Na. Joyce Ndunguru, Dodoma.

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mlage Yussuf Kabange amefungua rasmi kikao kazi cha maandalizi ya bajeti ya TAWA kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichofanyika Machi 13,2026, Jijini Dodoma, Kamishna Kabange amesema Bajeti ya mwaka 2026/27 ni ya kipekee kwa kuzingatia kuwa ni bajeti ya kwanza katika kuchangia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2025 pamoja na Dira ya maendeleo ya Taifa 2050.

“Pia bajeti hii imezingatia kutafsiri Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wa kuzindua Bunge la 13, Mkakati wa kuongeza mapato wa TAWA na ni bajeti ya kwanza tangu Bodi ya Nne ya Wakurugenzi ya TAWA iteuliwe”, amesema Kamishna Kabange.

Kamishna Kabange ameongeza kuwa katika bajeti hii TAWA itajielekeza katika vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuimarisha ulinzi na usimamizi wa Rasilimali wanyamapori na malikale.

Pia, Kuimarisha shughuli za utalii pamoja na kuongeza idadi ya watalii kwa kuboresha miundombinu ya utalii pamoja na kuongeza vyanzo vipya vya mapato.

Kadhalika, Utatuzi wa migogoro ya mipaka na udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na Kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi na uwezo wa Mamlaka katika kutoa huduma.

Vilevile , Kamishna Kabange amewapongeza Makamanda na Askari ambao wamekuwa mstari wa mbele kusimamia utekelezaji wa malengo ya Mamlaka. Aidha, amewaelekeza Makamanda wa vituo kuhakikisha Usimamizi madhubuti wa vitendea kazi yakiwemo magari.

Aidha, Kamishna Kabange amewaelekeza Makamanda kuendelea na utangazaji wa vivutio vya utalii pamoja na kubuni mazao mapya ya utalii.

“Nitoe rai kwenu kuendelea kuwa wabunifu na kutangaza maeneo mnayoyasimamia,” amesema Kamishna Kabange 

Sambamba na hilo, Kamishna Kabange amewaelekeza Makamanda kuendelea kusimamia askari kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia haki, sheria na miongozo iliyowekwa.

Kikao kazi cha maandalizi ya bajeti kimehudhuriwa na viongozi wa TAWA kwa ngazi ya Makao Makuu, Kanda na Vituo.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: