Na Mwandishi Wetu, Handeni

Wanawake katika Halmashauri ya Mji Handeni wametakiwa kutumia simu janja na teknolojia ya kidijitali kwa kuwa ni nyenzo muhimu ya kukuza biashara na kujikwamua kiuchumi kupitia fursa mbalimbali zinazopatikana mtandaoni.

 Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese ameyasema hayo wakati akizindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi katika kongamano la wanawake lililofanyika mjini Handeni.

Amesema matumizi sahihi ya simu janja yanaweza kuwasaidia wanawake kupanua masoko ya biashara zao kupitia mitandao ya kijamii pamoja na kupata taarifa muhimu za fursa za kiuchumi zinazotolewa na serikali.

Nyamwese amesema jukwaa hilo limekuja wakati muafaka kutokana na juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha kiuchumi wanawake na wasichana.

“Jukwaa hili litawawezesha kupata fursa na kujadiliana namna ya kujikwamua. Mtapata mbinu mbalimbali za kuongeza thamani ya biashara zenu na namna ya kuzifikia fursa zinazotolewa na serikali ikiwamo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri,” amesema.

Aidha, amewasisitiza wanawake kuwa wabunifu katika biashara zao na kutumia kikamilifu teknolojia pamoja na mikopo inayotolewa na halmashauri ili kujiongezea kipato.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju amesema halmashauri imeandaa mkakati wa kusaidia vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujiunga kwenye mfumo wa ununuzi wa umma wa NeST ili viweze kunufaika na fursa ya asilimia 30 ya zabuni zinazotolewa kwa makundi hayo.

Amesema kupitia mfumo huo vikundi vitapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika zabuni zinazotangazwa na halmashauri na hivyo kuongeza kipato na kukuza uchumi wao.

Akizungumza kuhusu kongamano hilo, Mkurugenzi huyo amesema katika kongamano hilo wanawake walipata elimu mbalimbali ikiwamo masuala ya fedha, msaada wa kisheria, umiliki wa ardhi pamoja na masuala ya ndoa ili kuwajengea uelewa na kuwasaidia kuwa chachu ya maendeleo ya Handeni.

Aliongeza kuwa elimu hiyo pia inalenga kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Akisoma taarifa ya uendeshaji wa shughuli za majukwaa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, Mratibu wa majukwaa hayo, Carin Umwambe amesema jukwaa hilo linalenga kuwaunganisha wanawake wajasiriamali na watoa huduma katika sekta za umma na binafsi ili waweze kupata fursa mbalimbali za kiuchumi na kibiashara.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Alex Sonna

Post A Comment: