukagua mradi huo ikiongozwa na Mwemyekiti wake Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) katika eneo la Hydom lilipo tangi kubwa la ujazo wa lita 2,000,000 la mradi huo.

Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mha. Wolta Kirita aliieleza Kamati hiyo kuwa tayari wananchi zaidi 800 wameshasajiliwa na kupatiwa kadi za malipo kabla ya matumizi kwani mradi huo unaenda sambamba na ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla, ambapo mwananchi anaweza kuchota maji kwenye kituo muda wowote anapokuwa anahitaji huduma hiyo.
Mkurugenzi Mkuu Kirita alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika Novemba 2027.
Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA mkoa wa Manyara Mha. James Kionaumela alisema mradi huo umeshaanza kutoa huduma katika vijiji vinne na ukikamilika utahudumia zaidi ya wakazi 100,000 wa eneo hilo.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mbulu Mhe. Michael Semindu akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga alisema kwa sasa wananchi wa wilaya hiyo wanapata maji kwa saa 12 kwa siku huku akiipongeza RUWASA kwa kazi nzuri katika kutekeleza mradi huo.










Post A Comment: