Na Mwandishi Wetu Wetu - DODOMA


Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) imetoa mafunzo ya vipimo kwa wanafunzi wa Dr. Samia Dodoma Secondary School, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi katika biashara na maisha ya kila siku.

Katika zoezi hilo, wanafunzi walipata fursa ya kujifunza kuhusu dhima na majukumu ya Wakala huo, pamoja na namna unavyolinda maslahi ya watumiaji na wafanyabiashara kwa kuhakikisha vipimo vinakuwa sahihi na vya kuaminika.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa WMA, Veronica Simba, amesema elimu ya vipimo itatolewa katika mikoa yote ya Tanzania Bara ili kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wanapata uelewa wa matumizi sahihi ya vipimo.

Amesema mpango huo unalenga kukuza uelewa wa masuala ya vipimo kwa vijana, sambamba na kuimarisha utamaduni wa uadilifu na uwajibikaji katika sekta ya biashara nchini.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma, Said Ibrahim, amesema mafunzo hayo yanaenda sambamba na uanzishwaji wa Klabu za Vipimo mashuleni ili kuendelea kuandaa mabalozi mahiri watakaotoa elimu ya vipimo shuleni na katika jamii kwa ujumla.

“Kwa Dodoma tayari tumeshatoa mafunzo katika shule mbili ambazo ni Shule ya Msingi Mtemi Mazengo na leo tumetoa hapa katika Shule ya Sekondari ya Dkt. Samia Dodoma. Tunaamini mabadiliko katika matumizi ya vipimo sahihi yataongezeka,” amesema Said.

Naye , Mwalimu Mussa Madandi, ambaye pia ni mlezi wa Klabu ya Vipimo shuleni hapo, amesema elimu hiyo wamekuwa wakiifundisha darasani, lakini mafunzo yaliyotolewa na WMA yamewapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kwa vitendo, jambo litakalosaidia kuongeza uelewa na kuimarisha matumizi ya vipimo sahihi.

“Vipimo ni somo tunalolifundisha karibu kila darasa, lakini leo wanafunzi wamepata mafunzo kwa vitendo kutoka kwa wataalamu wenyewe. Naamini hali hii itaongeza hamasa ya kuzingatia usahihi katika matumizi ya vipimo na kuwafanya wawe mabalozi wazuri kwa wazazi wao na jamii inayowazunguka,” amesema Mwalimu Madandi.

Mwanafunzi Itabangola Elias amesema elimu hiyo imewasaidia kuelewa namna ya kutambua vipimo sahihi na kujikinga dhidi ya udanganyifu unaoweza kujitokeza katika biashara.

Baada ya mafunzo hayo, wanafunzi walishiriki kujibu maswali mbalimbali kuhusiana na vipimo na shughuli za Wakala huo, ambapo waliofanya vizuri walipatiwa zawadi mbalimbali kama sehemu ya kuwahamasisha kuendelea kujifunza na kuwa mabalozi wa matumizi sahihi ya vipimo katika jamii.




Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: